Anataka Talaka Kwa Mumewe Ili Aolewe Na Mimi

SWALI:

As salaam aleikum warahmatuLLAHف wabarakatuh,naanza kuuliza swali  au duduku langu kwa jina la M/MUNGU.(s.a)
               

Ndugu zangu waislam,hakika M/MUNGU pekee ndie anaejuwa jinsi gani ninavyo mpenda yeye pamoja  na  Bwana MTUME(s.a.w) ktk maisha yangu,sitaki kuelezea sana isije ikawa ni kama ria.
   

Ndugu zangu waislam ningeomba mnisaidie kwa kunichangia mawazo ambayo hata kama Bwana MTUME(s.a.w)angekuwa hai angeweza kukubaliana nayo.Nikwamba toka nizaliwe nashukuru kuwa sijapata kuwa na  mwanamke,lakini miaka 2 iliyopita nilitaka kuposa kwa waschana 3 lakini kila mmoja alikataa kwa sababu mbalimbali,hivyo nikaamuwa kusafiri ili kuzidi kuboresha maisha yangu japo kuwa kabla ya hapo nilikuwa na kazi.Sasa hapa nilipo nimebahatika kuweza kuwasiliana na mtoto wa shangazi yangu ambae hatukuwasiliana kwa mda wa miaka mingi yaani toka yeye na umri wa miaka 8,na sasa ana miaka 21 na mimi ni 24.Namawasiliano hayo yameanza miezi 2 toka sasa,na ni kwanjia ya computer(msn),sasa yeye kaolewa takriban miaka 2 kabla.Lakini anasema kuwa hapendwi na mumewe,hivyo baada ya kuanza kuwasiliana nami,ameanza kugubikwa na mapenzi dhidi yangu,na ni mapenzi ya kweli kweli kiasi ambacho mimi nilidhani ni maskhara lakini ni kidhati kabisa,mpaka mimi kishaanza kunitia wasiwasi.

Hivi punde kabla sijaanza kuandika barua hii amenipigia simu na kuniuliza kwamba endapo mumewe akimuachanitamuowa?  
   

Ndugu zangu waislam,kama nilivyo tangulia kusema kuwa mimi ninamapenzi sana na M/MUNGU na MTUME wake,nilimjibu kuwa mimi nisingependa kuwa yeye awachwe na mumewe, basi aliangusha kilio mpaka mimi akaanza kunitowa machozi,siku zote huwa namwambia kuwa M/MUNGU hatokuwa radhi kuwa uwachwe kwa maksudi kisha mimi nikuowe.Na kwa kweli mimi pia nampenda huyu cousin wangu,lakini nakhofia kuwa M/MUNGU na Bwana MTUWE(s.a.w)wasije wakanikasirikia na uhusiano wangu na wao ukawa dhaifu kwani hakika nitapata tabu duniani na akhera.Nimejitahid kumshauri kuwa aelekeze mapenzi kwa mumewe lakini  anasema haiwezekani madhali mimi nipo hai duniani.


 Swali langu linakuja kwamba vipi nitaweza kuepukana na hali hii ili nisiharibu uhusiano na mapenzi dhidi ya M/MUNGU na Bwana MTUME(s,a,w)???
 


JIBU:

 

  بسم الله الرحمن الرحيم الحمد لله والصلاة والسلام على أشرف الأنبياء والمرسلين وعلى آله وصحبه أجمعين و بعد

Tunamshukuru Allaah kuona ndugu zetu wengine khaswa vijana wako katika msimamo wa dini yao na kwamba wako katika Iymaan na kukhofu kumuasi Allaah سبحانه وتعالى na Mtume Wake صلى الله عليه وآله وسلم.

Kwanza, lazima tufahamu kwamba mawasiliano baina ya mwanamke na mwanamue bila ya kuwa ni mahram wake mtu (mwenye uhusiano wa damu, yaani asiyeweza kumuoa/kuolewa naye) ni jambo lililokatazwa katika dini yetu kama hivyo kuwasiliana katika msn na kadhalika, kwani ndio huwa sababu ya kufikia mabaya ya aina nyingi. Ama ikiwa mawasiliano yatakuwa ni kwa ajili ya kufundishana mambo ya dini na kukatazana mabaya au kuamrishana mema  basi hakuna ubaya kufanya hivyo. 

Maelezo yako yanaonyesha na kufahamika ifuatavyo:

1)     Kwamba umejitahidi kabisa kumueleza mtoto wa shangazi yako kwamba haitokuwa vyema yeye kuachika kwa mumewe ili umuoe wewe na juu ya hivyo haikusaidia kitu na bado yuko katika hali ya kusisitiza.

2)    Mtoto wa shangazi yako huyo hapati mapenzi kutoka kwa mumewe, na bila shaka yeye pia hana mapenzi na huyo mume kwani imeshamdhihirikia mapenzi yako.

3)     Wewe vile vile unampenda na uko tayari kumuoa ila tu uko katika khofu ya kumuasi Mola Wako.

