Mataa'u (Kiliwazo, Kistarehea, Kitoka Nyumba, Masurufu) Ya Kumpa Mke Anayeachwa

 

Mataa'u  au Mut'ah Atw-Twalaaq

(Kiliwazo, Kitoka Nyumba, Masurufu) Ya Kumpa Mke Anayeachwa

Alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:  

 

Assalam alaikum, nashukuru kupata fursa hii ya kutaka kupata mwangaza juu ya dini yetu ya kiislamu, pia napenda kwapongeza na kuwaombea kwa Allah kwa kazi nzuri ya kuelimisha umma wa kiislamu.

swali langu : je unapotoa talaka zipo haki zozote kwa mwanamke uliemwacha? Au kuna fidia yoyote untakiwa kumpa mwanamke?

ukizingatia amekuzalia? waillah tawfi

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tunashukuru kwa swali lako zuri na muhimu na tutajaribu kulijibu kwa kirefu In Shaa Allaah.

 

Mume na mke wanapoachana, inawapasa waachane kwa ihsaan na si kwa ugomvi au kudhulimiana kama tunavyoona mara nyingi katika jamii yetu. Watu kugombana, kuvutana, kukhasimiana na kufedheheshana. Makatazo ya kutendeana uovu katika hali ya talaka na maamrisho ya kutendeana wema ni maelekezo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) Anayesema:

((وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النَّسَاء فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ سَرِّحُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ))

((Na mtakapowapa wanawake talaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema)) [Al-Baqarah: 231] 

 

 

Yapasayo kufanywa ni kama yafuatayo:

 

1. Kupewa mke mahari yaliyosalia ikiwa hayakukamilishwa:

 

((وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إَلاَّ أَن يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَ الَّذِي بِيَدِهِ عُقْدَةُ النِّكَاحِ وَأَن تَعْفُواْ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى وَلاَ تَنسَوُاْ الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ إِنَّ اللّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ))

((Na mkiwapa talaka kabla ya kuwagusa, na mmekwisha wawekea hayo mahari makhsusi, basi wapeni nusu ya mahari mlioagana, isipokuwa ikiwa wanawake wenyewe wamesamehe, au mume ambaye kifungo cha ndoa ki mikononi mwake awe amesamehe. Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na taqwa. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Allaah   Anayaona mnayoyatenda)) [Al-Baqarah: 237]

 

 

2. Kupewa mke "Mataa’u" (kitoka nyumba au masurufu ya talaka). Hii "Mataa'u" au "Mut'ah Atw-Twalaaq" (kiliwazo, kitoka nyumba) ni tofauti na ile "Mut'ah" (ndoa ya muda) wanayofanya Mashia ambayo wao wanaweza kuoana kwa masiku machache au hata kwa masaa machache tu. Ndoa hiyo imeharamishwa kabisa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hapa "Mut’ah Atw-Twalaaq au Mataa'u" ina maana ni kile ‘Kiliwazo’ au ‘Kistarehea’ na pia inajulikana kama ‘Kitoka Nyumba’ au ‘Masurufu ya Talaka’ anachopewa mwanamke pindi anapoachwa na mumewe.

 

((وَلِلْمُطَلَّقَاتِ مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ))

((Na wanawake walioachwa wapewe cha kuwaliwaza kwa mujibu wa Shariy'ah. Haya ni waajibu kwa wenye taqwa)) [Al-Baqarah: 241]

 

 

3. Kuachwa katika twahara yake bila kuingiliwa na kuhudumiwa mke kwa chakula, mavazi, makazi kama kawaida hadi eda yake imalizike ikiwa alishaingiliwa na abakie nyumbani kwa mumewe na si kumuondosha. Kwa maana jukumu la kumhudumia ni la mume. Ama ikiwa hakuwahi kuingiliwa basi hana haja ya kukaa eda. 

