Watu Na Ramadhwaan

Watu Na Ramadhwaan

 

Ummu Faraj

 

Alhidaaya.com

 

 

AlhamduliLlaahi Wa Kafaa, Wasw-Swalaatu Was-Salaamu ‘Alaa Nabiyyil Mustwafaa, War-Rasuulil Mujtabaa, Nabiyinaa Muhammad, Wa ‘Alaa Aalihi Wa Asw-haabihi Wamaniqtafaa

 

Amma Ba’ad,

 

Kwanza kabisa baaada ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kumtakia Rehma na Amani Rasuli wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nitachukua fursa hii kwa kuanza kutaja kwa uchache fadhila za mwezi mtukufu wa Ramadhwaan.

 

Hakika mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi miongoni mwa miezi 12 ya mwaka mzima. Ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameuchagua mwezi huu na Akaupa hadhi kubwa, na ni mwezi wenye fadhila nyingi. Miongoni mwa fadhila za mwezi huu mtukufu; ni kuwa huu ni mwezi wa kusamehewa madhambi, ni mwezi wa subira, ni mwezi wa Qur-aan, milango ya moto hufungwa na milango ya jannah hufunguliwa na Mashaytwaan hufungwa, ni mwezi ambao una siku iliyo bora kuliko miezi elfu nayo ni siku ya Laylatul Qadr, ni mwezi wa Du’aa; kwani maombi katika mwezi huu ni yenye kujibiwa, ni mwezi wa kutoa na mengi mengine.

 

Kwa hakika ni mwezi wa ‘Ibaadah na ‘amali zake zina ujira mkubwa katika mwezi huu kuliko miezi mingine.

 

Lakini basi ni masikitiko makubwa kwa watu walio wengi zinawapita fadhila hizi ima kwa sababu ya ujinga au kwa kufuata matamanio ya nafsi zao.

 

Alisikika Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa Msikitini kwenye Minbar aliitikia Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn, Swahaba wakamuuliza Ya Rasuli Allaah tumekusikia ukiitikia Aamiyn mara tatu;

 

“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Alinijia Jibriyl (‘Alayhis-sallam) akaniambia ni khasara iliyoje ya mtu imemfikia Ramadhwaan na isiwe ni sababu ya kusamehewa madhambi yake, sema Aamiyn, kisha akanambia ni khasara iliyoje ya mtu aliyewadiriki wazazi wake wawili na isiwe ni sababu ya kuingia Jannah, sema Aamiyn, kisha akanambia ni khasara iliyoje kwa mtu aliyesikia akitajwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha asimswalie, sema Aamiyn.”

 

Ukweli miongoni mwa watu walio wengi wamekosa msamaha na fadhila za mwezi huu mtukufu, wameacha mafundisho sahihi ya Dini yetu tukufu ya Kiislamu na makosa mengi yanafanywa na wengi wetu.

 

Nami nakusudia khasa kutaja baadhi ya makosa yanayofanywa na walio wengi katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhwaan, namuomba Rabb Mtukufu aniwezeshe In Sha Allaah.

 

Baadhi Ya Makosa Yafanywayo Mwezi Wa Ramadhwaan

 

v

- Miongoni mwa watu wanahifadhi Swawm zao za Ramadhwaan na kisimamo cha taraawiyh na Swalah za faradhi kila mwaka na ‘Ibaadah nyingine, lakini ‘Ibaadah zao wanazipeleka arjojo kwa kumshirikisha Allaah Mtukufu, wanakwenda kwa waganga kupiga ramli, kuangalia bahati kwa kupitia ‘nyota zenu’, na du’aa zao hawazielekezi kwa Allaah moja kwa moja bali wanaomba mizimu, makaburi na kuvaa mahirizi wakitaraji zinawakinga na madhara na Shaytwaan, hali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amelikemea sana jambo hilo, Amesema Allaah

 

 وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ﴿٦٥﴾

Kwa yakini umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: Ukifanya shirki bila shaka zitaporomoka ‘amali zako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Az-Zumar: 65]

 

Na Amesema Allaah Mtukufu:

 

 إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa: 48]  

 

Amesema tena Allaah Mtukufu:

 

  إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾

Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru. [Al-Maaidah: 72]

 

Hivyo basi mshirikina hatokubaliwa matendo yake mpaka aache ushirikina atubie kwa Rabb wake na ampwekeshe katika ‘Ibaadah zake ndio zitapokelewa ‘amali zake.

