Maimamu Wako Wangapi? Je Kuna Tofauti Baina Yao?

 

Imamu Wako Wangapi? Je Kuna Tofauti Baina Yao?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam Alaykum. Ama baada!! Napenda kufahamu Imamu wako wangapi? Na je kila imamu ana dhehebu lake? Na je wanapatikana kwa kuteuliwa vipi? Tafadhali ningependa kufahamu? Na imamu yupi ni bora kuliko wote?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kabla ya kutazama kuhusu idadi hiyo ya Imaam ni vyema tujue maana ya neno Imaam. Neno Imaam lina maana nyingi kilugha na hata kishari’ah. Imaam ina maana ya kiongozi wa juu katika dola. Pia ina maana ya kiongozi wa Waislamu katika Swaalah za jama’ah au pia mjuzi na aliyebobea katika mas-ala ya Dini ya Kiislamu mpaka akaonekana ni msingi wa Waislamu wa kawaida wa kuifahamu Dini yao.

 

Huenda muulizaji amekusudia maana ya mwisho katika swali lake na ndio tutataka kujibu hilo. Imaam kwa maana hiyo walikuwa wengi japokuwa wanaojulikana zaidi kwa sasa ni wanne, nao ni Imaam Abu Haniyfah, Imaam Maalik, Imaam ash-Shaafi‘iy na Imaam Ahmad bin Hambal. Hawa walibaki na kufuatwa na wengi miongoni mwa Waislamu kwa sababu walikuwa na wanafunzi walioendeleza fikra, rai na mafunzo yao kwa kila zama na pia waliacha maandishi, ilhali wale wengine hawakuwa na wenye kuyasambaza na pia ukosefu wa maandishi kutoka kwao kwa njia ya Vitabu. Ama Imamu wengine mbali na hao wanne tuliowataja hapo juu ni kama wafutao:

 

1)      ‘Abdur-Rahmaan bin al-Awzaa‘iy, maarufu akijulikana kama Imaam al-Awzaa‘iy.

2)      Al-Layth bin Sa‘d, maarufu kwa jina la Imaam al-Layth.

3)      Imaam Sufyaan ath-Thawriy.

4)      Daawuud bin ‘Aliy, maarufu kwa jina Imaam Daawuud adhw-Dhwaahiriy.

5)      Muhammad bin Jariyr bin Yaziyd atw-Twabariy, maarufu kwa Imaam atw-Twaabariy.

6)      Imaam Ibn Abi Laylaa.

7)      Imaam Abu Thawr.

8)      Imaam Ibn Taymiyyah au maarufu kwa Shaykhul Islaam, na wengine wengi.

 

Jambo muhimu ambalo tunafaa tulijue ni kuwa hawa wanachuoni hawakujitangaza kuwa wao ndio wanaojua kila kitu kwa hivyo Waislamu wawafuate kwa kila jambo. Bali wao walikuwa ni waaalimu waliojitahidi kwa kiasi kikubwa kueneza elimu ya Qur-aan na Sunnah. Na kwa ajili wao ni wanaadamu wanaopata na kukosa, wakawatahadharisha Waislamu wataokuja baada yao wasiwafuate kwa kila jambo, bali wanapokosea watu waache maneno yao na wayashike ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 Hebu tupate mfano wa kauli za Imaam kuhusu kufuata mambo walioyo yasema kimbumbumbu.

 

1)    Imaam Abu Haniyfah alitoa kauli nzito na za nguvu kuhusu kufuata kiupofu (Taqliyd) rai zake na zile za wanafunzi wake. Alikataza kwa msisitizo mtu yeyote kufuata rai zao au kutoa hukumu za kishari’ah kutegemea kwazo ila tu mtu huyo awe anaelewa zile dalili ambazo yeye na wanafunzi wake wamezitumia na yale machimbuko ambayo wamefikia hitimisho kwa uamuzi huo. Imaam amenukuliwa na mwanafunzi wake, Zufar kuwa alisema, “Haifai kwa yeyote yule asiyejua dalili na hoja zangu kutoa hukumu kulingana na kauli zangu, kwa hakika sisi ni binaadamu na tunaweza kusema kitu leo na kukikataa kesho”.

 

2)    Ibn ‘Abdil-Barr ameripoti kuwa Maalik wakati mmoja alisema, “Hakika ni kuwa mimi ni mwanaadamu, ninakosea na wakati mwengine ninasibu; hivyo chunguzeni vilivyo rai zangu, kisha chukueni yale yanayokubaliana na Kitabu na Sunnah, na yakataeni yote yanayopingana navyo”. Kauli hii ni dalili ya dhahiri kuwa Qur-aan na Hadiyth vilipewa kipaumbele juu ya vitu vyengine vyovyote na mwanachuoni huyu mkubwa ambaye hakuwa na Niyah ya kuwa rai zake zifuatwe pasi na kuchunguzwa.

 

3)    Imaam ash-Shaafi‘iy alitilia mkazo sana nukta muhimu kuhusu rai za kibinafsi dhidi ya Sunnah. Alisema, “Waislamu (wa wakati wangu) walikuwa na rai zinazokubaliwa na wote kwa pamoja kuwa yeyote anayepata Hadiyth sahihi ya Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) haruhusiwi kuipuuza kwa kufadhilisha rai ya mwengine yeyote”. "Ukiona katika maandishi yangu jambo ambalo ni tofauti na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi zungumza kwa kurejea Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na acha niliyoyasema mimi".Katika usimulizi mwengine: "…basi ifuate (Sunnah) na usitazame tena pembeni kufuata kauli ya mwengine yeyote" Amenukuliwa pengine akisema: “Hadiyth ikipatikana kuwa ni Swahiyh, basi hiyo ndiyo madhehebu yangu" Na akasema tena kumwambia Imaam Ahmad: "Wewe (Imaam Ahmad) ni mwenye elimu zaidi kuhusu Hadiyth kuliko mimi. Kwa hiyo Hadiyth ikiwa ni Swahiyh basi nijulishe, ikiwa ni kutoka Kufah, Basrah au Syria, ili nichukue rai ya Hadiyth madamu tu ni Swahiyh"

 

4)    Imaam Ahmad bin Hanbal naye amesema: “Msifuate rai yangu, wala msifuate rai ya Maalik, au Ash-Shaafi'iy au ya Awzaa’iy, wala Ath-Thawriy, lakini chukueni kutoka kule  walikotoa"

 

Katika usimulizi mmoja: "Msiige dini yenu kutoka kwa mtu yeyote katika hawa, bali chochote kilichotoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake, chukueni, kisha kwa At-Taabi'iyn (Waliofuata) ambako mtu ana khiari".

Akaeleza pengine: "Rai ya Awzaaiy, rai ya Maalik, rai ya Abu Haniyfah, zote ni rai, na ni sawa katika macho yangu. Lakini, dalili ni yale masimulizi kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake"

 

Akasema: "Yeyote atakayekanusha kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi yumo katika ukingo wa kuangamia"

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share