Anasoma Nchi Za Nje, Baba Hajaridhika Naye, Yeye Anahitaji Kisomo Apate Kuajiriwa Amhudumie Baba Yake Afanyeje?

SWALI:

 

Al Salam Aleikum Warahmatul Allahi Wa Barakatoh

 

Mimi nasoma Malaysia ilikua kwa hisabu ya company yangu lakini sasa imefilisika so imenibidi nitafute pesa ya kuendeleza masomo yangu.

 

suala langu ni hili mimi mzee wangu nahisi kama hajaridhika mimi kuendelea na kusoma anataka nirudi home, nahisi hata akiongea na mimi hajaniulizapo hata siku moja vipi masomo unaendelea vipi au chochote kuhusu masomo yangu, wala hajawahi kuniuliza unapata wapi matumizi yako au pesa ya kujiendeleza na masomo. Sijui nifanye nini na mimi nahitajia dua zake katika maisha yangu na wameachana na mama toka mimi mchanga so yeye baba ndio kila kitu katika dunia yangu.  kusoma nataka ili niweze kupata kazi nzuri kwa kudra ya Allah niweze kumsaidia maisha na same time sina raha vile dalili zote zinaonyesha kama yeye hajaridhika na nikimuuliza hayoko wazi kama nirudi au nibaki.

 

Please nisaidieni kidini kumridhisha Allah mafrudhi nifanye nini. Samahani kwa lugha yangu.

 

Shukran.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuendelea na masomo ilhali baba yako hajaridhika.

 

Hakika ni kuwa radhi za wazazi ni muhimu sana baada ya kupata radhi za Allaah Aliyetukuka na kumtii. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na Mola wako Ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema” (al-Israa’ [17]: 23).

 

Hata hivyo, kulingana na swali lako haliko wazi kama inavyostahiki kwani baba mzazi hajatoa uamuzi wa wazi. Na pia wewe mwenyewe hujatueleza kama alitoa ruhusa na idhini kwako ulipokuwa umekwenda kusoma kwa hesabu ya kampuni yako. Je, wakati huo alipinga au alikubali?

 

Haipaswi hadi kufikia kumuasi mzazi wako kwa ajili ya masomo ya kidunia ambayo si ya lazima na dharura kama masomo ya Dini. Ikiwa masomo ya Dini ambayo ni ya lazima na dharura vilevile unahitajia ridhaa za wazazi na kutowaasi kwa hilo, sembuse masomo ambayo si ya msingi wala si ya kukusaidia katika Aakhirah yako?

 

Kadhaalika, je, una msingi kiasi gani wa Dini yako hadi utilie hima na uzito wa kujiendeleza na hadi kufikia kuingia gharama kubwa na kusafiri nje ya nchi yako kwenda kuisaka hiyo elimu isiyo ya Dini? Hayo ni maswali ya msingi ya kujiuliza na kujitathmini.

 

Kukimbizana na dunia na yaliyofungamana nayo, kunasaulisha na kughafilisha na Aakhirah yetu, na hadi kufikia mja kuwa mtumwa wa dunia yake! Na hilo ni khatari sana kwa Dini ya mtu na mwisho wake.

 

Unaweza kukimbizana na kusoma masomo ya kidunia na ukawa na madigrii lakini usifanikiwe hiyo kazi au kipato unachotarajia. Muhimu ni kumcha Allaah na Yeye Atakufungulia kwa njia ambayo hutarajii.

 

Linalotakiwa ni wewe ni kumtii mzazi wako na kutilia hima kujiendeleza vilevile katika elimu ya Dini yako. Kadhaalika, kuwa karibu na Mola wako kwa ‘Ibaadah huku unamuomba Allaah Aliyetukuka Akufungulie milango ya rizki kwa njia nyingine na huku ukizidisha bidii katika kutafuta elimu ya Aakhirah yako.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akufanyie sahali katika mambo yako na maisha yako.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share