Ameandika Talaka Miezi Minne Nyuma Ila Alikuwa Anasita, Mwishowe Amemtamkia Mkewe Talaka, Mke Ahesabu Ametalikiwa Tokea Lini?
SWALI:
Assalamalekum.
Mume kaandika talaka kila akitaka kumpa mkewe anaghairi kwa kufikiria watoto. Baada ya miezi minne kupita amechoka kusubiri anamtamkia mke kuwa amemuacha jee huyu mke itambidi akae eda au talaka imesihi ilipoandikwa tu na alikua akikaa naye kihalali kabla ya kumtamkia? Naomba msaada
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuandika talaka na kuizuia bila kumpatia mlengwa ambaye ni mke wake.
Pale mtu anapoandika talaka tayari talaka huwa imepita kwani ‘amali zote zinakwenda na Niyah. Sasa katika swali lako kuna tatizo moja, nalo ni je, anapoghairi kumpatia hiyo barua anakuwa na Niyah ya kumrudia au vipi? Ikiwa alikuwa na Niyah ya kumrudia basi atakuwa umemrudia wakati huo lakini talaka aliyoitoa itakuwa tayari kwenye hesabu, na hivyo haijulikani ni mara ngapi kaitoa?
Ni bora mtu anapotaka kutoa talaka kwanza atake ushauri na aswali Swalah ya Istikhaarah, kwani ikiwa mke ana makosa pia ana mazuri yake mengi. Na mke haachwi kwa makosa bali hunasihiwa na katika kupewa nasaha anaweza kujirekebisha na kuishi pamoja kwa hali nzuri. Ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katuambia:
“Enyi mlioamini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu. Wala msiwadhikishe ili muwapokonye baadhi ya mlivyowapa - isipokuwa wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu Ametia kheri nyingi ndani yake” (an-Nisaa’ [4]: 19).
Talaka ilipoandikwa tu tayari ilipita kwani hakuna mzaha kuhusu talaka. Ikiwa hakuweka Niyah ya kumrudia basi eda ya huyo mke itakuwa imeisha na makosa yatakuwa ya mwanamme ambaye aliandika talaka bila ya kumtaarifu mkewe.
Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:
Na Allaah Anajua zaidi