Mke Aliyetelekezwa Na Mumewe Kwa Miaka 17 Ana Eda?
SWALI:
Mume alimwaga mkewe (mama yangu mdogo) kwenda tafuta maisha 1999. Baada ya kupita muda wa miaka miwili bila mawasiliano yoyote wala matunzo, Ndipo tulipopata taarifa kuwa ana familia nyingine huko (alikokwenda) na kuitelekeza familia yake ya mwanzo bila kutowa talaka (aliposhauriwa pia alikataa) kwa miaka 17! (Amewacha watoto hivi ana wajukuu). Imekuja taarifa a few days ago Mumewe amefariki je mke alie telekezwa kiasi hichi astahili kukaa eddeh?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Matatizo ya ndoa yamekithiri katika jamii zetu kwa kiasi na kiwango cha kutisha sana. Ilikuwa wakati na kipindi chote hicho ambacho alikuwa haangaliwi aende kwa Qaadhi au msomi wa Kiislamu ili amuelekeze. Hiyo ilikuwa ni dhuluma anadhulumiwa mama huyo aliyekaa kwa muda mrefu kama huo. Ilikuwa ni haki yake kuitafuta na kuitaka talaka kutoka kwa mume asiyemwangalia hata chembe.
Lakini hayo yamepita na mpaka mumewe amefariki, mume hakutoa talaka wala mke hakwenda kujiachisha. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Uislamu bado huyo ni mke wa mtu mbali na kuwa amedhulumiwa. Linalohitajika ni yeye kukaa eda na kisheria pia anafaa arithi fungu lake maalumu ambalo kwa kuwepo watoto na mke mwenziwe apate 1/16 ya mali yaliyoachwa na aliyefariki mumewe. Hata ikiwa hakupata haki kwa sababu moja au nyingine itambidi pia akae eda hiyo ya miezi minne na siku kumi (miezi 4 na siku 10).
Tunamtakia afueni mama yetu aliyefiliwa na mumewe na pia tunamuombea baba aliyeaga dunia kufutiwa kwa madhambi yake na subira kutoka kwa watoto walioachwa.
Ushauri etu wa mwisho kwa mfiliwa ni kuwa dhuluma iliyopita imepita amsamehe aliyefariki kwa yote aliyomfanyia. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amlipe subira na uvumilivu kwa hayo.
Na Allaah Anajua zaidi