Wameoana Bila Ya Wazazi Kujua Kukhofu Wasifanye Zinaa, Nini Hukmu Ya Ndoa Hiyo

SWALI:

 

Asalam alaikum

 

msichana mmoja alienda masomoni USA, kufika kule akakutana mvulana wakaowana bila ya ridhaa ya wazazi wa mwanamke na mwanaume ila wamepata mashahidi wa ndoa, wamefanya vile kwa ajili ya zinaa kuiepuka kwa kumuogopa Mola, hofu yao ni wazazi watakaposikia jambo hili itakuaje, pia ndoa yao itakuwa imesihi bila ridhaa ya wazazi? Pia njia ipi nzuri yakuwakabili wazee wao ili wawafahamu len 

 

AHSANTE MAASALAM


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu mwanamme na mwanamke kuoana bila kuwajulisha wazazi.

Uislamu ni nidhamu kamili ya maisha ambayo imetupatia njia ya kuweza kukabiliana na kila jambo kwa njia zake zilizo barabara. Katika nidhamu ya ndoa kuna masharti kadhaa ambayo yanatakiwa yapatikane ili ndoa yenyewe iswihi. Ni ajabu kwa watu kutaka kujiondoa na dhambi moja lakini wakaingia katika dhambi lingine ambalo huenda likawa ni kubwa au sawa na lile wanalolikwepa.

 

Pia ni ajabu kwetu kuwa tukawa tunauliza jambo baada ya tukio lenyewe kutokea, badala ya kuuliza kabla yake. Ni ajabu kuwa Muislamu akashindwa kujizuilia na dhambi kwa siku chake huku anatafuta njia ya kuingia katika uhalali wa jambo.

 

Ama masharti ya kuswihi ndoa ni kama yafuatayo:

 

1.     Walii: Awepo baba wa mke au jamaa ya karibu wa upande wa baba ikiwa baba ameaga dunia. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana ndoa bila ya walii” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na al-Haakim).

2.     Mashahidi wawili waadilifu.

3.     Tamko la kufungisha Nikaah liwe ni lenye kufahamika na kueleweka vyema, yaani ifahamike kwa wanaoana na kupatikane kuitikia na kukubali ndoa hiyo mke na mume.

4.     Mume kutoa mahari.

 

Inasikitisha kuona kuwa watu wawili wanafanya juhudi kutotaka kuingia katika zinaa lakini wakajiingiza huko huko kwa kichwa na miguu. Kulingana na masharti ya ndoa yaliyo juu hapana ndoa baina yako na huyo mwanamme uliye naye. Unalotakiwa kufanya sasa ni kuepukana na huyo mwanamme haraka sana na kila mmoja akae kwake. Baada ya hapo wasiliana na baba yako kuhusu kutaka kuolewa wala usiogope atakubali au atakataa. Bila shaka, mzazi kwa kumtakia kheri binti yake atakuwa ni mwenye kuridhika kwa hilo.

 

Lakini la muhimu ni toka katika zinaa kwa sasa mpaka uwasiliane na mzazi wako. Pia unatakiwa utubie kwa Allaah Aliyetukuka kwa kosa hilo kwa kujuta, kuazimia kutorudia tena kosa hilo na kuacha maasiya hayo.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

Kufunga Ndoa Kwa Njia Ya Simu, Inafaa Bila ya Walii?

Kumuoa Msichana Bila Ya Radhi Za Baba Yake Inafaa?

Hawezi Kujizuia Kufanya Zinaa, Je Anaweza Kufanya Ndoa Ya Siri Bila Wazazi Kujua?

Wazazi Hawataki Nifunge Ndoa Hadi Nimalize Kusoma Nami Niko Katika Zinaa, Nifanyeje?

Ndoa Ya Siri Inafaa Ikiwa Wazazi Hawataki?

Ndoa Bila Ya Radhi Ya Wazazi

 

 

Na Allaah Aliyetukuka Anajua zaidi

 

Share