Talaka Imepita Baada Ya Mwaka Anaweza Kumuoa?
SWALI:
s/a/w/w ama bada ya salamu mimi misoma maabobo mingi kuhusu talaqa lakini sijapata suali langu suali langu ni hili sheeqi wangu mutu akmwata mkewe ku talaqa moja hakusema rajaatu imepita miyaka 2 hoyo mke hakuolewa teen waka wonana na mumewe aliyemacha wan weza kurudiana na kiwa wanaweza kivipi na kiwa hawezi ni vipi ndgu zangu amaa masheqi wangu nipe ku uwaazi walilaahi toowfiiq s/a
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.
Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu talaka na mume kumrudia mkewe baada ya hapo. Hakika mume anapomuacha mkewe, Allaah Aliyetukuka Ameweka mfumo wa wao kurudiana bila ya ndoa mpya. Kwa ajili hiyo ikawa ni lazima kwa mke abakie katika nyumba ya mumewe katika kipindi cha EDA. Ikiwa mume anataka kumrudia kabla ya EDA kumalizika basi atakubaliwa kufanya hivyo bila ndoa mpya mbali na kuwa talaka imepita. Allaah Akiyetukuka Anasema:
“Na mtakapowapa wanawake talaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakayefanya hivyo, amejidhulumu nafsi yake” (2: 231).
Hilo halifanyiki wala kukubalika kisheria ikiwa talaka iliyotolewa ni ya tatu.
Ama ikiwa mtu amemuacha mkewe na EDA ikamalizika kwa kupitiwa na muda ulio zaidi ya miezi 3 basi kutakuwa hakuna tatizo ikiwa mume anataka kumrudia mtalaka wake. Katika hali hii itabidi mume apeleke posa mpya na mwanamke naye akubali kuolewa na mume huyo wake wa kwanza. Na mahari pia yatakuwa ni mengine watakayokubaliana. Allaah Aliyetukuka Anasema:
“Na mtakapowapa wanawake talaka nao wakamaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao endapo baina yao wamepatana kwa wema. Hayo anaonywa nayo yule miongoni mwenu anayemuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hayo ni bora zaidi kwenu na safi kabisa. Na Allaah Anajua, lakini nyinyi hamjui” (2: 232).
Kwa hiyo, mume anaweza kumrudia bila matatizo yoyote.
Na hapa unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu EDA na mas-ala ya Talaka:
Na Allaah Anajua zaidi