Kwanza kabisa tutatambue kwamba talaka sio jambo jema na ni jambo la kuchukiza katika dini yetu. Yanapotokea matatizo baina ya mume na mke, inatakiwa kabla ya kuamua talaka kwanza ifanyike sulhi baina ya mume na mke, na ikiwa haikuwezekana kupatikana sulhi baina yao, basi wawaite wazazi au jamaa zao ili wajaribu kwanza kupatanisha na ndoa irudi katika hali ya usalama kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى  :

((وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُواْ حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلاَحًا يُوَفِّقِ اللّهُ بَيْنَهُمَا إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا))  

((Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Mwenyezi Mungu Atawawezesha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye khabari)) [An-Nisaa: 35]   

Kisha tena ikiwa haikupatikana sulhi, au ndoa imerudia tena na tena kubakia katika matatizo hapo tena ndio ifikiriwe talaka.

Na ikiwa mumewe atamuacha, yaani atampa talaka, basi hakuna ubaya kwenu kuoana. Mfano tunao katika Siyrah ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika ndoa ya bibi Zaynab Bint Jahsh na Swahaba Zayd ibn Haarithah رضي الله عنه ambao walifungishwa ndoa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم 

Jibu ni kwamba, ikiwa hali ni hiyo na ikiwa mumewe atamuacha, yaani atampa talaka, basi hakuna ubaya kwenu kuoana. Mfano tunao katika Siyrah ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika ndoa ya bibi Zaynab Bint Jahsh na Swahaba Zayd ibn Haarithah رضي الله عنه ambao walifungishwa ndoa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم .

Bibi Zaynab alikuwa ni mtoto wa Umaymah bint 'Abdul-Muttwalib, shangazi yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na alipenda amfungishe ndoa na Zayd bin Haarithah ambaye alikuwa ni mtumwa aliyekuwa huru na ambaye alimlea mwenyewe tokea mdogo.

Ndoa hiyo ilidumu kwa muda wa mwaka tu, kwani kulikuwa hakuna mapenzi upande mmoja, yaani Zaynab alikuwa hana mapenzi na Zayd, hivyo mashaakil yakaanza kujitokeza na kila mara Zayd alikuwa akienda kushtaki kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akimpa majibu ya kuwa ashikamane naye bado, mpaka tena Allaah سبحانه وتعالى Alipomuamrisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuwa baada ya kuachika Zaynab kwa Zayd bin Haarithah amuoe yeye. 

Jambo hili likuwa gumu sana kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akawa anaficha amri hii ya Allaah سبحانه وتعالى katika nafsi yake hadi ikateremka aya ya kudhihirisha haya yote:

 ((وَإِذْ تَقُولُ لِلَّذِي أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِ وَأَنْعَمْتَ عَلَيْهِ أَمْسِكْ عَلَيْكَ زَوْجَكَ وَاتَّقِ اللَّهَ وَتُخْفِي فِي نَفْسِكَ مَا اللَّهُ مُبْدِيهِ وَتَخْشَى النَّاسَ وَاللَّهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَاهُ فَلَمَّا قَضَى زَيْدٌ مِّنْهَا وَطَرًا زَوَّجْنَاكَهَا لِكَيْ لَا يَكُونَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ حَرَجٌ فِي أَزْوَاجِ أَدْعِيَائِهِمْ إِذَا قَضَوْا مِنْهُنَّ وَطَرًا وَكَانَ أَمْرُ اللَّهِ مَفْعُولًا))

 ((Na ulipomwambia yule Mwenyezi Mungu Aliyemneemesha,   nawe ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini mwako Aliyotaka Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zayd alipokwisha haja naye tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapokuwa wamekwisha timiza nao shuruti za talaka. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa)) [Al-Ahzaab: 37]

Ingawa pia lengo mojawapo katika amri hii ilikuwa ni kuondosha mila ya tabanniy (mtoto wa kupanga yaani (adoption) kisha awe kama aliyehusika kwa damu) iliyokuwa ikifuatwa zama hizo,  lakini pia ni Rahma ya Allaah سبحانه وتعالى kwa viumbe vyake kutujaalia kuwa na talaka katika maisha yetu ya ndoa ili inapokuwa ndoa haina masikilizano, mapenzi, utulivu huwa haina haja ya kujikalifisha mtu kwa mwenzake. Na talaka huleta faida kwa wote, kwani pengine wote wawili wapate kuoa/kuolewa na mtu mwingine ambaye wataweza kuwa na maisha bora zaidi ya kindoa yenye ukamilifu na khaswa itakayopatikana mapenzi ndani yake.

Na kwa niya hiyo yenu na jinsi hali ilivyo pande zote, mtakuwa hamkumuasi Mola wenu. Na ni vizuri kukimbilia haraka kumuoa baada ya yeye kupata talaka na kutimiza Eda yake ya talaka.

 

 Wa Allaahu A'alam

 

Share