Nani Muhammad Bin 'Abdil-Wahhaab Na Kuhusu Mji Wa Najd
Nani Muhammad Bin 'Abdil-Wahhaab Na Kuhusu Mji Wa Najd
SWALI:
Assalaleikum warahmatullah. Amma baad, ndugu katika iman ninafuraha zisizo na kifani kupata website ya dini kama hii ambayo itasaidia wengi ambao watakayo ithamini. Allaah Awabariki wale waliofanya juhudi ya kuleta tuzo kama hii kwa ummati Muhammad Salla Allahu alayhi wasallam.
Swala langu ni kuhusu historia ya Muhammad ibn Abdulwahab nataka unieleze tarekh yake kwa jumla na huku alikozaliwa Najd je ni ile nadj aliyoitaja Nabiy Swalla Allahu ('Alayhis-Salaam) wasallam kuwa ndiko alikotoka shetani?
JIBU:
بسم الله، والحمد لله، والصلاة والسلام على أشرف الأنبياء والمرسلين نبينا محمد صلى الله عليه وآله وسلم وعلى آله وصحبه ومن اهتدى بهداه
Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah ('Azza wa Jalla) Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn
Shukrani kwa swali lako hili zuri ambalo kwayo baadhi ya watu wameona kuwa wamepata fursa ya kuweza kuwadharau na kuwatweza ‘Ulamaa ambao wameipigania Dini hii. Hakika watu ambao wanafuata matamanio yao wamempaka matope Shaykh huyu mwema na mtukufu.
Muhammad bin Abdil-Wahhaab ni Mujaddi (mwenye kukirejesha kitu kwenye upya wake) katika Dini yetu hii ya Kiislamu. Maana ya kujadidisha katika Dini ni kuyafufua upya mafundisho yaliyo fichika kwa kuwarejesha watu kwenye mafundisho sahihi yenyewe kama yalivyo.
Jina lake kamili ni Muhammad bin Abdil-Wahhaab bin Sulaymaan bin ‘Aliy bin Muhammad bin Ahmad bin Raashid at-Tamiymiy. Alizaliwa mwaka 1703 katika mji wa ‘Uyaynah, Saudia. Alikuwa ni mtu mwenye akili kali sana hivyo kuweza kuhifadhi Qur-aan akiwa na umri wa miaka chini ya 10. Alisoma Fiqhi ya madhehebu ya Imaam Ahmad bin Hanbal akiwa mwanafunzi wa babake. Kuanzia ujana wake alivutiwa sana kusoma vitabu vya tafsiri na Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na vitabu vya Tawhiyd. Alivutiwa na kuathiriwa sana na vitabu vya Shaykh Ahmad bin Taymiyah na vya Ibn al-Qayyim. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta ilimu.
Baada ya kusoma Uislam vizuri, Shaykh aligundua kuwa mambo mengi yanayofanywa na Waislam hayaambatani na mafunzo sahihi ya Uislam. aliona kuwa uharibifu huo uko kwao Najd na uko kila alipotembelea. Huo ni upotevu uliowapata Waislam kwa kuitakidi itikadi mbovu na kushikamana na ada chafu. Shaykh aliyaona maovu mengi na akachukulia kuwa ni wajibu wake wa kidini wa kujitolea na kusimama kinyume nayo kwa kubaini haki. Alipata misukosuko kwa sababu ya msimamo wake.
Alitumia mbinu mbali mbali ya kufanya kazi hiyo kama kuandika vitabu, barua, makala, kuwahutubia watu na kuweka halaqah za mafunzo na darasa kwa ajili ya kubainisha ‘Aqiydah sahihi na ‘Ibaadah za kisawa. Allaah Alimpatia umri mrefu ulio tumiwa wote kwenye amali za kheri na kuitakasa Dini ya Kiislam na uchafu na mambo ya uzushi. Katika uhai wake aliwahi kuona matunda ya juhudi zake kwa idhini ya Allaah Aliyetukuka katika sehemu tofauti. Aliaga dunia mwaka wa 1792. Alikufa kifo cha kawaida lakini ulinganizi wake ulibaki na kuwa ni ulinganizi wa haki wa kufuata Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) utaendelea kwa sababu nuru ya Uislam haizimiki.
Haya aliyoyafanyia bidii si kuwa alianzisha Dini mpya bali aliendeleza ile Dini ya Allaah ('Azza wa Jalla) iliyokamilishwa kupitia kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Msimamo wake ulikuwa ni Qur-aan na Sunnah, na kwa juhudi zake leo Waislam wengi wameweza kufungua macho na kuona haki.
Maadui kuanzia enzi zake walijaribu kulipaka matope na kuliharibu jina lake lakini walishindwa kwani Allaah ('Azza wa Jalla) hulinda waja wake wema. Jina lake litaendelea kutajwa kwa wema na tunamuombea Allaah Amrehemu na Amwingize Jannah ya Al-Firdaws ya juu.
Najd ni hiyo hiyo ambayo ipo Hijaaz na ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuomba Allaah Aibariki.
Lakini katika Hadiyth ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliashiria kwa mkono wake kuwa atatoka shaytwaan au pembe ya shaytwaan, ishara hiyo kwa vitabu vyote inasemwa ni Iraq. Na hakika Iraq kama tulivyoona kwenye historia na hadi leo hii, kumetokea balaa nyingi na fitna nyingi kupita kiasi. Hata hivyo haiimanishi kuwa Iraq yote ina fitna, la! Kuna mazuri na historia kubwa ya Uislam na kuna wema wengi waliokuwa huko. Maelezo zaidi kuhusu Hadiyth hiyo ambayo Mashia wamezusha kuwa alikusudiwa Shaykh Muhammad, ina uchambuzi mpana mzuri kutoka kwa ‘Ulamaa.
Mashia kwa uovu wao mkubwa wanadai pia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaja Hadiyth hiyo aliashiria kwenye nyumba yake! Haiwezekani kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aashirie kuwa shaytwaan anaweza kuwa katika ambalo leo hi ni kaburi lake (maana Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam kazikwa nyumbani kwake). Allaah Awahizi wote wenye kumtusi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wake zake na Maswahaba na wema wote.
Ni kawaida kuwa katika jamii wapo walio wazuri na wapo mashaytwaan wa ki-bin Aadam. Lakini unaposoma maisha ya Shaykh huyu tabia na maadili yake ni tofauti kabisa na shaytwaan. Kawaida shaytwaan anaamrisha mabaya lakini tunaona Shaykh alifanya juhudi kufufua Sunnah ambazo zilikuwa zimekufa na kupiga vita bid‘ah (uzushi) katika Dini hii yetu tukufu.
Kwa maelezo na manufaa zaidi bonyeza viungo vifuatavyo :
Imaam Muhammad Ibn Abdul Wahhaab - Maisha Yake Na Harakati Zake
Historia Fupi Ya Imaam Muhammad Bin 'Abdil-Wahhaab
Uwahabi: Ufafanuzi Na Majibu Juu Ya Majungu Dhidi Ya Shaykh Muhammad 'Abdul-Wahhaab
Marekebisho Yanayohusiana Na Kuelewa Kimakosa Taariykh (Historia) Ya “Uwahabi”
Na Allaah Anajua zaidi