 

v

- Na miongoni mwa watu wameufanya mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi wa kucheza na mambo ya upuuzi, mwezi wa kupoteza wakati na kuifanya Swawm ni jambo jepesi bila mazingatio yoyote; utawaona watu mchana wa Ramadhwaan na usiku wake wanacheza Karata, Keram, Dhumna, Bao na mfano wake. Wamejikusanya makundi makundi wake kwa waume watoto kwa wazee wamechanganyika wala hawaoni hayaa, na wengine wameufanya ni mwezi wa kupiga ngoma khasa ukiangalia katika nchi zetu za Afrika Mashariki; wanadai kupiga ngoma kuamsha watu kula daku, na wengine hucheza ngoma hizo khasa ikaribiapo siku ya ‘Iyd huanza kupiga ngoma zao mchana wa Ramadhwaan wakiomba ‘Iyd toa’, yaani wapewe pesa na huku wanaume wakiwa wamejivisha mavazi ya kike na kukata viuno hadharani!! Hawajui kuwa hiyo ni laana!

 

Kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Allaah Amemlaani mwanaume anayejifananisha na mwanamke na mwanamke anayejifananisha na mwanaume”

 

Jamani huku ni kuudhalilisha Uislaam kwani dini hii si ya mchezo na magoma au kusikiliza miziki; hiyo sio ‘Ibaadah bali ni katika makosa makubwa kwa wanaocheza na wanaosikiliza na wanaoshangilia na kuwapa pesa hao waimbaji na wachezaji, kwani wote hao wanapata madhambi.

 

Allaah (Subhanahu wa Ta’aalaa) Amesema:

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٦﴾ وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِ آيَاتُنَا وَلَّىٰ مُسْتَكْبِرًا كَأَن لَّمْ يَسْمَعْهَا كَأَنَّ فِي أُذُنَيْهِ وَقْرًا ۖ فَبَشِّرْهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٧﴾

Na miongoni mwa watu, yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) njia ya Allaah bila elimu, na huichukulia mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha. Na anaposomewa Aayaat Zetu, hugeuka huku akitakabari kama kwamba hazisikii, kama kwamba kuna uziwi masikioni mwake, basi mbashirie adhabu iumizayo. [Luqmaan: 6-7]

 

Hivyo ndugu zanguni hiyo sio dini ya kucheza wala kupiga ngoma za ‘daku kula” wala ‘Idi toa’ wao wanajiona wako katika dini, lakini hakika yote hayo wayafanyayo ni makosa. Wamesahau kuwa mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi wa ‘Ibaadah na Jihaad na kujivunia thawabu kwa wingi na kuacha mambo ya kipuuzi.

 

v

- Na miongoni mwa watu wameufanya mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi wa kulala na uvivu, wakesha kwa kula Mirungi na kuangalia vipindi vya kipuuzi kwenye TV. Vipindi vya vichekesho (Vunja Mbavu), Michezo ya Kuigiza (Tamthilia), Miziki (hususan wanayoiita ya vizazi vipya!), Masinema ya ovyo, na misalsalati. Kukesha usiku na kulala karibu ya Alfajiri, wanalala mchana kutwa na kupitwa na Swalah ya Adhuhuri na Alasiri wanaamka karibu ya Magharibi kwa ajili ya kufuturu, kufanya kwao hivyo wajue kuwa wanachuma madhambi na hawapati kitu kwa Allaah, kwani wanafuata hawaa za nafsi zao na kuacha maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Wamesahau kuwa huu ni mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi wa Jihaad ya Nafsi kushindana na matamanio yote ya kipuuzi ili mtu apate kufuzu na asipitwe na fadhila za mwezi huu mtukufu.