 

((يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاء فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ وَاتَّقُوا اللَّهَ رَبَّكُمْ  لَا تُخْرِجُوهُنَّ مِن بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ إِلَّا أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ))

((Ee Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hesabu ya eda. Na mcheni Allaah, Mola wenu. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi)) [Atw-Twalaaq: 1]

 

 

4. Kuachiwa mke achukue vitu vyake mwenyewe na vile alivyopewa na mumewe kwa mapenzi, hapana ruhusa kumnyang'anya. Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa):

 

((الطَّلاَقُ مَرَّتَانِ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ وَلاَ يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَأْخُذُواْ مِمَّا آتَيْتُمُوهُنَّ شَيْئًا إِلاَّ أَن يَخَافَا أَلاَّ يُقِيمَا حُدُودَ اللّهِ))

((Talaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlichowapa wake zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Allaah)) [Al-Baqarah: 229]

 

 

Kinachotolewa katika "Mut’ah Atw-Twalaaq" au "Mataa'u" na hukmu zake:

 

"Mut’ah Atw-Twalaaq" au "Mataa'uni mali inayotolewa na mume pindi anapomtaliki mke wake iwe kama ni kiliwazo. Na inaweza kuwa ni pesa, nguo au chochote cha kumliwaza mke.

 

 

Ama katika hukmu yake 'Ulamaa wamekhitilafiana katika kauli tatu zifuatazo:

 

Ya kwanza: "Mut’ah Atw-Twalaaq" au "Mataa'uni waajib kwa kila anayetalikiwa:

 

Hii ni rai ya 'Aliy bin Abiy Twaalib, Hasan, Sa'iyd bin Jubayr, jamaa katika Salaf, Abuu Thawr, Adhw-Dhwaahiriyyah nayo ni riwaaya kutoka kwa Ahmad na ameipa nguvu Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah kutokana na Ayaah kwa ujumla zinazoamrisha. Dalili ni maneno ya Allaah (Subhaanu wa Ta’aalaa):

 

((وَلِلْمُطَلَّقَاتِ مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ))

((Na wanawake walioachwa wapewe cha kuwaliwaza kwa mujibu wa Shariy'ah. Haya ni waajibu kwa wachaji Allaah.)) [Al-Baqarah: 241]

 

 

Ya Pili: "Mut’ah Atw-Twalaaq" au "Mataa'u" inapendekezeka kwa kila mtaliki lakini si waajib:

 

Hii ni rai ya madhehebu ya Maalik, Al-Layth bin Sa'iyd na Shurayh. Nao wamechukulia kauli za Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) zinazomalizia kusema kuhusu Mataa'u kwamba ni:   

 

(( ... مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ))

((…wapewe cha kuwaliwaza kwa mujibu wa Shariy'ah. Haya ni wajibu kwa wenye taqwa)) [Al-Baqarah: 241]

 

Na pia:

 ((... مَتَاعاً بِالْمَعْرُوفِ حَقّاً عَلَى الْمُحْسِنِينَ))

((…maliwaza kwa mujibu wa desturi kuwa ni haki juu ya watendao mema)) [Al-Baqarah: 236]

 

Hivyo wameona kwamba kutekeleza ni kufanya wema.

 

 

Ya tatu: "Mut’ah Atw-Twalaaqau "Mataa'u" ni waajib kwa Mufawadhwah – Naye ni yule mwanamke aliyeachwa kabla hajaingiliwa na ambaye alikuwa hajapangiwa mahari – kinyume na yule aliyekuwa tayari mahari yake yameshapangwa yanajulikana.

 

Nayo ni madhehebu ya Abuu Haniyfah na wafuasi wake, Ash-Shaafi'iy, Al-Awzaa'iy na Ahmad katika riwaayah ya jamaa kutoka kwake. Nayo ni kauli ya Ibn 'Umar, Ibn 'Abbaas na kundi miongoni mwa Salaf. Nao wametoa hoja kutokana na kauli ya Ibn 'Umar:

 “Kila mtalakiwa (mwanamke aliyeachwa) apate "Mut’ah Atw-Twalaaq" au "Mataa'u" isipokuwa aliyetalikiwa bila ya kuingiliwa na ambaye mahari yake yashapangwa (ametajiwa mahari yake) huyo anatakiwa apate nusu ya mahari, na yeye hapati "Mut’ah Atw-Twalaaq" au "Mataa'u"”  [Isnaad Swahiyh imetolewa na Atw-Twabaaraniy].  

