Mali Ya Urithi Iliyokuzwa Na Ndugu Mmoja Inakuwa Haki

SWALI:

 

Assalam alykm warahmatu LLah wabarakatuh, ama baada salam ningependa kuwapongeza ndugu zetu kwa bidii yenu na ishaAllah Allah awaeeke mahala pema, amin. Tafadhali naomba kujua taratibu za miradhi hulingana na
 

1. baba amefariki ameacha urathi walakin kabla kufariki alimuachia mkubwa wetu aendeleze biashara ya duka, ndugu yetu akafanya bidii na kuliendeleza kwa kiasi kikubwa na kuzaa biashara zingine. Jee nani anahaki ya kumiliki yote haya, yeye ama sisi sote?

2. baba ameacha nyumba ikiwa ina thamani duni baadaye huyu ndugu yetu akaiboresha na ikawa inatoa kodi kubwa, jee hizi kodi pamoja na nyumba  ni haki yake ama yetu sote na kama ni sote fungu lake na ndugu zake wengine wa kiume litakuwa sawa na vipi mirathi yatatekelezwa baada ya kujibu nawaomba kunijulisha kama kuna electronic book nikasoma zaidi. shukran jazila wallahu yajzykum

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mirathi ya baba baada ya kufa. Hakika hili ni suala nyeti katika masuala ya kijamii mbali na kuwa ni suala lenye mfumo mzuri uliowekwa na Allaah Aliyetukuka. Inatakiwa matatizo yote ambayo yanajitokeza katika mas-ala ya mirathi yaelekezwe katika Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na utata wote utaondoka.

 

Awali ya yote ni kuwa baba anapokufa huwa anaacha watoto akiwa amebariwa nao kama mlivyo nyinyi. Jambo ambalo ni zuri ni kuwa anapokufa tu Muislamu inatakiwa mali yake igawanywe baina ya warithi baada ya kutoa madeni na pesa za mazishi na ikiwa aliyefariki aliacha wasiya wa kutoa mali yake isiyozidi thuluthi kama wakfu. Ikiwa jambo hilo linafanywa basi baadaye huwa hakuna shida ya aina yote kuwa kaka kazalisha mali na kisha kudai kuwa ni yake na masuala kama hayo hayataibuka. Kwani watoto wanapokuwa na kubaleghe kila mmoja atapatiwa haki yake aliyoachiwa na babake, aliyefariki.

 

Allaah Aliyetukuka Anatuambia yafuatayo kuhusiana na mali ya mayatima: “Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu kubwa” (an-Nisaa’ [4]: 2). Na tena: “Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa. Mkiwaona ni wekevu, basi wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na aliyekuwa tajiri naajizuilie, na aliye fakiri basi naale kwa kadri ya ada. Na mtakapo wapa mali yao washuhudizieni. Na Allaah Anatosha kuwa Mhasibu” (an-Nisaa’ [4]: 6). Kwa mujibu wa haswa Aayah ya pili, ni kuwa msimamizi wa mali ya mayatima na hapa tunapata ni kaka ambaye anatakiwa awe muadilifu na afanye ihsani kwao kwa kufanya hivyo anapata thawabu kubwa mbele ya Allaah Aliyetukuka. Wasimamizi wa mali hiyo wameamriwa na Allaah Aliyetukuka watumie kulingana na kadiri yao ikiwa ni mafakiri lakini wasimamizi wakiwa ni waweza basi wanafaa wajizuilie kula mali hayo ya yatima. Kwa minajili hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) akawanasihi wasimamizi wa mali ya mayatima ambayo inafaa yatolewe Zakaah wayafanyie biashara yasije yakamalizwa na utowaji wa Zakaah. Hivyo, kumaanisha kuwa mwenye kuyashughulikia atakuwa ni mwenye kupata chochote na yatima naye apate faida.

 

Tunapata kuwa Maimaam al-Bukhaariy na Muslim wamenukuu Hadiyth kutoka kwa ‘Abdillaahi bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasimulia kisa kuhusu watu watatu waliofungiwa na jiwe katika mlango wa pango. Walimuomba Allaah Aliyetukuka kwa amali zao njema. Na mmoja wao alikuwa na mfanyikazi ambaye hakuchukua ujira wake wa siku. Huyu mwajiri akatumia ujira huo kwa kuufanyia biashara mpaka ikazaa ngamia, ng’ombe, mbuzi na watumwa. Na mwajiriwa aliporudi kutaka ujira wake, mwajiri akamwambia kuwa kila unachoona ni chake, naye akachukua kila kitu bila kumbakishia chochote. Jiwe likaondoka kwenye mlango na wakawa ni wenye kutoka huku wanatembea. Huu ni uadilifu wa hali ya juu kabisa mpaka mwajiri huo akapata radhi za Allaah Aliyetukuka seuze ndugu ambaye anatakiwa awe ni mwenye kuwajali zaidi ndugu zake ambao kwa sasa wa wamekuwa.

 

Tukirudi kwa maswali yako mawili ni kuwa tunasema hivi: Ikiwa mali iligawanywa baada ya kuaga baba yenu, na kaka yenu akatumia sehemu yake kuzalisha nyie hamtakuwa na chochote katika faida hiyo kabisa. Ikiwa mali haikugawanywa baada ya kufa aliyefariki baba na kaka yenu ndiye aliyetumia mali hiyo yenu kwa ujumla na kuyazalisha basi kila mmoja atakuwa ni mwenye kupata sehemu katika kodi ya nyumba na faida ya biashara kila mmoja na kiwango chake. Kwa kuwa kaka yenu ndiye aliyetumia akili yake, nguvu zake na wakati wake, yeye atapata faida kubwa zaidi kuliko nyote.

 

Nasaha ambayo tunaweza kukupeni ni kuwa msiwe na pupa kwa hilo bali inatakiwa mzungumze hayo katika kikao kwa busara, utaratibu mwema ili kila mmoja apate haki yake katika mali na faida. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka ikiwa kuna mzozo wowote usiwe ni wenye kulipuka bali msuluhishe kwa njia iliyo muafaka pamoja na kuwashirikisha wazee wenu waliobakia.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share