Ugonjwa Wa Ndege Ulioingia, Je, Inajuzu Kuwaua Kuku Na Bata?
Ugonjwa Wa Ndege Ulioingia, Je, Inajuzu Kuwaua Kuku Na Bata?
SWALI:
Asalam alaykum warahmatullah wa barakatuh
Na anza kwa kumshuru Allaah ambaye yeye ndiye mueza wa kila kitu pia nikitaka ziada ana amani zimuendeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na waislam watakao mfata Nabiy hadi siku ya mwisho. Pia niki kutakieni kila la kheri kwa Allaah kutokana na juhudi ambayo mnayo jitolea kwa kutuelimisha sisi.
Mimi swala langu ni hili mimi ni mwislam naishi nchi bara ulaya, sasa nimepata kazi kuwakamata kuku ama bata wagonjwa ili kuwatia sehemu penye gas ili wafe, jee hiyo kazi inajuzu mimi kuifanya ?
Natumayi majibu In shaa Allaah wabillah ataufiki.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Suala la kazi ni suala ambalo limehimizwa sana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Qur’an na kutiliwa mkazo sana na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth zake tukufu. Baada ya kusema hayo hatuna budi sisi kuzingatia kazi tunayofanya kwani zipo kazi ambazo haziendi sambamba na misingi ya Uislamu. Kazi kama hizo inakuwa ni haramu kuzifanya.
Tunapokuja katika suala lako inatakiwa tuelewe kuwa tumekatazwa kisheria kutoa roho ya kiumbe chochote pasi na ruhusa ya kisheria na inapobidi kutolewa basi inatakiwa itolewe kwa njia ambayo ni nzuri na ya muruwa. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Hakika Allah Ameamrisha ihsani (wema) katika kila kitu. Kwa hivyo, mkiua ueni vizuri; na mkichinja chinjeni vizuri. Kila mmoja wenu akitie makali kisu chake, na akipunguzie uchungu kichinjwa chake" [Muslim kutoka kwa Abu Ya‘laa Shaddaad ibn Aws [Radhwiya Allahu 'anhu].
Na katika msingi wa Uislamu wapo wanyama ambao wanaweza kuuliwa kwa sababu ya amri ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema:
"Aina Tano ya wanyama wanaweza kuuliwa hata katika Haram. Hawa ni kunguru, kipanga, nge, panya na mbwa mwenye kichaa (au mkali)" [Al-Bukhaariy, Muslim na Maalik kutoka kwa ‘Aa’ishah [Radhwiya Allahu 'anhaa], na kwenye riwaya ya Muslim kuna nyongeza ya 'nyoka'].
Wasiokuwa hawa hawafai kuuliwa isipokuwa kwa sababu ya kuliwa ikiwa wanaliwa au kuondoa madhara ambayo huenda yakapatikana kwa sababu ya ugonjwa ambao kwa tafiti barabara zilizofanywa zimeonyesha kuwa huenda wakawaambukiza binadamu ugonjwa kama ilivyo sasa katika Bara Ulaya na Asia kwa homa hii ya ndege. Lakini suala la kujiuliza sisi ni je, imehakikishwa kuwa kweli huu ugonjwa huwapata wanaadamu kwa ima kula nyama ya hao kuku au kwa kukaa nao pamoja? Au ni maoni tu ya wanasayansi kuwa jambo hilo hutokea bila ya wao kufanya utafiti? Na je, wale kuku au bata wanaouliwa wanapimwa kabla ya kuuliwa au wanashikwa tu walio wazima na wagonjwa na kuuliwa? Ikiwa wanachanganywa wazima na wagonjwa jambo hilo litakuwa halifai kisheria na hivyo kazi hiyo kuifanya haitafaa.
Ikiwa ni kweli kuwa wanaadamu hupatikana na ugonjwa kutoka kwa ndege hao basi kisheria ndege hao wanaweza kuuliwa kwa njia nzuri ili kuwaepusha wanaadamu na madhara kutoka kwao. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amemkirimu na Kumtukuza binadamu, na viumbe vyote vimeletwa katika kumtumikia yeye mwanadamu ambaye ana majukumu. Lakini inayofaa kutumiwa inatakiwa iwe ni ya kibinadamu na wala sio ya kinyama na ikiwa watakuwa wanatiwa katika gasi basi watakuwa wanawaadhibiwa sana, na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia tuchinje vizuri.
Lakini kwa maslahi ya binadamu ikiwa hiyo ndiyo njia ya pekee kuepusha magonjwa hayo kuenea baada ya utafiti basi itakuwa inakubaliwa na hivyo kazi yako ni halali. Ikiwa ipo njia nyingine iliyo nzuri lakini wakubwa hawataki tu kwa maslahi yao wenyewe, njia hiyo munayotumia itakuwa haifai na itabidi ufanye juhudi kuwaeleza hilo. Na wewe ndio muamuzi wa suala hilo kwani unaishi katika mazingira hayo na unaelewa yale ambayo yanayoweza kufanyika na yasiyoweza.
Na Allaah Anajua zaidi.