Ukimbizi Na Kubadilisha Jina La Baba
Ukimbizi Na Kubadilisha Jina La Baba
SWALI:
Assalam alaykum
Napenda kuuliza suali. Mimi naishi London maisha yetu sisi huku huwa tunakwenda magration na kuomba ukimbizi kwa kubadilisha uraia(mfano mkenya unasema wewe unatoka somali) sasa wakati tunapoulizwa majina yetu huwa tunabadilisha majina kama mtu unaitwa Khadija Ali basi unabadilisha jina la baba unasema unaitwa Khadija Ahmed sasa je inakubalika kiislam na kama haikubaliki tufanye nini? kwa upande wangu binafsi nimebadili jina la baba kwa nchi hii naitwa jina jingene lakini nyumbani najiita jina jengine hili nalitumia kwa hapa tu sasa je Allaah atatuweka katika watu wa fungu gani? Naomba majibu na hivi kubadilisha uraia ni sahihi? lakini Dini sijabadilisha nimesema ni Muislam.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kulingana na mafunzo ya Kiislamu kudanganya ni haramu, Kubadilisha uraia hakuna ubaya lakini kusiwe kinyume cha Sheria ya Kiislamu kwa mfano; kwa njia ya udanganyifu na kadhalika.
Ile nchi uliotoka ikiwa unafanya hijra (kuhama) kwa sababu ya kudhulumiwa kwa ibada au haki nyiginezo uhame kwenda nchi ambayo utapata uhuru wa kuendesha ibada zako bila pingamizi zozote, kupata hali ya kimaisha bora, na kadhalika. Lakini kuhama huku kusiwe kwa gharama ya dini yako.
Asli katika Uislamu, Hijra ni kuhama kutoka nchi ya kikafiri kwenda katika nchi ya Kiislamu au ya Waislamu. Mtu kubadalisha jina la babake haifai, Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Amesema:
ادْعُوهُمْ لِآبَائِهِمْ هُوَ أَقْسَطُ عِندَ اللَّـهِ ۚ
Waiteni kwa (majina ya) baba zao, huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Allaah. [Al-Ahzaab: 5]
Na Allaah Anajua Zaidi