Babu Kaacha Mke Na Watoto Saba Wasii Kagawa Mali Kwa Upendeleo, Wengine Hawajapata
SWALI:
Asalam aleykum wa rahmatullah wabarakatu, Ramadhani kareem,
Naomba kuuliza kuwa Babu yangu amefariki ameacha mke na watoto 7 wakike na waume zao, mmoja alikuwa mume wake ameisha fariki na walikuwa na bin ami yao mmoja, sasa hapa kwanza nataka kuja mirathi yao itakua vip? Pili palipita muda hapa kurithiwa kuwa wasia alisema mali aliyo acha Babu yana deni ni mpaka lipite deni, ilipo malizika deni wasii akasema kua hizi mali nime usiwa kila mtu chake na akafanya hivo, lakin tuliona kua wasiya huo kua ume wapa wengine zaid kuliko wengine kwa mfano nyumba 7 kila mtu kapata yake lakini kuna shamba wame chukua dada wawili na waume zao kwa sababu ni wana wa mjomba kwa shangazi na waume zao ni ndugu kuna nyumab pia wamechukua. Sasa kuna matizo wajukuu wadai haki ya mama yao na watoto wengine mama zao wamisha fariki pia wadai. Na hapa ndio na omba msaada wa marifa juu ya urithisha wa mali hizi? Namna ya urathi huu.
WASHUKRAN JAZAKA LLAH KHEIR.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Mirathi ya babu aliyeaga dunia.
Hakika ni kuwa masuala yanayohusiana na Mirathi yamekuwa na ugumu sana kwa kuwa tumeshindwa kudhibiti mipaka iliyowekwa na Allaah Aliyetukuka.
Mwanzo kabla ya kugawa Mirathi inatakiwa aliyefaiki alipiwe madeni yake yote anayodaiwa kutoka katika mali yake. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Baada ya kutoa mlivyousia au kulipa deni” (an-Nisaai’ [4]: 12).
Na mara nyingi, kama vile ulivyosema kuwa babu aliusia mgao na hii ni miongoni mwa makosa yanayofanywa na walezi pamoja na wazazi. Mzazi hawezi kuusia mgao kwa warithi wake, kwani warithi na mgao tayari umeelezwa katika Qur-aan na Sunnah, wasiya inakuwa ni kumpatia mtu ambaye harithi kisheria au kutoa kama wakfu kwa Msikiti au Madrasah lakini isizidi thuluthi moja (1/3).
Ama waume wa binti za aliyefariki hawarithi chochote kutoka kwa alichoacha aliyefariki. Na binti wote mgao wao unakuwa ni mmoja tu wakipata sawasawa bila kutAzamwa kwa tofauti ya miaka. Mke mgao wake unafahamika kwani yeye aliyefariki akiwa na mtoto au watoto anapata thumuni (1/8). Na mabinti wakiwa zaidi ya wawili wanagawa thuluthi mbili ya mali yote (2/3).
Kisha umetueleza kuwa wapo baadhi ya watoto wa aliyefariki walioaga dunia, je, waliaga dunia kabla ya baba yao au baada? Hili ni muhimu kuweza kujua kama wajukuu wataweza kurithi au hawatorithi. InshaAllaah tutangojea ufafanuzi huo kutoka kwa muulizaji. Pili, twaomba utupatie kwa muhtasari wale jamaa wa aliyefariki walio hai baada ya kuaga dunia kwa babu. Kufanya hivyo kutatusaidia kuweza kuwajibu kwa urahisi zaidi.
Na Allaah Anajua zaidi