Talaka Kwa Mume Kurejea Matendo Maovu

 

 

SWALI:

Suali langu maudhui yake ni nafikiri niliandika mke akimuambia mumewe nikifanya kitu fulani umeniwacha je inasihi ni kuhusu talaka suala la kwanza lilikua ni hili  mume akikuacha  akikurejea palepale akikuambia nimekurejea inasihi  na la pili  ni nilijua mume wangu kama na wanawake tukagombana  akaniambia hafanyi tena sasa mmnikamuambia nikija kujua kama unaendelea bc umeniwacha akanijibu ee baada ya muda nimeona kama anaendelea sasa hii ni talaka/ ahsanteni sana.

 



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako dada yetu ikiwa tutakuwa tumekosea kwa chochote kwa kutolifahamu swali lako utatuwekea wazi. Swali hili lina utata kidogo kwa kuchanganywa maneno na hivyo kutofahamika kama inavyostahiki.

Tunawaomba ndugu zetu wenye kuuliza maswali wawe ni wenye kuuliza kwa njia ambayo itaeleweka kwa uwazi kabisa. Ama kuhusu maswali yako ambayo ni takriban matatu, majibu yake ni kama yafutayo:

Kuhusu swali la kwanza, ni kuwa talaka huwa katika Uislam haitoki kwa mke. Mke akimwambia mumewe ukifanya jambo fulani itakuwa umeniacha hapo hakuna talaka. Na mambo kama haya si mazuri kabisa kwa Muislam kuyafanya kwani yanaondoa mapenzi na huruma baina ya wanandoa.

Mume ndiye aliyepewa haki ya kutoa talaka na anapaswa kuitumia kwa njia iliyo nzuri kabisa. Haifai kwake kuitumia kwa njia ambayo sio nzuri. Talaka inatolewa tu ikiwa wanandoa hawawezi kuishi kwa njia iliyo nzuri pamoja. Hivyo mume akikuambia kuwa amekuacha basi utakuwa umeachika, na kwa hekima Aiujuayo Allaah Aliyetukuka Akaweka kuwa mume anaweza kumrudia mkewe katika kipindi cha eda bila ya Nikaah mpya. Kwa hiyo, mume akikuacha kisha papo hapo akasema amekurudia inasihi bila tatizo lolote.

Ikiwa kuna talaka iliyowekewa sharti kama hapo ulivyosema kuwa alikubali kuwa akiwa ataendelea na tabia ya kuwa na wanawake nje ya ndoa atakuwa amekuacha. Hivyo, ikiwa atakuwa na mwenendo huo ambao pia unaweza kumletea madhara makubwa yeye na wewe pia talaka itakuwa imepita. Lakini kwa kupita talaka, ni lazima wewe uwe una hakika ya hilo unalomtuhumu nalo, na pia umweleze wazi kuwa unataka talaka yako. Hivyo, inabidi uzungumze naye kwa uwazi ukiwa kama mkewe na akiungama kuwa bado yupo katika tabia hizo na kuwa ndio amekiri kuwa ukijua wewe basi ndio kakubali kuwa ni talaka yako. Hivyo itakuwa hapana ndoa baina yenu.


 
Na Allaah Anajua zaidi

 

Share