Sifa Za Muhsin Ni Zipi Na Je, Sifa Hizo Zinalingana Na Sifa Za Muumin.

 

SWALI:

As salaam aleykum

Nina swali linanisumbua sana kwa sababu niliota ndoto nzuri nikisisitizwa kutoacha kuwa muhsin. Kitu nina choelewa ni kuwa muhsin ni mtu mwema! na sijui hasa nini huo wema pamoja na mtu mwema sifa zake ni zipi na je sifa hizo zinalingana na sifa za mtu muumin? Tafaadhali kama mnaweza kunifahamisha kwa undani zaidi sna hata nikapata kutulia kiroho pamoja na kufuata nilivyo amrisha ktk ndoto hiyi na wabillahi tawfiq salam aleykum.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutaka kujua sifa za Muhsin.

Mwanzo hutakikani wewe kama Muislamu kutaka kuwa mwema kwa sababu ya kuota ndoto. Unatakiwa uwe mwema kwa sababu tayari Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wamekuamrisha uwe hivyo.

Muhsin ana daraja kubwa kuliko Muumini kumaanisha ni mtu aliye karibu zaidi na Allaah Aliyetukuka. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatufafanulia kuhusu Ihsaan pale alipoulizwa na Jibriyl (‘Alayhis salaam), akasema:

Ihsaan ni kumuabudu Allaah kama kwamba wamuona, ikiwa humuoni basi Yeye Anakuona” (Muslim).

Na Allaah Aliyetukuka Naye Akatuelezea kuwa Muhsin ni mwenye sifa zifuatazo:

1.     Wenye kutoa kwa siri na dhahiri,

2.     Wenye kuzuia khasira,

3.     Wenye kuwasemehe watu,

4.     Wenye kufanya uchafu au kudhulumu nafsi zao, wanamkumbuka Allaah na hawashikilii kwa walioyafanya nao wanajua (al-‘Imraan [3]: 134 – 135).

 

5.     Kuamini nguzo zote za Uislamu na kuzitekeleza.

6.     Kuamini nguzo zote za Imani na kuzifanyia kazi.

7.     Kumuabudu Allaah Aliyetukuka kama kwamba unamuona.

 

Na haya yote umeamrishwa na Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo yatekeleze bila kusita na ujira wako kwa Allaah Aliyetukuka ni mkubwa.

Na mwisho tunakunasihi usiwe ni mwenye kuendekeza ndoto na kuzifanyia kazi. Unachopaswa ni kusoma mafundisho na makatazo ya Uislamu kutoka katika Qur-aan na Sunnah na kutekeleza yote yale uliyoamrishwa kuyatekeleza na kuacha na kujiweka mbali na yote yale ambayo umkatazwa nayo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share