Kumuoa Mjukuu Wa Kaka Yake Baba Mmoja Inajuzu?
SWALI:
Assalaam alaykum Warrahmatullahi Wabarakaatu. Naomba kuuliza swali. Mimi nina kaka yangu tumechangia baba je naruhusiwa kumuoa mjukuu wake?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumuoa mjukuu wa kaka yako kwa baba.
Hakika suala hili liko wazi kabisa katika Qur-aan pale Allaah Aliyetukuka Aliposema:
“Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khalati zenu, na binti wa ndugu mume” (an-Nisaa’ [4]: 23).
Kipengele cha swali lako ni, “Na binti wa ndugu mume”. Binti wa ndugu yako akiwa baba yake ni nduguyo kwa mama tu, au baba tu au shaqiqi huwa hufai kumuoa kisheria.
Na hivyo ndivyo kwa mjukuu wa kaka yako hata ikiwa babu yake huyo ni nduguyo kwa baba tu, basi haifai kwako kumuoa.
Na Allaah Anajua zaidi