Kumuoa Msichana Bila Ya Radhi Za Baba Yake Inafaa?

 

SWALI:

 

Assalaam alayqum, nishawahi kuoa mke nimezaa nae watoto watatu halafu tumeachana kutokana na tabia yake mbaya na sababu nyenginezo. baada ya hapo nimekutana na msichana mmoja ambaye nimempenda na yeye amenipenda kakaa hapa Tanzania mwaka halafu kasafiri kaenda Uingereza kwaajili ya masomo sasa mimi nataka kuoa huyu msichana nimepeleka posa yangu kwa baba yake ambayo mara ya kwanza kaleta sababu zake za kukataa kuniozesha ambazo hazina ukweli sasa ukawa mvutano mwaka mzima halafu imekuwa clear kwamba zile sababu alizotoa si za kweli na mwenyewe amekubali kwamba si za kweli ana ametoa ahadi- inaendelea kwenye msg ya pili.....

 

atashauriana na familia halafu atanijibu baada ya kama miezi minne kuona kimya mimi nimetuma mtu kuulizia jibu langu sasa baba yake yule msichana amejibu ya kwamba hataki kusikia suala hili tena nimeuliza sababu ni nini amesema hamna sababu na yeye ndio hataki na anasema yeye ndio mwenye amri na amekataa kuzungumza kabisa na msichana pia amemwambia baba yake kwamba amenipenda na anataka kuolewa na mimi ila baba yake bado hataki na sasa hivi ni muda mrefu sasa naomba mnisaidie je inawezekana mimi kumuoa huyu msichana bila ya idhini ya baba yake?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumuoa msichana bila idhini ya baba yake.

 

 

Hakuna Nikaah bila ya ruhusa ya baba mzazi wa msichana au walii wake. Hata hivyo, ikiwa walii amekataa bila ya udhuru wowote wa kisheria basi ndoa inaweza kufanywa bila ya tatizo lolote.

 

Kulingana na ulivyotueleza ni kuwa inaonekana kuwa baba hana udhuru wowote wa kisheria. Kwa sasa unalotakiwa kufanya ni wewe na huyo msichana kupeleka mashitaka kwa Qaadhi au kwa Shaykh anayejulikana kwa ucha Mungu, elimu na uadilifu ili kuweza kutatua tatizo hilo. Qaadhi anamuita baba ili amuulize sababu ya kukataa, ikiwa sababu ya kisheria haipo Qaadhi huyo atakuwa na uwezo kisheria kuwaoza bila ya tatizo lolote.

 

Hata hivyo, ndoa kama hizo huwa hazina raha kwani mara nyingi baba huwa na utesi, uhasama na kutokuwa mapenzi na binti yake na wewe, na kwa ajili hiyo hata wajukuu hawatapata fursa na nafasi ya kumuona babu yao. Unatakiwa kabla ya kuchukua hatua hiyo utumie mbinu zote za kumkinaisha baba wa binti huyo. Kufikia hilo waweza kufanya yafuatayo:

 

 

  1. Kuwatumia wazazi wako waende rasmi kuwaona wazazi wa huyo binti.

 

  1. Kuzungumza na jamaa ya baba wa msichana wenye kuikubali ndoa hiyo wazungumze na jamaa yao.

 

  1. Watumie rafiki za baba huyo ili pia wazungumze naye.

 

  1. Na wengine kama Shaykh au Imaam ambao wanaweza kumkinaisha kuhusu hilo.

 

Tunakutakia kila la kheri katika kufanikiwa kwa jambo hilo la kheri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share