Binamu Anafaa Kuwa Walii Ikiwa Hawako Wanaopasa? Mume Kuishi Mbali Naye Na Kuonana Naye Kila Baada Ya Miaka 3 Inafaa?

 

SWALI:

 

Amani ya allah iwe juu yenu: namshukuru mungu muweza wa kila jambo yeye mwenye ufalme wa mwanzo na wa mwisho: natowa shukurani zangu za dhati kwa kujibiwa swala langu la urithi: nimeelewa na nitafatiliya:
ila ninalo swala lingine kuhusikana na ndowa.


mimi ni binti, mzazi wangu wa kiume alisha fariki na nilikuwa ninasomeya nchini misri nikapata mchumba na yeye tulikuwa tunasoma wote hapo; ilibidi tuwafahamishe wazazi wetu, wakakubali na mahari zikatoka; ndipo ikafikia siku ya harusi ila ilitubidi tufungie ndowa hapo hapo misri; nikawafahamisha wazazi wetu kuhusikana na sharehe ya harusi yetu, ila kabla hatujaanda sharehe hata moja ilibidi tuulize wazazi kuhusikana na walii na hapo nilipokuwa ninasomeya walikuwepo vijana wawili mmoja ni mtoto wa bwana mkubwa wake na dada yangu na mungine mtoto wa binamu yangu; ndipo baba zangu wadogo wakasema sasa uko mbali ni nani atakae kuwa walii wako? Hapo ilibidi tupendekeze uyo kijana wa binamu yangu ndio akawa walii na kupewa mkono yeye na uyo mungine ndio akawa shahidi sasa swali langu ni hili je iyo ndowa yetu ilijuzu au itabidi tufanye ndowa nyingine? Na huyo mume wangu anaeshi ulaya huwa anakuja baada ya miaka 3 sasa inajuzu kweli mke na mume kueshi mbali kiasi cha muda huyo?

Wabillahi tawfiq


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa iliyofungwa Misri kwa kuwakilishwa binamu yako.

 

Kwanza tunatoa tanbihi kuwa watu wanapaswa waulize jambo kabla hawajalifanyia kazi na si baada ya kulifanyia kazi.

 

Tufahamu kuwa katika ndoa ya Kiislamu si lazima walii awepo katika Nikaah yako japokuwa idhini yake ni lazima, bali kule walii kutuma ujumbe awakilishwe tosha ndoa huwa imesihi. Na hata kama huna mtu kabisa kama walii wako basi Qaadhi anakuwa walii na anaweza kufungisha ndoa yako bila ya wasiwasi. Bora tu yule anayewakilisha awe ni kweli walii wako katika shari’ah.

Hivyo, ikiwa baba yako ameridhika na ndoa yako na akamuwakilisha mtu kuisimamia ndoa hiyo, awe mtu huyo ni binamu yako au mwengine, basi ndoa yenu haina mashaka.

 

Ama kwa mume kukaa nje kwa miaka mitatu, kidogo kuliko hiyo au zaidi ni maelewano yenu ikiwa kweli mtaweza kukaa mbali na uzinzi na madhambi mengine. Hata hivyo, hali iliyo bora ni kuishi pamoja na ikiwa mume anaishi mbali basi kwa uchache aje kwako baada ya kila miezi minne. Na ikiwa hali hairuhusu inabidi msikilizane na muelewane na kila mmoja awe ni mwenye kutekeleza hayo mapatano.

 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi

 

Je, Inafaa Mume Na Mke Kuishi Mbali Kwa Muda Mrefu?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share