Ugomvi Wa Urithi Wa Mama Aliyeacha Mtoto Wa Nje Ya Ndoa Na Kaka Ya Huyo Mama Wanaoshiriki Baba
SWALI:
Mama amekufa ameacha mtoto wa kike mmoja ambaye amemzaa bila ya kuolewa. Na kaacha ndugu zake na ameacha nyumba na vitu ndani yake. Mjomba wa mtoto huyu (ndugu wa mama) anasema urithi ni wake yeye mtoto huyu hana haki ya chochote. Lakini mjomba huyu ni baba mmoja tu na mama huyu mama ni mbali mbali. Jee urithi ni wa mtoto au wa mjomba?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho..
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ugomvi wa mirathi. Ni vigumu kidogo kujibu swali hili kwani muulizaji amesema aliyefariki kaacha ndugu zake. Hawa ndugu ni wangapi – yaani wanawake ni wangapi na waume wangapi? Je, wote ni ndugu kwa baba tu au ni shakiki? Je, wazazi wa aliyefariki wapo hai? Na je, aliyefariki aliolewa na ana mume wakati wa kufa kwake?
Na Allaah Anajua zaidi.
Ufafanuzi:
Mama huyu ameacha ndugu wakike wanne na wakiume mmoja ndo huyu anaetaka mali yote. Ndugu wa kike mmoja ni baba mmoja mama mmoja na huyu mama aliefariki waliobakia ni baba mmoja. Mama huyu hana mume, baba wala mama. Na ameacha huyu mtoto wa kike.
Shukrani kwa ufafanuzi huo ambao umetuletea. Na kwa ufahamu wangu kuhusu ufafanuzi wako inaonekana jamaa za aliyefariki ambao wanaweza kurithi ni kama wafuatao:
- Binti wa mama ambaye anataka kunyimwa urithi.
- Dada 1 shaqiqi.
- Dada 3 kwa baba.
- Kaka 1 kwa baba.
Kwa hiyo, hao walio juu ndio wanajulikana kisheria ndio wanaoweza kurithi. Urithi utakuwa kama ufuatavyo:
- Binti wa nje ya ndoa atarithi nusu ya mali ya mamake.
- Dada shaqiqi (kwa baba na mama) atarithi pia nusu ya mali ya aliyefariki.
- Waliobaki (dada na kaka kwa baba) hawatarithi chochote.
Na Allaah Anajua zaidi