Mu'aawiyah (رضي الله عنه) Alikuwa Mwema?
Mu'aawiyah (رضي الله عنه) Alikuwa Mwema?
SWALI:
Assalamu Alaykum.
Naomba munifafanulie kiundani, je? ni nani huyu Mu'awiyyah? Pamoja na matendo yake kaika historia ya Kiislamu. Na je, alikua ni mtu mwema au muovu? Nakutakieni kila la kheri kwa kutusaidia ndugu zenu katika Uislamu, Allah (Subhanahu wata'aala atakulipeni mema)
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Mu'aawiyah (Radhwiya Allaahu 'anhuma) ni swahaba wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Mu'aawiyah (Radhwiya Allaahu 'anhuma) alizaliwa katika mji wa Makkah. Babake alikuwa ni Abu Sufyaan bin Harb (Radhwiya Allaahu 'anhu) na mamake ni Hind bint 'Utbah (Radhwiya Allaahu 'anha). Wote hawa wazazi wake walikuwa maadui wakubwa sana wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini mwishowe wakati wa kufunguliwa Makkah mwaka wa 8 H (sawa na 630 Miladi) wote wazazi walisilimu pamoja na watoto wao wakiwemo Yaziyd na Mu'aawiyah (Radhwiya Allaahu 'anhuma).
Baada ya kusilimu familia mzima ilishikamana barabara na Uislamu na ikaipigania Dini hii kwa kila njia. Baba yake hata kabla ya kuaga dunia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mwenye kupoteza jicho katika Jihadi. Walisimama imara wote katika Uislamu na wakafa wakiwa ni Waislamu wazuri.
Ama Mu'aawiyah na nduguye Yaziyd (Radhwiya Allaahu 'anhuma) walishiriki katika kuifungua nchi za Shaam. Na Yaziyd (Radhwiya Allaahu 'anhuma) akafanywa liwali (gavana) katika Ukhalifa wa 'Umar bin al-Khatwtwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu). Baada ya kufa Yaziyd (Radhwiya Allaahu 'anhuma), 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimtawazisha Mu'aawiyah (Radhwiya Allaahu 'anhuma) katika cheo hicho. Na katika miaka ishirini akabaki katika cheo hicho kuonesha alikuwa ni mahiri katika uongozi na mwaminifu.
Zipo tuhuma nyingi zinazotoka kutoka kwa hasa Mashia kwa kupatikana mapigano ya Siffiyn baina yake na 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu), Khaliyfah wa nne baada ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam). Kutokea kwa vita hivyo kulitokana na mikakati ya Mayahudi, hasa 'Abdullaah bin Sab'aa au Ibn Sawdaa' na wanafiki walioitakia maangamivu dola ya Kiislamu. Na kuna uongo wa jeshi la Mu'aawiyah kunyanyua misahafu mia sita jambo ambalo ni muhali wakati huo. Na uwongo wa kumshutumu Mu'aawiyah (Radhwiya Allaahu 'anhuma) ni mwingi uliozuliwa na Mashia na wengine wenye chuki kubwa dhidi yake.
Na kuna wengine wana chuki naye hata kusikia au kusoma yanayomhusu hawataki, na hakika wanaomchukia Mu’aawiyah wengine wanamchukia na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) vilevile kwa kufanya naye suluhu. Kwa hiyo, utakuta chuki haziishii kwake tu bali zinasambaa hadi kwa Maswahaba wengine na hizo ni dalili za unafiki, kwani hakuna amchukiaye Swahaba yeyote wa Nabiy ila lazima ana unafiki katika moyo wake.
Hata hivyo, kwa muhtasari ni kuwa Mu'aawiyah (Radhwiya Allaahu 'anhuma) aliishi katika Uislamu wala hakurudi nyuma kabisa. Bali katika ukhalifa wake wa miaka ishirini (661 – 680 Miladi) dola ilishamiri na kupanuka. Na katika wakati wake ndio alimpeleka mtoto wake, Yaziyd kuwa amiri jeshi wa kwenda kufungua Istambul, Uturuki na katika jeshi hilo walikuwemo Maswahaba kama Abu Ayyuub al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'anhu).
Mu'aawiyah (Radhwiya Allaahu 'anhuma) alikufa katika Uislamu. Jambo ambalo tunaweza kusema ni kuwa kama mwanadamu huenda akawa amekosa katika rai zake katika baadhi ya mambo na hilo ni katika ubinadamu kwani Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Kila mwanadamu ni mkosa na mbora wa mwenye kukosa ni mwenye kurudi nyuma na kutubia" (Ahmad).
Sisi kama Waislamu wa kihakika na kweli inafaa kuwaheshimu Maswahaba wote (Radhwiya Allaahu 'anhum) bila kubagua baina yao.
Kwa kirefu zaidi kuhusu Mu’aawiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ingia kwenye kiungo hiki hapa chini:
Mu'awiyah bin Abi Sufyaan (Radhwiya Allaahu 'anhu)
Na Allaah Anajua zaidi