Kisa Cha Swahaba Tha’labah Kukataa Kutoa Zakaah Ni Cha Kweli?
Kisa Cha Swahaba Tha’labah Kukataa Kutoka Zakaah Ni Cha Kweli?
SWALI:
Amani iwe kwenu waelimishaji na Mola atulipe mazuri diniani na akhera.
Swali langu ni kwamba nimesikiliza mawaidha mengi lakini sijabahatika kujua hatima ya bwana thaalaba baada ya kuambiwa atoe mali na akakata. Naomba unifamishe niweze kufungua nijue mwisho wake na kama hakuna japo kwa maelezo nijulishe kupitia email yangu hakika nimevutiwa na kutaka kujua mwisho wake.
Wabilah taufik.
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Aayah inayozungumzia mtu aliyekataa kutoa Zakaah kwa ajili ya unafiki wake hata baada ya kumuahidi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni katika Suwrah At-Tawbah Anayosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ﴿٧٥﴾
Na miongoni mwao wako waliomuahidi Allaah (kuwa): Akitupa katika fadhila Zake, bila shaka tutatoa Swadaqah, na bila shaka tutakuwa miongoni mwa Swalihina.
فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ﴿٧٦﴾
Alipowapa katika fadhila Zake; walizifanyia ubakhili, na wakakengeuka huku wakipuuza.
فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُوا اللَّـهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ﴿٧٧﴾
Basi Akawapatilizia unafiki katika nyoyo zao mpaka Siku watakayokutana Naye kwa vile walivyomkhalifu kwao Allaah kwa waliyomuahidi, na kwa yale waliyokuwa wakikadhibisha. [At-Tawbah: 75-77]
Kuhusiana na Aayah hizi ‘Ulamaa wa Tafsiyr ya Qur-aan wametofautiana kuhusu jina la huyu mnafiki. Lakini rai yenye nguvu kabisa wamesema kuwa haiwezekani kuwa amekusudiwa Tha’labah kwa sababu alikuwa ni Swahaba aliyehudhuria vita vya Badr na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwashuhudilia waliohudhuria Badr kuwa ni wenye Iymaan na waliosamehewa madhambi yao.
Wengine wanasema kuwa wapo Tha’labah wawili mmoja Swahaba Muumini na wa pili ni yule aliyekuwa mnafiki na ndiye aliyekusudiwa hapa.
Ama Adhw-Dhwahhaak amesema: Aayah hizi ziliteremshwa kwa wanafiki nao ni Nabtal bin al-Haarith, al-Jadd bin Qays na Mu’attib bin Qushayr.
Kwa muhtasari kisa hicho hakiwezi kuwa kimetokea kwa Tha’labah bin Haatwib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) lakini kilitokea kwa asiyekuwa yeye kwa mnafiki au wanafiki kama walivyoyatajwa majina yao hapo juu.
Maelezo mazuri na marefu zaidi ya uchambuzi wa suala hilo, yanapatikana katika kiungo kifuatacho:
Kisa Kisichokuwa Sahihi Kinachonasibishwa Na Swahabi Tha'labah Bin Haatwib Kuhusu Kukataa Kutoa Zakaah
Na Allaah Anajua zaidi