Kuna Ubaya Gani Kutumia ‘Ta’ala’ Katika Salaam?
Kuna Ubaya Gani Kutumia ‘Ta'ala’ Katika Salaam?
SWALI:
Assalaam allaikum
Je? Vipi kuhusu hii Ta'ala' nini madhara yake hasa wassalam
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Ama kuhusu kutumia 'Ta'ala' kwenye Salaam, hilo ni jambo ambalo halijafundishwa na Nabiy wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika mafundisho yake aliyotupatia ya kutoleana na kurudishiana Salaam. Na hakuna uongofu mzuri usipokuwa wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na hakuna shari ya mambo kama uzushi, na kuongeza jambo katika mafundisho ya Diyn yaliyoletwa ima na Allaah au Nabiy Wake, hilo ni jambo ovu ambalo linaweza kumpelekea mwenye kufanya hilo kuishia katika moto. kama Hadiyth mashuhuri inavyomalizia kuwa "Wa kulla bid'atin Dhwalaalah, wakula Dhwalaatin fiyn Naar"
Lakini, tutofautishe kutumia 'Ta'ala' katika Salaam, na kutumia 'Ta'ala' katika sehemu zingine anapotajwa Allaah. Sehemu nyinginezo zozote kama kwenye Khutbah, Mawaidha, au maongezi, mtu hakatazwi kuweka neno 'Ta'ala' bali inatakiwa haswa kwani ni katika kumtukuza Allaah. Kama kusema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) au Allaah (Ta'ala') n.k.
Kwa hiyo ieleweke kuwa panapokatazwa ni pale kwenye Salaam kwani tayari kuna mafundisho rasmi ya Salaam na hakukufundishwa kuwekwa 'Ta'ala' ndani yake, na mtu akawa anatia ufundi ndani ya mafunzo yaliyokamilika ya Nabiy wetu, kuna mawili yanaweza kupatikana:
1. Kuwa Nabiy hakujua uzuri au umuhimu wa kuweka 'Ta'aalaa' kwenye Salaam na sisi ndio tunaojua zaidi.
2. Kuwa Nabiy alijua hilo lakini ametufanyia ubakhili.
Na yote hayo mawili ni madhambi makubwa ikiwa mtu atachukulia hivyo.
Ndio maana Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) akasema, 'Kile ambacho hakikuwa Diyn wakati ule (karne tatu), hakiwezi kuwa Diyn leo hii'
Anakusudia, kuwa chochote ambacho hakikufundishwa au kufanywa wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake na karne mbili bora alizozitaja baada yake, basi hakiwezi kuwa ni jambo katika Diyn leo hii.
Mfano wa mambo mengineyo yaliyokuja baadaye ni kama Khitmah, Talaqini, Kutazamia katika ndoa, na Mawlid ambayo yalianzishwa na Mashia karne ya nne na saba baada ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Mfano wa hilo la kuweka neno 'Ta'ala' pasipo pahala pake, ni mfano wa kuweka neno 'Sayyidana' kwenye Tashahhud wakati tunasema 'Ash-hadu Anna Muhammadan 'Abduhu wa Rasuuluh' kwani sipo palipofundishwa kuwekwa neno 'Sayyidana'. Lakini haikatazwi kwenye Khutbah, mawaidha au katika maongezi mtu anapomtaja Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema 'Sayyiduna Muhammad'.
Na mifano ni mingi.
Na huenda matatizo mengi ya kuzushwa mambo, kuongezwa, kuzidishwa na kuchomekwa katika Diyn, sababu yake kubwa ni watu kudhani wanapendezesha lile jambo, kulitia nakshi, kulivutia, kulifanya liwe la aina yake tofauti na mazoea, kudhani atapata thawabu zaidi n.k. n.k.
Lakini hajui mtu kuwa kufanya hivyo ni kutumbukia katika Hadiyth hizi mbili nzito kabisa:
Kutoka kwa Mama wa Waislamu Ummu ‘Abdillaah ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye alisema, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
"Yule anayezua kitu kisichokuwemo (kisichokuwa) katika jambo (Dini) hili letu kitakataliwa." [Al-Bukhaariy na Muslim]
"Yule anayetenda kitendo ambacho hakikubaliani na jambo (Dini) letu kitakataliwa." Muslim
Bila shaka hayo yatakuwa yameweka wazi utata wako katika matumizi ya 'Ta'aa' katika Salaam.
Na unaweza kuirudia tena kuisoma hapa chini Hadiyth yenye kuonyesha namna Nabiy alivyofundisha Salaam na ujira unaopatikana katika kuikamilisha Salaam hutoona ndani yake neno 'Ta'ala' pamoja na uzuri wa neno hilo.
'Imraan bin Huswayn (Radhwiya Allaahu 'anhuma) amesimulia: "Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamkia: "Assalaamu 'Alaykum" (Nabiy) akamrudishia (Salaam) kisha yule mtu akaketi. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Kumi)) [Kwa maana amepata thawabu kumi]. Kisha akaja mtu mwengine, akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLlaah" Naye akamrudishia, kisha yule mtu akaketi, Nabiy akasema: ((Ishirini)). Kisha akaja mtu mwingine akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLlaahi wa Barakaatuh". Naye akamrudishia kisha akasema ((Thelathini)) [Imesimuliwa na Abu Daawuud na At-Tirmidhiy na akasema Hadiyth Hasan]
Na Allaah Anajua zaidi