 

v

- Na miongoni mwa watu wameufanya mwezi huu ni mwezi wa kula na kunywa na kushindana katika vyakula na kujifakharisha na vyakula vya kila aina kwa wakati mmoja, wanakula na kunywa wanashiba kupita kiasi mpaka wanashindwa kufanya ‘Ibaadah khasa ‘Ibaadah ya taraawiyh,

 

Wamesahau kuwa mwezi huu ni mwezi wa kutoa na kuwalisha masikini. Kadhalika ni mazingatio ya kujikumbusha ‘Ibaadah hii ya kufunga ili kutambua shida ya kukaa na njaa kwa mwenye nacho kuwakumbuka waso nacho na sio kufanya Israfu na kujifakharisha.

 

v

- Na miongoni mwa makosa yanayofanywa na wanawake ni kuanza kuingia jikoni toka asubuhi; wanapika na kuandaa vyakula vya kila aina, anataka siku moja hiyo apike mahanjumati yote; sambusa, kababu, katles, kachori, kunde, maharage, chapati, maandazi, vibibibi, huku akisikiliza nyimbo badala ya kusikiliza Mawaidha, mpaka inafika robo ya Ramadhwaan anaanza kujiuliza ‘nipike nini’ maana kila kitu keshapika! Kwa wakati mfupi ‘Ibaadah zinampita za kusoma Qur-aan, madarasa ya kumpandisha Iymaan ya kumuelimisha juu ya ‘Ibaadah yake yanampita hana nafasi, yeye anaandaa na kupika tu, na ifikapo Magharibi anaanza kupakua tu kuandalia waume, hata anachelewa kufungua Swawmu na Swalah ya Magharibi inampita au anaiswali kwa kuchelewa. Amesahau kuwa Swalah ni Waajib inapofika wakati wake.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesema:

 

  ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ﴿١٠٣﴾

Hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu. [ An-Nisaa: 103]

 

Na pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;

 

“Hawatowacha kuwa katika kheri umati wangu pindi watakapofanya haraka ya kufturu (kufungua Swawm) na kuchelewa kula daku”

Na amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;

 

“Allaah aliyetukuka Anasema: “Nampenda Mja wangu anapofanya haraka ya kufungua Swawm”

 

Na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) “Walimuuliza wanaume wawili katika Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mmoja wao anachelewa kufuturu, na anachelewa kuswali, na mwengine anawahi kufuturu na anawahi kuswali, ni nani aliye bora? Akasema: ambaye anawahi kufuturu na anawahi kuswali ndio bora.” [Muslim]

 

Inapendeza kwa mwenye kufunga Swawm awahishe kufungua pindi tu jua linapozama.

 

v

- Na miongoni mwa watu wanafunga Swawm zao vizuri lakini wanafuturu na vitu vya haramu; kama wavutaji Sigara, Tumbaku na uraibu mwengine ambao ni haramu si Ramadhwaan tu bali hata miezi mingine iliyosalia. Watu hao hustahi wakati wa mchana wa Ramadhwaan kwa ajili wamefunga lakini ifikapo Magharibi wanaisubiri kwa hamu na pakti ya sigara mkononi au mkebe wa tumbaku; kitu cha mwanzo baada ya kuzama jua ni kufungua kinywa kwa haramu hizo. Hakika watu hao wamesahau au hawaijui Hadiyth ya Mtukufu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba:

 

“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikua akifungua kwa Ratab, akikosa anafungua kwa Tende, akikosa anafungua kwa funda la maji.”

 

Inapendeza na ni Sunnah kufungua kwa tende au kwa maji na sio kufungua kwa vitu vilivyoharamishwa au hata vilivyo halali lakini si katika Sunnah; huko ni kujikosesha thawabu na fadhila, pia harufu ya sigara mtu anapoingia Msikitini huwakera watu na Malaika.

