Kutumia Vyombo Vya Jikoni Vya Dhahabu Na Fedha Inafaa?
Kutumia Vyombo Vya Jikoni Vya Dhahabu Na Fedha Inafaa?
SWALI:
Assalam Alaykum ama nauliza kama ifuatavyo, Je kutumia vyombo vya nyumbani kama jagi, sahani na mfano wa hivyo vilivyotengenezwa na silver (fedha) au dhahabu (Gold) inafaa au haifai? Tafadhali naomba kufahamishwa, Nawatakia kheri nyingi inshaalah na ALLAH KARIM awajaze jaza yake wa hadha Assalam Alaykum.
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika hilo limekatazwa kwa Hadiyth za wazi kabisa za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hiyo, inatakiwa tuepuke na kuvitumia vyombo hivyo kwa hali yoyote ile. Hiyo ni kwa mujibu wa Hadiyth zifuatazo:
1. Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote mwenye kunywa katika vyombo vya fedha, hakika atavurumishwa kwa tumbo lakemoto wa Jahanamu” [Al-Bukhaariy na Muslim].
Na katika Riwaayah ya Muslim: “Hakika mwenye kula au kunywa katika vyombo vya fedha na dhahabu”.
2. Hudhayfah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza kutumia hariri nzito na nyepesi na kunywa katika vyombo vya dhahabu na fedha, na akatwambia: “Hivyo ni vyao (makafiri) duniani na ni vyenu Akhera” [Al-Bukhaariy na Muslim].
Kwa hiyo, haifai kutumia vyombo vya dhahabu na fedha kwa kunywea kinywaji au kulia chakula.
Na Allaah Anajua zaidi