Mtoto Kumkanya Mzazi Wake Anayetoa Mawaidha Ya Dini Lakini Vitendo Vyake Ni Kinyume Na Anayosema
Mtoto Kumkanya Mzazi Wake Anayetoa Mawaidha Ya Dini Lakini Vitendo Vyake Ni Kinyume Na Anayosema
SWALI:
Assalam alaykum warrahmatullahi wabarrakatu! Kabla ya yote ningelipenda kutowa shukrani zangu za dhati kwa kuweza kututatuliya maswali yetu mbalimbali yanayo tutatiza. Allaah awazidishie kila la kheri (amin).
Swali: Mimi ni kijana ambae niko na miaka 18. Nnekuwa napenda kujuwa kwanza kuna ubaya wowote mtoto kugombana na babake kwa ajili ya Allah na si kwa ajili ya kinyume chake? Mimi mzee wangu namuishimia sanaaaaa lakini tunakufa nae kitu kimoja tu. Maa shaa Allaah alisoma kidogo na akishika mimbar wafwasi wake wanamkubali kabisa kwa kipaji chake. Tatizo nikuwa mawaidha yake na vitendo vyake nitafauti kabisa. Naomba unielewe Sheikh nikikwambia nitafauti yaaani namaanisha ivo kabisa.
Mi kama mtoto wake binaniuma sana mpaka ilifikia juzijuzi nilimuandikia message yakumwambia ajirekebishe tabia yake si nzuri. Kwa jinsi niliiandika message iyo wazi kabisa yaani sikumficha kitu alipoiona ilimuuma sana na kusema mambo mabaya kabisa. Swali langu nikupenda kujuwa kuna ubaya wowote kumkumbusha mzee wako wazi kabisa japokuwa atachukiya na kukwambia vibaya? Kutengana nae kwa ajili ya Allah ni vibaya? Ni ipi mipaka ya mtoto na mzazi wake? Jazzakallahu Kheir
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kulingania mema na kukataza maovu ndio njia inayotakiwa kwa kila mmoja wetu kila mmoja kwa uwezo wake na njia zake.
Allaah Aliyetukuka Anasema:
وَمَن يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّـهَ يَجِدِ اللَّـهَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿١١٠﴾
Na atakayetenda ovu au akajidhulumu nafsi yake; kisha akamwomba Allaah maghfirah; atamkuta Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-‘Imraan: 110].
Hata hivyo, Da‘wah ina maelekezo yake na njia zake ili Muislamu afike katika hali ya ufanisi. Na sifa moja muhimu ni kutumia hekima na mawaidha mazuri katika ulinganiaji. Allaah Aliyetukuka Anasema:
ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ﴿١٢٥﴾
Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi. Hakika Rabb wako Yeye Anamjua zaidi aliyepotea njia Yake, Naye Anawajua zaidi waliohidika. [An-Nahl: 125].
Katika ulinganiaji ni muhimu sana kutoa nasiha kwa njia nzuri sana na kujitoa na kujivua na kumfedhehi mtu. Lugha mtu anayotumia katika nasiha inaweza kumpelekea mtu kufuata au kukata uhusiano. Ilikuwa njia nzuri mwanzo kutafuta vitabu, kanda za mawaidha na njia nyingine ambazo zinatumika katika ulinganizi badala ya kumuandikia ujumbe mkali kama huo. Mwanzo unampa vitabu au mawaidha ambayo si moja kwa moja yana uhusiano na lile tatizo lake, baada ya hapo utampatia vitabu vingine na mawaidha yanayoendana moja kwa moja katika suala ambalo ana tatizo nalo.
Licha ya baba yako hata rafiki au nduguyo Muislamu hufai kumpatia changa moto kama hiyo uliyoandika “Jirekebishe tabia yako si nzuri”. Bila shaka, umesema kweli lakini si mahali pake kwani umetoka katika msingi wa mawaidha mazuri. Na ingekuwa busara zaidi kama ungekuwa unataka kumuambia moja kwa moja basi ukutane naye na uzungumze naye kwa njia ambayo ni nzuri ya kumfanya arudi nyuma na kujirekebisha kwa tabia hiyo mbaya aliyo nayo. Hili ni suala la kulichukua kwa umakinifu na hatua moja ukielekea nyingine na kufanya hivyo, Allaah Aliyetukuka Hukutilia tawfiki ya hali ya juu kwa njia hizo na malengo hayo.
Ikiwa utaendelea kumuaidhia kwa muda mrefu bila yeye kusikiliza na kubadilika, unaweza kumsusa kwa mambo fulani bila kumvunjia heshima kwani heshima yake kama baba ni lazima ibakie pale pale.
Kwa hivyo, tunakuomba uyazingatie hayo na utumie njia ndefu ambayo utapata natija kuliko hiyo ambayo inaonekana kuwa ni fupi lakini isiyokufikisha unapokwenda.
Tunakuombea kheri na fanaka katika shughuli yako hiyo ya kumlingania baba yako mzazi. Na bila shaka Allaah Aliyetukuka Atakutilia tawfiyq inshaAllaah.
Na Allaah Anajua zaidi