Mume Anamkataza Mke Asiende Kwa Mama Yake, Je, Aende Kwa Siri?

 

Mume Anamkataza Mke Asiende Kwa Mama Yake, Je, Aende Kwa Siri?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalam aleikum. Kwanza ningependa kuwapongeza kituo chenu na In shaa Allaah Allaah awafanikishie katika kila jambo. Swali ni hili..kuna madada wawili wameolewa na waume ndugu, kukatokea misukosuko mabwana wakakosana, sasa huyu bwana mmoja amkataza mkewe kwenda kwa dadake kwa sababu ameteta na nduguye. Imefika mpaka mama ya madada ameshukia kwa dada mmoja na huyu bwana wa pili amkataza mkewe kwenda kumuona mamake kwa sababu ameteta na nduguye. Je hukmu yake ni nini? Na amaweza kuvunja sheria akaenda kumuona mamake kwa huyo dadake ama aende kisiri bila ya bwana kujua? Na ikiwa amemwambia ukikanyaga talaka imepita itakuaje? Tafadhali ningependa usaidizi wenu.na inshaAlah Mungu awape jaza yenu. shukran

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Inafaa tufahamu kuwa mke anawajibika kumtii mumewe katika mambo ambayo si ya maasiya. Na utiifu wa mume unatangulizwa juu ya mwengine yeyote ila Allaah Aliyetukuka na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ndio kwa ajili ya hiyo Allaah Aliyetukuka Akasema kuwa wanawake wema na walio wazuri ni wale wenye kuhifadhi kila kitu cha mume anapokuwa hapo mjini au nyumbani kwa yale Allaah Aliyotaka yahifadhiwe (an-Nisaa’: 34). 

فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ

Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. [An-Nisaa: 34]

 

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema yafuatayo:

 

"Du’aa za watu watatu hazitonyanyuka juu ya vichwa vyao kwa urefu wa mkono: Mtu anayewaswalisha watu na huku wanamchukia; mwanamke mwenye kumuasi mumewe na ndugu wawili walioteta" [at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

 

Hadiyth imewajumlisha watu aina mbili waliotajwa katika swali lako: Mke anayemuasi mumewe na ndugu waliogombana kuwa wapo mahali pabaya na du’aa zao hazitokuwa ni zenye kukubaliwa. Hiyo ni hasara kubwa sana kwao.

 

 

Na utiifu wa mke kwa mume, umehimizwa kwa jinsi ambayo mke hawezi kufunga Swawm ya Sunnah bila idhini ya mumewe. Na hata ikiwa amefunga na mume akamtaka itabidi afungue.

 

 

Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Mwanamke hafai kufunga kwa hata siku moja ikiwa mumewe yupo mjini ila kwa idhini yake, isipokuwa kwa funga ya Ramadhwaan" [Ahmad, al-Bukhaariy na Muslim]. Hata kwenda Hija inapendeza kwa mke kuomba ruhusa kutoka kwa mumewe. Akipatiwa ruhusa au asipewe anaweza kwenda kwani Hija ni wajibu kwa mwenye uwezo. Hata hivyo, hawezi kwenda Umra mpaka apate ruhusa kutoka kwa mumewe na awe na Mahram wake.

 

 

Katika ubora wa kutiiwa, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwa kuitilia mkazo:

 

"Lau ingewezekana kuwa mtu amsujudie mwengine, ningemuamuru mke amsujudie mumewe" [At-Tirmidhiy].

 

Na akasema,

 

"Mke anapokufa ikiwa mumewe yuko radhi naye, ataingia Peponi" [at-Tirmidhiy].

Amesema tena,

 

"Mke anaposwali Swalah tano, akafunga mwezi wa Ramadhwaan, akachunga heshima yake (kwa kutozini) na akamtii mumewe, ataingia Peponi kwa mlango wowote atakao" [At-Tirmidhiy].

 

 

Si vyema kwa mume kumkata mkewe na watu wake kwa sababu moja au nyingine isipokuwa tu kwenda kwake kwa watu anarudi na tabia mbaya au anavunja nyumba yake. Hata hivyo, ikiwa mume amemkataza kwenda huko itabidi mke asiende kwa siri au kwa dhahiri. Na lau ataenda kwa njia yoyote ile atakuwa ameasi na mahali pake patakuwa ni pabaya. Kwa njia hiyo mama na dada wanaweza kuja kumtazama yeye mpaka tatizo la utesi litakapoondoka. Na lau mume ataweka sharti kuwa ukienda huko si mke wangu tena, akikanyaga nyumba hiyo atakuwa tayari ameachwa na itabidi akae eda. Kwa hivyo, huyo mke asifanye masikhara ya kutaka kwenda kwa dada yake kwa siri.

 

 

Jambo ambalo linafaa lifanywe ni mama na wazazi wa pande zote mbili za mke na mume waingilie kati ili walete suluhu na upatinishi baina ya hao ndugu wawili. Uislamu umekataza ndugu wawili katika Imani wa damu kuteta zaidi ya siku tatu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Haifai kwa ndugu wawili kuteta zaidi ya siku tatu” [Muslim]. Atakayekuwa bora na kupata daraja kati ya hao wawili ni yule atakayeanza kumtolea mwenziwe salamu.

 

 

Suala la kugombana baina ya ndugu wa damu au katika Imani ni jambo lenye kutokea na kuonekana. Kwa hiyo, pindi linapotokea ni lazima ndugu mwenyewe (mmoja wapo), wazazi, jamaa wa karibu washirikiane ili kuweza kuwaleta pamoja tena katika undugu wao. Na Allaah Aliyetukuka Anasema:

وَالصُّلْحُ خَيْرٌ ۗ

Na suluhu ni bora.. [ An- Nisaa: 128]

 

Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa anasema pia,

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ﴿١٠﴾

Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu. Na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa. [Al-Hujuraat: 10].

 

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi

 

Baba Ametukataza Tusiwasiliane Na Dada Yetu – Je Tumtii?

 

Mume Hataki Niwasiliane Na Jamaa Zangu, Nafanyiwa Karaha Je, Niombe Talaka?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share