Subira... Subira... Subira...

 

Subira... Subira... Subira...

 

Ummu ‘Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمنِ الرَّحيم

 

 

 

AlhamduliLlaah, Himdi Anastahiki Allaah (‘Azza Wa Jalla) Rabb wa walimwengu na Mmiliki wa kila kitu, Rahman na Amani zimshukie Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Ahli zake na Swahaba wake na watangu wema hadi siku ya mwisho, ama ba’ad.

 

 

Maudhuu niliyoikusanya mbele yenu, ni ‘Umuhimu Wa Muislaam Kuwa Na Subra.’  Subra ambayo iwe ni kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) pekee katika kutekeleza maamrisho Yake kwa kustahamili kufanya mambo mema na kujiepusha na makatazo Yake kwa kustahamili kuacha maovu, vilevile kustahamilia viumbe kwa maudhi mbalimbali na kustahamili na misukosuko ya kidunia.

 

Umuhimu wa Subra umeelezwa katika Qur-aan na Sunnah, kwa kupatiwa mafundisho mbali mbali kupitia Manabii wa Allaah (‘Alayhimus-Salaam) na pia kwa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum).  Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) Anatueleza katika Qur-aan Tukufu:

 

 

وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلَّا بِاللَّـهِ ۚ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلَا تَكُ فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ﴿١٢٧﴾

 

Na subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na haiwi subira yako isipokuwa kupitia kwa Allaah. Na wala usiwahuzunukie, na wala usiwe katika dhiki kutokana na njama wanazozifanya.” [An-Nahl: 127]

 

Kwa hiyo, tunaona kuwa tutapata ujira wa Subra kutoka kwa Allaah kwa kusubiri kwa ajili Yake Pekee. Na hakika hakuna Subra yenye ujira ispokuwa inayokwenda sambamba na Ikhlaasw kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) kwa kukubali na kuwa na Iymaan juu ya mitihani itakayokupata kwa kuamini kuwa Allaah Ndiye Aliyekupatia, Naye Ndiye wa kuiondosha. Allaah (SubhanaahuWa Ta’aalaa) Anatueleza:

 

 ۗ إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿١٠﴾

 

Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu.” [Az-Zumar: 10]

 

Hawa watakaopata ujira bila ya hisabu ni wale watakaosubiri na kukithirisha ‘Ibaadah zao na kushukuru kwa mitihani itakapowakabili, sio kama baadhi yetu tukipatwa na mitihani basi tunavunjika mioyo kwa kuacha matendo mema na kuacha kukithirisha kumuabudu Allaah (‘Azza wa Jalla) kwa kufuata shinikizo la shaytwaan na kuzidi kupotea na kusahau fadhila ulizokuwa nazo kipindi chote cha awali.

 

Tunatakiwa kuiga Subra aliyokuwa nayo Nabiy Ayyuwb (‘Alayhis-Salaam) ambayo daima inapaswa iwe ni ukumbusho kwetu sote. Inatakiwa tusome kisa hiki mara kwa mara kwa ajili ya kujikumbusha. Wengi wetu tunalalamika kwa kitu kidogo katika maisha. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alimpa mtihani Nabiy Ayyuwb (‘Alayhis-Salaam) kwa namna ambayo kweli inatakiwa tujihusishe nayo na kuiga ili tuweze kupata ujira.

 

Iymaan yake na uvumilivu ni kitu ambacho kama sisi ni Waumini wa kweli tunapaswa kuiga na kutekeleza katika maisha yetu pindipo tupatapo mitihani katika hali mbalimbali. Tunaona jinsi gani Allaah Anavyomsifia katika Qur-aan:

 إِنَّا وَجَدْنَاهُ صَابِرًا ۚ نِّعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ ﴿٤٤﴾

“Hakika sisi Tulimkuta mwenye subira mno, uzuri ulioje wa mja, hakika yeye ni mwingi wa kurudiarudia kutubia.” [Swaad: 44]

 

 

Na baada ya hapo nini kilifuata kwa Nabiy Ayyuwb (‘Alayhis-Salaam) baada ya kuwa na Subra na kuendelea kuwa Mja mwema na mnyenyekevu? Allaah (SubhaanahuWa Ta’aalaa) Anatujulisha:

 

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ فَكَشَفْنَا مَا بِهِ مِن ضُرٍّ ۖ وَآتَيْنَاهُ أَهْلَهُ وَمِثْلَهُم مَّعَهُمْ رَحْمَةً مِّنْ عِندِنَا وَذِكْرَىٰ لِلْعَابِدِينَ ﴿٨٤﴾

