Mume Hajiwezi Je Mke Anaweza Kudai Talaka?
SWALI:
SALAM ALEYKUM NASHUKURU KWA KUINGIA ALHIDAAYA KUULIZA SWALI KATIKA HALI ZA KIISLAM, MIMI NINA NDUGU YANGU MSICHANA KAOLEWA KOTA ALIVYOKUWA ANA MIAKA 18 LAKINI KABAHATIKA TU KUZAA MTOTO MMOJA BAADA YA HAPO MUMEWE ALIKUWA HAWEZI TENA KUMUINGILIA ALIKUWA ANA MATATIZO YA KIUME INAFIKA MIAKA SITA SASA HAJAMGUSA MKEWE, NA MKE ANAMUOGOPA MUME SANA KACHOKA TENA IMEBIDI MKE ATOWE SIRI YA MUMEWE, LAKINI ANAMPENDA BADO SISI TULIVYOSIKIA HIVYO WAZEE WA MKE HATUKUFURAHI TUNAMUONA MTOTO WETU ANAPATA TAABU SANA ANAKOSA MAPENZI NA PIA YEYE KASHACHOKA KUSTAHAMILI MPAKA KAFIKA KUSEMA SIRI YA MUMEWE, MUME ANASEMA ANAJITAFUTIA DAWA ATAFAA LAKINI MWAKA WA SITA HUU HAMNA KILICHOMFAA. JE NAOMBA USHAURI WENU, NI HAKI MKE HUYO KUMUACHISHA? KIISLAM
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukran sana kwa swali lako hili nyeti sana katika mas-ala ya unyumba. Hakika ni kuwa huko si kutoa siri bali ni njia ya kupata ufumbuzi wa tatizo hilo. Na tatizo kama hili au jingine lolote baina ya mume na mke hafai mmoja wao kumuogopa mwengine kwani kufanya hivyo ni kumeza ushingo bila kupata usaidizi aina yoyote.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) wametupatia njia za kuweza kutatua matatizo yetu ili tuwe ni jamii na familia bora za kuweza kuzungumza kwa hali ya uwazi, hivyo, kuweza kutazama njia bora na kusuluhisha mzozo au kutatua tatizo. Mke hafai kumuogopa mume ila tu anataka amuheshimu au kwa vyema zaidi waheshimiane. Lau kama mke angeweza kuzungumza na mumewe basi hili tatizo halingeweza kufika mpaka muda wa miaka yote hiyo.
Tatizo la kupoteza nguvu za uume lipo na lina sababu nyingi zinazopelekea hilo. Na pia mara nyengine mke pia naye hukosa shauku ya kulala na kustarehe na mumewe. Tatizo hili si kuwa haliwezi kutatuliwa, laa! Jambo hili lina dawa.
Nasaha zetu ni kuwa mwanzo mume aende kwa daktari huenda ikawa ni tatizo ambalo linaweza kutatuliwa kwa kufanyiwa oparesheni au kwa madawa. Japokuwa madawa ya kuongeza nguvu za kiume nyingi zina madhara kwa mwanamume mwenyewe zikitumiwa kwa muda. Ikiwa njia hii haikuweza kutatua tatizo hilo basi aende kwa matwabibu ikiwa wapo katika sehemu anayoishi nao dawa zao zimejaribiwa. Mojawapo ya dawa hizo ni ile inayoitwa hawlinjaan. Hii anaweza kuchemshiwa na maji au ikatiwa katika maziwa akanywa nusu saa kabla ya jimai.
Ikiwa dawa hii pia haikufaa, huenda akawa labda amefanyiwa sihri na kufungwa ili asipate kufanya jimai na mkewe kwa sababu moja au nyengine. Kwa hiyo, mume anaweza kupelekwa kwa Shaykh ambaye anatibu kupitia kwa Qur-aan na du’aa sahihi za Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) na huenda hiyo ikiwa ni shifaa kwake.
Ikiwa njia zote hizo hazikufaa, mke na mume au wazazi wao wanaweza kukaa na kuzungumza jambo hilo ili mume amuache mke wake. Ikiwa haitafanyika hivyo mke atakuwa anadhulumika jambo ambalo halifai katika Uislamu. kwa msingi wa Kiislamu mtukufu ni ile kauli ya Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Haifai kudhuru wala kulipana madhara” Ibn Maajah, Maalik na ad-Daaraqutwniy).
Kudhulumu na kudhulumiwa ni mambo ambao hayafai kabisa katika Uislamu. Ikiwa mume amekataa basi mke anaweza kwenda kwa Qaadhi naye atawaachisha kwani kutoweza jimai kwa mume ni sababu tosha ya talaka.
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amuonyeshe dawa ndugu yetu na waendelee na ndoa katika hali iliyo mzuri kuliko awali na utesi na husma zote ziondoke.
Na Allaah Anajua zaidi