Vipi Afanye Biashara Ili Ajiepushe Na Haramu Na Apate Baraka Za Allaah?

SWALI:

 

Kama ni mimi nataka kufanya biashara ya kupeleka vitambaa dar-es-salam na kuchukua nguo kama vile nguo za kike za kitoto na za kiume jee? ili nipate baraka kutoka kwa Allaah nifanye nini ili biashara yangu hiyo iende vizuri na nijilinde vipi ili nisiweze kutumia haramu ktk biashara nakuomba unisaidie


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kufanya kwako biashara. Hakika ni kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ameisifu sana kazi ya biashara na mwenye kufanya biashara anakuwa ni mwenye kubarikia akiwa atafuata masharti yafuatayo:

 

  1. Ashikane na Ibaadah katika biashara yake kwa kuswali Swalaah za faradhi kwa wakati wake na kuleta adhkaar kwa kiasi kikubwa. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Allaah, na kushika Swalaah, na kutoa Zakaah. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka” (an-Nuur [24]: 37).

 

  1. Kuwa mkweli na mwaminifu katika biashara yako.

 

  1. Usifanye udanganyifu katika biashara kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Mwenye kutudanganya si katika sisi (Muslim).

 

  1. Usiape yamini la uwongo katika biashara yako.

 

  1. Kama una wafanya kazi usiwe ni mwenye kuwadhulumu na uwape haki yao kama mlivyo agana na kuahidiana.

 

  1. Jiepushe na haramu kabisa katika biashara yako.

 

  1. Na ukiwa na shaka ya uhalali au uharamu wa kitu ima ulizia au achana nacho.

 

  1. Muombe sana Allaah Aliyetukuka Akupatie tawfiki.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share