Ndani Ya Ka’bah Kuna Nini?
Ndani Ya Ka’bah Kuna Nini?
SWALI:
Assalamu aleikum,
Nimefurahi sana baada rafiki yangu kunipa website hii ambayo tunajifunza mengi kwa uwezo wa Allah (Alhamdulillah Rabil-alamina) Suali langu ni kutaka kujua ndani ya Al-Kaaba mna nini? Ahsante
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika baadhi ya mas-alah kama hili la kujua kitu au vitu vilivyomo ndani ya Al-Ka‘bah hakumuongezei mtu iymaan yake.
Kabla ya kuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kabla ya kutekwa kwa mji wa Makkah mwaka wa 8H kulikuwa na masanamu yaliyokuwa yakiabudiwa na Maquraysh na vijiti ambavyo vilikuwa vikitumiwa katika kuangalilia na kupiga bao.
Ifahamike kuwa Ka‘bah yenyewe ni kama boksi, kumaanisha kuwa ndani kuna uwazi. Na kwa miaka kadhaa iliyopita katika Ka‘bah kulikuwa na nguzo ndani yake, kijibao cha kuwekea msahafu na msahafu na hakuna kitu chengine chochote. Kwa sasa hatuwezi kusema kwa uhakika kuhusu vilivyo ndani lakini inaweza kuwa ni kama hivyo tulivyovitaja au patupu wazi tu bila chochote.
Na Allaah Anajua zaidi