Dada Mmoja Karitadi, Wengine Wanaishi Na Wanaume Wakiristo, Je, Akate Mahusiano Nao?
SWALI:
Asalaam aleykum warahmatullah wabarakatuh
[1] Naomba kupata ufafanuzi;kuna mdogo wangu wa kike tumechangia mama alibadilisha dini na kuwa mkristo na kufunga ndoa ya kikristo na wakati huo mama yetu alikuwa hai;mimi na ndugu zangu wa kiume hatukujihusisha na swala la hiyo ndoa japo aliyefariki mama alikasirika sana akaona kama hatumtendei haki huyo mdogo wetu na yeye pia, hata hivyo mimi binafsi nilimkanya kabla huyu mdogo wangu akadai mama ndio amemshauri wakati huo alikuja kwangu kutaka ushauri na kunidanganya hajabadili dini kumbe alishabadili na walikuwa kataka mipango ya ndoa; hata hivyo ndugu zangu na mimi hatukanyagi kwake wala yeye haji kwetu sisi wote ambao tulipinga swala la kubadilsha dini na yeye kutoka katika uislam.
[2] Kuna dada zangu wengine nimechangia nao baba wapo wawili wao nao wanaishi na wanaume wakristo na wamezaa nao ila hawajafunga ndoa, mimi huwa nakwenda kwao kwani bado ni ngugu zangu kwa damu na imani, je nafanya makosa kuwatembelea kwani hata wao kwangu wanakuja? Shekhe naomba majibu kwa haraka kidogo ili niyafanyie kazi.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu dada aliyeritadi na dada walioolewa na Wakristo.
Hakika masuala haya mawili ni nyeti sana kwa wakati wetu huu wa ulimwengu. Kwa kuwa tunakumbana na mambo hayo katika majarida na vyombo vya habari na kwa ajili hiyo tunaiga bila kujua ukweli na uhakika wa masuala hayo.
Kuritadi ni jambo baya katika Uislamu kwani linakuingiza mtu Motoni ikiwa hatorudi tena katika Dini. Lau kungekuwa na dola ya Kiislamu basi dada kama huyo au Muislamu yeyote anayefanya hivyo itabidi achukuliwe hatua na serikali kwa kumfanyia Da‘wah na kumnasihi ili arudi katika Dini ya Fitwrah (maumbile ya asli). Kwa kuwa dola hiyo haipo shughuli hiyo inabidi ifanywe nanyi huku mukizingatia maadili ya ulinganizi na nasaha.
Hamtopenda dada yenu apate shida hapa duniani na Kesho Akhera. Ikiwa sisi hatupendelei hilo basi nasi pia tusimuache dada yetu aelekee paovu. Itabidi mtumie busara na hekima ya kuweza kumvutia tena katika Uislamu kwa njia zote. Kwa kwenda kuzungumza naye, kuwatuma watu wenye ujuzi wa dini, kumtumia vitabu na hata kaseti. Ikiwa atang’ang’ania katika ukafiri wake itabidi wakati huo mukate mahusiano naye ya moja kwa moja lakini baada ya kutumia mbinu zote muwezazo za kumrudisha katika Uislamu.
Hakika ni makosa makubwa kwa dada Muislamu kukaa na asiyekuwa Muislamu kwa njia yoyote ile. Hiyo kisheria ni zinaa ambayo ni dhambi kubwa katika Uislamu. Na hata kama wangeolewa, kisheria pia hakuna ndoa baina ya binti Muislamu na mume kafiri, ndoa ya namna hiyo haitambuliki kuwa ni ndoa. Kwa njia hiyo pia itakuwa ni zinaa kisheria. Jambo ambalo mnafaa kufanya sio tu kutembeleana bali kuwalingalia dada zako waachane na wanaume hao kwani wapo katika njia iliyo mbaya. Inafaa mtumie njia mbalimbali za Da‘wah ili kuwavutia tena warudi katika Uislamu. Pia muwatumie watu wenye elimu kuliko nyinyi ili waende kuzungumza nao, kuwatumia vitabu, makala, kaseti kuhusu mambo tofauti ya Uislamu yakiwemo hayo waliyo nao wao. Ikiwa wataendelea na hayo waliyo nayo itabidi kwa madhambi hayo mkate uhusiano nao kwani kufanya hivyo huenda wakatia fahamu na kurudi katika njia ya sawa.
Na Allaah Anajua zaidi