Ni Waajib Wa Mwanamke Kumhudumia Mumewe Kazi Za Nyumba?
Ni Waajib Wa Mwanamke Kumhudumia Mumewe Kazi Za Nyumba?
SWALI:
Ndugu zangu wa Alhidaaya swali ni kwamba mwanamke kumpikia mumewe, kumuandalia chakula na kutunza nyumba katika masuala ya usafi pamoja na kuangalia watoto huo ni wajibu wake ama si wajibu?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Bila shaka ni jambo linaloeleweka kuwa mume katika Uislamu anahitajika kumtimizia mkewe mahitaji ya msingi kama malazi, chakula, matibabu na mengineo. Hii ni kwa mujibu wa maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Aliyesema:
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ
Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao. [An-Nisaa: 34].
Pia anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَا تُضَارَّ وَالِدَةٌ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَّهُ بِوَلَدِهِ ۚ
Na ni juu ya mzazi wa kiume kuwapatia chakula chao na nguo kwa mujibu wa ada. Hailazimishwi nafsi ila kwa iliwezalo. Asidhuriwe mzazi wa kike kwa ajili ya mwanawe, na wala mzazi wa kiume kwa ajili ya mwanawe. [Al-Baqarah: 233].
Ni katika desturi na ada za Kiislamu tulizozirithi kutoka kwa watangu wema wa Kiswahaba hadi leo kuwa mwanamke anakuwa na jukumu la kumsaidia mumewe kazi za nyumbani mbali na kuwa si wajibu wake. Kufanya hivyo kunawafanya wawe ni wenye kusaidiana mmoja anakwenda kuchuma cha halali na mwengine anatunza vya nyumbani. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anatueleza kuwa mke mwema na mzuri ni:
فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ
Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. [An-Nisaa: 34].
Tunapata mifano mingi katika maisha ya Swahaba wa kike (Radhwiya Allaahu ‘anhunna) ambao walikuwa wakifanya kazi zote za nyumbani. Ama kuhusu kulea watoto ni jukumu kubwa zaidi la mama huku akisaidiwa katika hilo na mumewe ambaye ni baba wa mtoto.
Na Allaah Anajua zaidi