Nimempa Talaka Mke, Ananidai Niuze nyumba Na Shamba Ili Apewe Kiwango Kikubwa Cha Mata'aa (Kitoka Nyumba)
SWALI:
Asalaam alyakum
Mimi nimemuacha mke na nikachukulia ni jambo la kawaida nilimkanya kwa yale anayoyafanya nikafumilia kwa muda mrefu sana Allah shahidi juu ya hayo, ikafika muda nikamrejesha kwao ili akumbushwe wajib wake ktk ndoa, lakini hakubadilika nikaamua kumuacha, akenda kwa wasimimaizi wa Kiislamu kushtaki wakamua nimpe mutaa nikakubali na yeye akakubali na tukasaini, kabla sijaanza kulipa ile mutaa akarudi tena na kutoa masharti ya kiwango cha kulipwa ambacho mimi sikuwa na uwezo nacho na akasema nisipoweza hicho kiwango apewe barua aende mahakamani kesi bado inaendelea, mimi kwa kweli sikuweza hicho kiwango na sasa kaenda mahakamani lengo lake nyumba na shamba viuzwe ili tugawane sawasawa, hii ni sahihi au mimi nina kosa? Pia tumezaa watoto wawili na wote ninao mimi.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu talaka na mataa'a anayotaka mtaka wako. Hakika ni kuwa Uislamu una kanuni zake, na ada na mila zetu zina desturi zake. Uislamu uko wazi kabisa katika mas-ala ya talaka na hakuna shaka iliyobakia ndani yake. Pindi unapomuacha mkeo, unafaa uwe ni mwenye kumuweka kama mkeo mpaka eda yake imalizike. Ikiwa mtakubaliana kurudiana itakuwa kheri kwenu na lau mtaona kila mmoja ashike yake itakuwa hivyo.
Kuoana ni kwa wema na pia kuachana ni kwa wema. Allaah Aliyetukuka Anasema:
"Na mtakapowapa wanawake talaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakayefanya hivyo, amejidhulumu nafsi yake" (2: 231).
Na ama kitoka nyumba ikiwa ipo kupatiwa mke itakuwa ni ihsani upande wa mume na wala hafai kukalifishwa kwa asichoweza.
Allaah Aliyetukuka Anasema:
"Na mmehalilishiwa wasiokuwa hao, mtafute kwa mali yenu kwa kuoa pasina kuzini. Kama mnavyostarehe nao, basi wapeni mahari yao kwa kuwa ni wajibu. Wala hapana lawama juu yenu kwa mtakachokubaliana baada ya kutimiza wajibu" (4: 24).
Hapa Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha kuwa iliyo ya faradhi ni wanawake kupewa mahari wanapoolewa lakini chochote zaidi ya hayo hakuna lawama katika Shari'ah. Lakini kutopata lawama ni kusikilizana kwa njia nzuri na katika uwezo wa mume kwa awezacho.
Hakika ni kuwa kulingana na swali lako umempatia vya kutosha na ikiwa uwezo wako ni huo inakuwa hulazimiki kutoa cha ziada. Tatizo linakuja katika mas-ala ya kwenda mahakama za kikafiri ambazo kanuni zake nyingi si za uadilifu kwa sababu moja au nyingine. Nasaha yetu ni kuwa labda nawe ufanye haraka kwenda kwa Mashaykh wanaojulikana kwa elimu na uadilifu wao ili waamue kesi hii yenu.
Kiungo kifuatacho kinaelezea hukmu za Mut'ah (kiliwazo/kitoka nyumba):
Mut'ah (Kiliwazo, Kustarehea, Kitoka Nyumba, Masurufu) Ya Kumpa Mke Anayeachwa
Tunakutakia kila la kheri na fanaka.
Na Allaah Anajua zaidi