Mke Kumlazimisha Mumewe Atoe Talaka

SWALI:

 

Asalam Aliekum, Nawapa shukrani kwa kutuelimisha na majibu yenu mazuri Inshallah jaza yenu iko kwa Allah (S.W)

 

Mimi suali langu nikuhusu kuomba talaka. Nimeolewa na mume ambae hasikizani na mamangu ikanibidi nimuombe talaka. Mume mwenye hana shida yoyote yuwanipenda na mimi nampenda. Swali ni kuwa kama nina makosa yoyote nimefanya kwa kuomba hiyo talaka. Manake huyo mume alikuwa hatiki kunipa nimemlazimisha akanipa na alipo nipa aliniambia kuwa yeye hakuridhika na kiyeye nikama bado hajaniacha. Je talaka imepita na nimefanya makosa?

 

Maasalam Na Shukran Sana.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu wewe kumlazimisha mumeo kutoa talaka.

Mume kawaida anatakiwa atazame zile hisia za haraka haraka za wanawake hasa kutaka talaka bila sababu yoyote. Ikiwa umemlazimisha mumeo atoe talaka naye akatoa talaka basi talaka hiyo imepita pasi na wasiwasi wowote. Kwa kufanya hivyo wewe umepata madhambi ambayo inabidi uombe msamaha kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Mumeo ana nafasi ya kukurudia bila ya kulipa mahari kabla ya eda yako ya kuachwa kumalizika. Ikiwa eda imemalizika bado mumeo anaweza kukurudia ikiwa mtaonelea iwe kwa Nikaah mpya na mahari mapya isipokuwa kama utasema hutaki hayo mahari.

 

Ama kuhusu shida ya kuwa yeye hasikilizani na mamako ni suala ambalo linaweza kutatuliwa kwa nyinyi kukaa pamoja na kutazama shina ya tatizo hilo. Inatakiwa wanandoa wasikilizane na wakwe zao na familia za mwendani wao bila ya tashwishi. Ikiwa hakuna masikilizano basi ni tatizo lazima litatuliwe kwa njia iliyo nzuri na tija si kuomba talaka kiwepesiwepesi.

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

018 - Kutaka Talaka Bila Ya Kuwepo Tatizo Ni Jambo Lililoharamishwa Kishari’ah

Kuomba Talaka Bila Sababu

Kiwango Gani Mke Avumilie Maudhi Ya Mume? Na Sababu Zipi Za Kuomba Talaka?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share