“Tukamuitikia basi Tukamuondoshea dhara aliyokuwa nayo, na Tukampa ahli zake na mfano wao pamoja nao; ni rahmah kutoka Kwetu na ni ukumbusho kwa wanaoabudu (Allaah).” [Al-Anbiyaa: 84]

 

Subra ni nusu ya Iymaan, na humjenga Muislaam katika maisha mazuri na kuridhika katika hali ya mitihani atakayokumbana nayo, na hakika ukiwa na uvumilivu na kuwa na Subra basi Allaah (‘Azza wa Jalla) Hukurahisishia mitihani kwa kuona ni kitu cha kawaida na kuridhika na hali hiyo huku ukitaraji malipo mema na mazuri zaidi toka Kwake. Sisi kama wana-Aadam tuna upungufu sana katika Iymaan zetu na ndio maana wengi wetu tunapopatwa na mitihani basi hushindwa kuwa na uvumilivu kwa maana mioyo yetu imejaa udhaifu wa Iymaan na kutokuwa na mapenzi ya kweli kwa Muumba wetu. Kwa kuridhika na hali ya mitihani kwa kuamini kuwa Yeye Ndiye Aliyetuumba na Ndiye katupatia mitihani hiyo, basi tuamini kuwa hakika Yeye Ndiye Atakayetuondoshea kwa kutupa malipo mema hapa duniani na kesho Aakhirah.

 

Na Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kubakia katika subira kwa siku moja katika njia ya Allaah ni bora zaidi kuliko dunia hii na vyote vilivyomo ndani yake” [Al-Bukhaariy, Ahmad].

 

Tuangalie sisi wana-Aadam tumeumbwa na kuruzukiwa mambo mbalimbali ya malipo kutoka kwa Aliyetuumba, na kuturuzuku vitu mbali mbalimbali bila ya kutuhini, na hali Yeye Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) ni mwenye Subra juu yetu pamoja na utukufu Alionao kwa kuendelea kutuneemesha kwa kutupatia rizki, kutughufuria na kutuhifadhi hali ya kuwa tunamkosea usiku na mchana. Lakini, tazama Subhaana Allaah! Allaah Alivyo Al-Haliym (Mvumilia waja Wake) Ar-Rahiym (Mwenye kurehemu), Ar-Razaaq (Mwenye kuruzuku) na hali Yeye Ndiye Aliyetuumba na Hahitajii kitu chochote kutoka kwetu, ila sisi ndio twahitaji kutoka Kwake.

 

 

Tunatakiwa tufahamu kuwa Mja anapopatwa na mitihani mbalimbali kama misiba, mali, magonjwa na kadhalika, basi anatakiwa asubiri kwa maana Allaah (Subhaanahu Wa Taa’alaa) Amempa mitihani hiyo kwa majaribio ya kumpima Iymaan yake je, atasubiri ili upate kuneemeka zaidi au atakufuru ili apotee zaidi na awe ni mtu wa mitihani daima na kuwa khasarani.

 

 

Kutoka kwa Abu Sa'iydil-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba, amesema Rasuli wa Allaah  (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam: “Atakayetaka kusubiri (kufanya Subra) basi Allaah Atampa Subra. Na hakupewa mtu jambo la kheri na pana kama Subra [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kwa hivyo, ni khiyari katika kusubiri kwa faida na manufaa yetu wenyewe. Basi Tujitahidi kuwa na Subra katika kila mitihani na tukumbushane katika kuwa na Subra pale mwenzetu anapokabiliwa na mitihani, kwani shaytwaan hutumia fursa ya kumtoa mja katika Subra. Na hakika Waislaam walio bora ni wale wanaokumbushana na kuusiana katika mambo ya khayr ikiwemo kusubiri. Namalizia na kauli ya Allaah (‘Azza Wa Jalla) katika Qur-aan:

 

 إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ ﴿٣﴾

“Ila wale walioamini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri.” [Al-‘Aswr: 3]

 

Subra… Subra… Subra… ndugu zangu ni muhimu sana katika maisha yetu sisi Waislaam, naiusia nafsi yangu na wote kuwa na Subra, maana kwa kuwa na Subra tunapata thawabu ambazo tunazihitaji sana mbele ya Allaah (‘Azza wa Jalla) siku ya hukumu.

 

Kwa uwezo wake Allaah (‘Azza wa Jalla)  Ajaalie makala hii iwe ni yenye kufanyiwa kazi kwa kila atakayeisoma ili tuweze kupata malipo mema bila ya hisabu yatokayo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).  

 

 

Share