 

v

- Na miongoni mwa watu wanaswali taraawiyh lakini wanachagua ni mahali gani pa kuswali hiyo taraawiyh ambapo huswalishwa haraka haraka kwa Suwrah fupi fupi na kumalizika mara moja. Kadhalika wanaswali kwa uvivu na kukatakata Swalah zao, mara wanaswali mara wamechoka hawamalizi sambamba na Imamu utamuona mtu anaswali za mwanzo na anakaa kusubiri za mwisho; huo ni uvivu wa ‘Ibaadah. Hali wengine hawaswali kabisa.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Amesema:

 

“Mwenye kusimama (kwa Swalah) mwezi wa Ramadhaan kwa Iymaan na kutarajia malipo atasamehewa madhambi yake yaliyopita” [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

v

- Na miongoni mwa watu wanafunga Swawm kwa sababu ya mazowea au wanafunga kwa sababu nyumbani watu wote wanafunga au katika mji watu wanafunga anaona aibu kula mchana inabidi naye afunge, hafungi kwa Niyah ya ‘Ibaadah na kuwa hiyo ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), hali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;

 

“Mwenye kufunga Ramadhwaan kwa Iymaan na akataraji malipo Allaah humsamehe madhambi yake yaliyopita” [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

v

- Na miongoni mwa watu wanafunga Ramadhwaan lakini hawaachi yaliyokatazwa miongoni mwa mambo ya haramu kama kusengenya, kusema uongo, kutukana, kufitinisha watu na ushuhuda wa uongo kufanya ghishi (udanganyifu) wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa alihii wa Sallam) amesema:

 

“Yeyote ambae hatoacha kusema uongo, kusengenya, kufitinisha, kutoa ushuhuda wa uongo, basi ajue kuwa Allaah hana haja na Swawm yake katika kuacha chakula chake na kinywaji chake” [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

Hivyo basi inampasa kila Muislam awe makini na aachane na mambo kama haya na mfano wake hasa akiwa ndani ya Swawm, kwani hupelekea Swawm kuharibika na kukosa Thawabu na Fadhila za mwezi huu Mtukufu.

 

v

- Na miongoni mwa watu wanafunga Mwezi wa Ramadhaan lakini hawaswali kabisa si Swalah ya taraawiyh tu bali hata Swalah za Faradhi. Wengine huswali kwa kuchagua nyakati za Swalah wengine wanaswali Magharibi tu tena wanakwenda kwa kufuata mahanjumati Misikitini na haya ni makosa Ndugu zanguni, kwani kwa kufanya hivyo mtu ataingia katika kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) inayosema;

 

الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾الَّذِينَ هُمْ يُرَاءُونَ ﴿٦﴾وَيَمْنَعُونَ الْمَاعُونَ ﴿٧﴾

Ambao wanapuuza Swalaah zao. Ambao wanajionyesha (riyaa). Na wanazuia misaada ya matumizi madogodogo ya kawaida ya kila siku. [Al-Ma’uun: 5-7]

 

Na miongoni mwa watu wengine huswali Ramadhwaan hadi Ramadhwaan au Ijumaa mpaka Ijumaa, inapomalizika Ramadhwaan wanaacha kuswali.

 

Na Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Swalah Tano, na Ijumaa hadi Ijumaa, na Ramadhwaan hadi Ramadhwaan, unasamehewa madhambi baina yake pindi utakapojiepusha na madhambi makubwa”

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesema:

 

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا ﴿٣١﴾

Mkijiepusha na madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu. [An-Nisaa: 31]

 

Na miongoni mwa madhambi makubwa ni kuacha Swalah kwa makusudi bila ya udhuru wa kishari’ah.

