Ugawaji Wa Nyumba Iliyoachwa Na Baba Aliyefariki Akaacha Mke Na Watoto Watatu

SWALI:

Assalam alakum: Naitwa R'DHAN umri 25. Baba yetu amefariki akiwa ameacha watoto 3. wawili wanaume na mmoja mwanamke na mjane. Wakati wa uhai wake aliwahi kununua nyumba yeye na ndugu yake ambaye yuko hai (AMI YETU). Sasa kwa muda huu nyumba tunataka kuiyuza sababu hatufaidiki nayo. Swali langu Sheikh: Je nyumba hii itagawiwa vipi na mama (ambae ni mjane) ataingia wapi?  

 

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kutoka kwetu na tunawanasihi muwe katika hali ya subira katika wakati huu wa huzuni nzito. Vile vile tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amuweke mzazi wenu pema pamoja na wema katika Jannatul Firdaws al-A‘laa, Amiyn.

Ama kuhusu swali lako lina utata kwani maelezo hayo yanazua maswali kutoka kwetu mengine ili tuweze kufahamu vizuri swali lako hilo. Mwanzo tunapenda kukunasihi ndugu yetu pamoja na wengineo wenye kuuliza maswali yao kuwa wajaribu kuandika majina yao kwa ukamilifu kwani unapofupisha huenda ikabadilisha maana kabisa. Mfano ni Ramadhaan kuitwa Rama, na tunavyoelewa ni kuwa jina hilo Rama ni la mungu wa kibaniyani! Wengine wana majina kama Muhammad na kufupishwa na kuwa Moha au Mudy au Edy, Naaswir kugeuzwa Cholo au Faatwimah kuitwa Fetty, na Khadiyjah kuitwa Dida n.k.. Sasa tukijiuliza Moha ina maana gani inawezekana kuwa ni moharo au mfano wake. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza yafuatayo:

 “Wala msitukanane kwa kabila, wala msiitane kwa majina mabaya (ya kejeli): Jina baya kabisa kuambiwa mtu ni asi baada ya kuwa ni Muislamu” (49: 11).

Ama tukija katika swali lako tungependa kujua yafuatayo:

1.     Je, hiyo nyumba ambayo mnataka kuiuza aliyefariki baba yenu alikuwa ni shirika na nduguye (yaani ami yenu)?

 

2.     Je, wazazi wa aliyefariki wapo hai kwa sasa?

 

 

Mfano ikiwa nyumba hiyo ni shirika baina ya aliyefariki na nduguye (ami yenu) hautaweza kuiuza mpaka mumtake shauri ami yenu kwani yeye analo fungu lake. Ikiwa yeye pia amekubali kuwa nyumba hiyo iuzwe basi itauzwa naye kupatiwa fungu lake alilotoa katika kununuliwa nyumba hiyo.

Ama ikiwa nduguye alimsaidia aliyefariki lakini hawakuwa shirika katika hilo au alimkopesha ili kununua hiyo nyumba kisha akalipwa. Watoto watakuwa na uhuru wa kuiuza na kila mmoja atapata fungu lake la wirathi. Katika hali zote mbili, akishapatiwa fungu lake ami yenu pesa zilizobakia zitagawanywa ifuatavyo: Ami yenu hatarithi chochote kwa sababu ya watoto wanamzuia. Mjane fungu lake litakuwa ni thumuni (1/8). Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Allaah Aliyetukuka:

Lakini ikiwa mnaye mtoto (mjukuu), basi wao hao wanawake watapata thumuni” (4: 12).

Sehemu itakayobakia itapigwa mafungu matano sawa sawa. Hii ni kuwa mvulana hupata mara mbili ya msichana kama alivyosema Aliyetukuka:

 “Allaah Anawausieni juu ya watoto wenu; mwanamume apate sawa na sehemu ya wanawake wawili” (4: 11).

Hivyo, kila mtoto wa kiume atapata sehemu mbili na dada yao atakuwa na fungu moja. Mgao huu utafanyika tu ikiwa aliyefariki hana wazazi lakini pindi mzazi au wazazi wake watakapokuwa wapo hai basi mgao utabadilika.

Ikiwa wazazi wapo basi mgao wao utakuwa kama ifuatavyo: mjane atapata sehemu yake ya thumuni (1/8). Wazazi nao kila mmoja atapata sudusi (1/6) kwa mujibu wa kauli ya Allaah Aliyetukuka:

Na wazazi wawili, kila mmoja wao atapata sudusi ya mali aliyoiacha maiti, akiwa aliyefariki anaye mtoto (au mjukuu)” (4: 11).

Watoto watagawana kilichosalia, mtoto mvulana akipata sehemu mbili kwa msichana.

Ni vyema nyinyi kama watoto muwe ni wenye kumtazama mama yenu na inafadhilishwa na ni bora zaidi kwa mjane kukalia eda katika nyumba aliyokuwa akikaa. Lakini ikiwa ipo haja na dharura ya kuiuza nyumba inabidi nyinyi mchukue jukumu la kumtazama mama yenu. Allaah Aliyetukuka Atawawezesha kumkirimu mama mjane katika hali ngumu aliyonayo na Allaah Amuweke aliyefariki pema.

Kifo cha baba iwe ni waadhi kwetu kufanya mema na msisahau kumuombea du'aa kila wakati kwani kufanya hivyo inamfanya baba yenu aendelee kupata thawabu.

Maelezo zaidi yanapatikana katika kiungo kifuatacho:

Mirathi

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share