Kampa Talaka Kisha Kamuoa Dada Yake Wa Baba Mmoja Je, Ndoa Inasihi?
SWALI:
ASSALAM ALIKOUM WARAHMATULLAHI TAALA WABARAKATUH. SUALA LANGU NI KUA NIKO NA RAFIKI YANGU AMBAE AMEOLEWA NA AMEZAA WATOTO WATATU, BAADAE AMEACHANA NA MUME WAKE, LAKINI YULE MUME BAADA YA MUDA AMEKWENDA KUMUOA NDUGU YAKE YULE MTALAKA WAKE, AMBAE NI NDUGU WA BABA MMOJA SUALA LANGU JEE NDOA HIO INAFAA. NAOMBA MNISAIDIE ENYI NDUGU ZANGU.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumuoa dada wa baba mmoja na baada ya kumuacha dada yake.
Hakika hii ni ndoa inayokubalika kishari’ah bila ya shaka au wasiwasi wowote.
Ama lililokatazwa waziwazi na shari’ah ya Kiislamu ni kuwa na dada wawili wakati mmoja wakiwa wote ni wake zako. Hii ni kwa mujibu wa Qur-aan, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
“Na kuwaoa pamoja dada wawili isipokuwa yale yaliyokwisha pita” (an-Nisaa’ [4]: 23).
Hivyo, linalokatazwa kisheria ni kuwaoa dada wawili wakati mmoja, lakini ikiwa umemuoa wa kwanza kisha mkaachana unaweza kumuoa mwingine bila ya tatizo lolote.
Na Allaah Anajua zaidi