 

‘Ulamaa wamesema yule ambaye haswali Swalah tano hana Swawm kwa sababu mwenye kuacha Swalah ni Kaafir kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Baina ya Mtu na kufru na Shirki ni kuacha Swalah” [Muslim]

 

Na Kaafir na Mushrik hakubaliwi ‘amali zake’ kwa kauli ya Allaah Mtukufu:

 

ۚ وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٨٨﴾

Na kama wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda. [Al-‘An’aam: 88]

 

v

- Na miongoni mwa watu wanafunga mwezi wa Ramadhwaan kwa shime inapokuwa mwanzo wa mwezi, na wanafanya uvivu katika kumi la mwisho wakati kumi la mwisho ni bora kuliko ya mwanzo, khasa utawaona kina Mama hawana nafasi ya kufanya ‘Ibaadah kutwa wanahangaika madukani kuwatafutia atoto nguo za ‘Iyd, wakirudi majumbani wamechoka hawawezi tena kusoma Qur-aan wala harakati nyingine za ‘Ibaadah. Wameufanya ni mwezi wa kuhangaika na si mwezi wa ‘Ibaadah.

 

Wamesahau kuwa katika kumi la mwisho kuna usiku wa Laylatul Qadr usiku ulio bora kuliko miezi Elfu, Amesema Allaah Aliyetukuka:

 

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ ﴿٤﴾سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ ﴿٥﴾

Laylatul-Qadr ni mbora kuliko miezi elfu. Wanateremka humo Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Rabb wao kwa kila jambo. Amani mpaka kuchomoza Alfajiri. [Al-Qadr: 3-5]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyopokewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha);

 

“Alikuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inapoingia kumi la mwisho anakesha usiku, na kuwaamsha watu wa nyumbani kwake (wake zake), na anaikaza shuka yake (yaani kukaza shuka makusudio kujitahidi kufanya ‘Ibaadah kwa wingi)” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Amesema tena Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

 

“Hakuwahi kumuona Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiisoma Qur-aan yote usiku mmoja, wala kusimama mpaka asubuhi, wala kufunga mwezi mzima katu isipokuwa Ramadhwaan tu.” [An-Nasaaiy]

 

Rasuli wa Allaah anajitahidi na kusoma Qur-aan yote kwa na hali ya kuwa yeye amesamehewa madhambi yake yaliyopita na yatakayokuja Je, mimi na wewe hizo juhudi tunazo na hali hatuna uhakika wa kusamehewa madhambi yetu?

 

 

v

- Na miongoni mwa watu kuna ambao hawaisomi Qur-aan, wala hawaswali, ispokuwa mwezi wa Ramadhwaan tu. Akimaliza Ramadhwaan kusoma na kuswali kumekwisha mpaka Ramadhwaan nyingine ifike, kama vile kapewa ahadi na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa atafika Ramadhwaan nyingine. Na miongni mwao wako ambao hawaijui Qur-aan kabisa si katika Ramadhwaan wala miezi mingine, hao Allaah Amewaziba nyoyo zao na macho yao kwa matamanio ya nafsi zao kupenda Dunia kuliko Akhera yao.

 

“Na amesema ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

“Zingetwaharika nyoyo zenu endapo mngezishibisha maneno ya Allaah.”

  

Mwisho nawausia pamoja na kuiusia nafsi yangu kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kujipinda kufanya ‘Ibaadah kama itakikanavyo na sio kufanya ‘Ibaadah mwezi huu tu ukimalizika tunaacha. Tujitahidi tudumu katika kumtii Rabb wetu Mtukufu, kwani Swawm inakulea na kukufanya udumu katika ‘Ibaadah pindi ukiifanya kwa ikhlaasw na sio kudharau kwani huu mwezi ni wa Jihaad ya kupambana na nafsi kutokana na vitimbi vya Shaytwaan, na ili tuweze kumshinda, tunapaswa kujikurubisha kwa Allaah (Subhanahu wa Ta’aalaa) katika kumtii kwa Aliyotuamrisha na kujiepusha na Aliyotukataza.

 

 

WabiLlaahit Tawfiyq

 

Share