Ametamka Talaka Kwa Hamaki Kuwa Pindi Mkewe Akitoka Nje Ya Ndoa Itakuwa Talaka Yake – Anaweza Kurudisha Kauli Yake?

SWALI:

 

Assallam allaykum?

Mimi ni swali moja, Nilimwambia mke wangu kama ataniendea kinyume kwa kutoka nje ya ndoa, atakuwa ameachika, lakini nilikuwa na jazba wakati wa kusema maneno yale. sasa nimefikiria na kuona kama haikuwa na ulazimu kusema maneno yale, swali langu ni hili je upo uwezekano wa kufuta yale niliotamka, kwani binadamu tunakosea na ulimi unateleza?

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kutoa masharti ya talaka kwa jazba.

 

Tunatakiwa tufahamu kuwa talaka inapita ikiwa imetamkwa kwa jazba, mzaha, ukweli au njia yoyote ile. Talaka ambayo imewekewa sharti kumaanisha kuwa lau mke atatoka nje ya ndoa au kufanya kadhaa, hiyo moja kwa moja ni talaka inayohesabiwa.

 

Zaidi ya hayo, suala hilo la wewe kudai kuwa ulitoa kauli hiyo kwa jazba na kuwa unataka kufuta kauli yako, ni kuonyesha namna gani ndugu yetu ulivyokuwa dhaifu na kukubali uharamu na uchafu uendelee ndani ya nyumba yako kwa kuonyesha kuwa unajuta kutoa kauli ya talaka na kwamba mke huyo aendelee kuishi na wewe. Hakika mke kama huyo si tu haifai kwa mtu kama wewe kumuonyesha kuwa ulifanya kosa kwa kumwekea sharti la talaka na unataka uishi naye.  Bali vilevile haifai kuishi naye kwani ni kufuga uchafu ndani ya nyumba yako kwa sababu anaonyesha ataendelea na tabia hiyo kwa kujua kuwa mume wake ni dhaifu na hawezi kufanya lolote lile.

 

Muislamu anafaa awe na wivu kwa mkewe kwa kiasi ambacho hawezi kuvumilia hata kumuona mkewe anazungumza tu au kukaa na mwanamme mwengine ambaye si maharimu wake.

 

Ama ikiwa mke huyo kajutia kosa lake na wewe bado unamuona anakufaa, na kama hiyo ni talaka ya kwanza au ya pili, basi upo uwezekano wa kumrejea na kuishi naye. Lakini ikiwa ni talaka ya tatu, basi hutoweza tena kumrejea hadi aolewe na mtu mwengine na aingiliane naye kindoa na atakapomwacha kwa khiyari yake na si kwa makubaliano na wewe au mapatano fulani, basi utaweza tena wewe kumuoa.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Mume Kasema Nikifanya Jambo Nimeachika, Nami Nimefanya Na Kumdanganya Kuwa Sikufanya, Nini Hukmu Yake?

 

 Talaka Ya Mume Aliyeniacha Wakati Wa Hasira

 

Mume Kamtamkia Mkewe Talaka Kisha Akataka Kumrejea Katika Eda, Mwanamke Anayo Haki Kukataa Kurudiana Na Mumewe?

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share