Amali Inayotaqabaliwa
Amali Inayotaqabaliwa
Kutoka: ‘Kitaabul-Ikhlaasw’
Imetarjumiwa Na Iliyaasa
Maana ya Ikhlaasw ni kusafisha niya kutenda amali kwa ajili ya Allaah (‘Azza wa Jalla) bila ya kujionyesha.
Kabla ya kuchukua hata hatua moja, Ee kaka yangu na dada yangu uliye Muislamu, ni muhimu kwako kuijua njia ambayo maokozi yako yatapokuwa. Usijichokeshe kwa kutekeleza mambo mengi (ambayo ndani yake hamna Ikhlaasw). Kwani inaweza kuwa ya kwamba mtu atatenda matendo mengi, lakini hafaidiki na chochote isipokuwa kupata machofu kutokana na matendo hayo hapa duniani na kupata adhabu katika Aakhirah. Haya yanatolewa mfano katika kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Inawezekana mtu anayefunga asipate chochote katika funga yake isipokuwa njaa na yule anayesimama usiku kuswali asipate chochote isipokuwa machofu.” [Imesimuliwa na Ibn Maajah kutoka kwa Abu Hurayrah na ameiSwahiyhsha Shaykh Al-Albaaniy Swahiyh al-Jaami’, (3482).
Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema:
وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾
“Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zinazotawanyika.”[Al- Furqaan:23]
Anasema pia:
الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ﴿٢﴾
“Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Naye ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa kughufuria.” [Al-Mulk: 2)
Kwa hiyo, fahamu kabla ya kitu chochote kile chengine masharti ya lazima ya ‘amali kabla ya kukubaliwa kwao. Ni muhimu sana ya kwamba mambo mawili makubwa yatekelezwe kwa ajili ya kila tendo.
La kwanza: Ya kwamba yule ambaye aliyetenda amali njema asitamani kupata chochote isipokuwa Radhi za Allaah (‘Azza wa Jalla) wa ‘amali ile.
Ya Pili: Ya kwamba ‘amali hiyo iwe inakubaliana na yale ambayo Allaah (‘Azza wa Jalla) Ameyaruhusu katika Kitabu Chake au kutoka kwa Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam.)
Fudhwayl bin Ayyaad, ambaye ni Taabi’iy, alisema kuhusu Aayah hii:
لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ
“... ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri vizuri zaidi... [Al-Mulk: 2)
“Ambayo yana Ikhlaasw na yako Swahiyh”. Wale ambao walio mzunguka wakasema “Na yapi hayo ambayo yana Ikhlaasw na yako Swahiyh?” Akajibu “Amali, ikiwa iko Swahiyh lakini haina Ikhlaasw ndani yake, basi haitakubaliwa, na kama ina Ikhlaasw lakini si Swahiyh hatakubaliwa mpaka iwe na vyote, iwe Swahiyh na ina Ikhlaasw. Ikhlaasw inamaanisha ya kwamba hamna kitu chochote ambacho kinatafutwa isipokuwa Radhi za Allaah (‘Azza wa Jalla) Swahiyh inamaanisha ya kwamba kinaendana na Sunnah.”
Na Salaf (watu wema waliopita) walikuwa wakisema: Hamna kitendo, japokuwa kama ni kidogo vipi, isipokuwa kitawekewa maswali mawili: Kwanini umekifanya? Na: Vipi umekifanya?
Swali la kwanza ni kuhusu sababu ya kutenda kitendo hicho na niya yake. Ikiwa Niya ilikuwa kwa ajili ya madhumuni miongoni mwa madhumuni ya kidunia kama vile kutafuta kusifiwa au cheo au malengo yoyote yale ya kidunia, (kitendo) hicho kitakuwa ni kitendo kiovu na kitarembewa kwa yule aliyekifanya. Ikiwa Niya ya kufanya hicho kitendo ni kutekeleza Haki ya Allaah ya kujiweka katika hali halisi ya utumwa Kwake na kutafuta njia ya kumkaribia, basi kitakuwa ni kitendo chema na kitakubaliwa, Allaah Akipenda.
Swali la pili ni kuhusu kumfuata na kumuigiza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Je hicho kitendo kilikuwa ni miongoni mwa vitendo vilivyoruhusiwa katika Shariy’ah au kilikuwa kutokana na bid’ah zinazotoka kwako wewe? Ikiwa kinatokana na muongozo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi kitakuwa ni kitendo chema na ikiwa kilikuwa ni kinyume na matendo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi kitakuwa ni kitendo kiovu na hakitakubaliwa kutoka kwa yule aliyekitenda kama ilivyothibitishwa katika Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye alisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Yeyote atakayeleta katika jambo (Diyn) letu hili kitu ambacho hakimo basi hakitakubaliwa.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na pia anasimulia ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Yeyote atakayetenda kitendo ambacho hatukikuamrisha basi hakitakubaliwa.” [Muslim]
Ikiwa kama moja kati ya masharti mawili (yaliyokwishatajwa) juu haijakamilishwa, kitendo kinakuwa si chema wala chenye kukubalika. Haya yanathibitishwa katika kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
ۖ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾
“Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende ‘amali njema na wala asimshirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Rabb wake.” [Al-Kahf :110]
Allaah (‘Azza wa Jalla) katika Aayah hii Anaonyesha ulazima wa kitendo kuwa chema, kwa maana, kiwe kinakubaliana na Shariy’ah. Kisha Akaamrisha ya kwamba mtu akitende kwa Ikhlaasw kwa ajili ya Allaah, bila ya kutaraji kitu chengine isipokuwa Yeye tu.
Al-Haafidhw Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) kasema:
“Hizi ni nguzo mbili za ‘amali zinazokubaliwa. Inahitajika ya kwamba kitendo kiwe na Ikhlaasw na pia kiwe Swahiyh katika Shariy'ah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mfano wa haya yamekwisha simuliwa kutoka kwa al-Qaadhwi Iyyaadhw (Rahimahu Allaah) na wengine.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) pia Anasema:
وَمَنْ أَحْسَنُ دِينًا مِّمَّنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلَّـهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ وَاتَّبَعَ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۗ ﴿١٢٥﴾
“Na nani aliye bora zaidi kwa Dini kuliko yule aliyejisalimisha kwa Allaah naye ni mtendaji mazuri …” [Al-Nisaa: 125]
Maana ya mtu kuunyenyekesha uso wake kwa Allaah ni: Mtu kuweka Niya na kutenda vitendo vyake kwa ajili ya Allaah. Na maana ya kutenda vitendo vyema ni: Kuiigiza na kuifuata Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).