 

Katika hizo, rai iliyo na nguvu na sahihi zaidi ni kwamba "Mut’ah Atw-Twalaaqau "Mataa'u" ni waajib kwa kila mtalakiwa (mwanamke aliyepewa talaka), iwe aliingiliwa au hakuwahi kuingiliwa, na iwe mahari yake yalikwishapangwa au hayakupangwa. Lakini yatupasa tuzingatie kuwa anachopasa kupata aliyeachwa kabla hajaingia kwenye "Mut’ah Atw-Twalaaqau "Mataa'u" (kiliwazo au masurufu ya talaka) kinatakiwa kisizidi zaidi ya nusu ya mahari yaliyopangwa. Hii ni kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa):

 

((وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إَلاَّ أَن يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَ الَّذِي بِيَدِهِ عُقْدَةُ النِّكَاحِ وَأَن تَعْفُواْ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى وَلاَ تَنسَوُاْ الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ إِنَّ اللّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ))

((Na mkiwapa talaka kabla ya kuwagusa, na mmekwisha wawekea hayo mahari makhsusi, basi wapeni nusu ya mahari mliyoagana, isipokuwa ikiwa wanawake wenyewe wamesamehe, au mume ambaye kifungo cha ndoa ki mikononi mwake awe amesamehe. Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchaji Allaah. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Allaah Anayaona mnayoyatenda)) [Al-Baqarah: 237]

 

Na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) Amewajibisha waliotalakiwa ambao hawakuingiliwa wapewe "Mataa'u" (kiliwazo) na pia Ameeleza kuwa hawahitajii kukaa eda, Amesema katika kauli Yake:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا))

((Enyi walioamini! Mkiwaoa wanawake, Waumini, kisha mkawapa talaka kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayoihesabu. Basi wapeni cha kuwaliwaza, na muwaache kwa kuachana kwa wema)) [Al-Ahzaab: 49]

 

Kwa hiyo "Mut’ah Atw-Twalaaqau "Mataa'u" anapotalakiwa mke ima itakuwa ni iliyokadiriwa au isiyokadiriwa, na Aayah zinazohusu katika Suwratul-Baqarah zimebainisha apasaye kupewa nusu ya mahari ikiwa katalikiwa kabla ya maingiliano. Ama asiyetajiwa mahari "Mut’ah Atw-Twalaaqau "Mataa'u" yake ni ya kukadiriwa bali akipenda mume ampe kwa kadiri ya uwezo wake kama ilivyo katika Aayah ifuatayo:

 

((لاَّ جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاء مَا لَمْ تَمَسُّوهُنُّ أَوْ تَفْرِضُواْ لَهُنَّ فَرِيضَةً وَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعاً بِالْمَعْرُوفِ حَقّاً عَلَى الْمُحْسِنِينَ))

((Hapana ubaya kwenu mkiwapa talaka wanawake ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari yao. Lakini wapeni cha kuwaliwaza, mwenye wasaa kadiri awezavyo na mwenye dhiki kadiri awezavyo - maliwaza kwa mujibu wa desturi kuwa ni haki juu ya watendao mema)) [Al-Baqarah: 236]

 

Tunaweka maelezo ya mukhtasari ya wa mas-alah haya ili ieleweke vizuri zaidi katika taratibu ifuatayo:

 

 

Hukmu Ya  "Mataa'u" au "Mut’ah Atw-Twalaaq" (Kiliwazo, Kitoka Nyumba, Masurufu Ya Talaka)

 

Hali Ya 1:

Nikaah imefungwa, maingiliano hayakutendeka, mahari hayakubainishwa.

Hukmu Yake: Alipwe kadiri ya uwezo wa mume na pia mwanamke hahitaji kukaa eda.

 

Hali Ya 2:

Nikaah imefungwa, maingiliano hayakutendeka, mahari yamebainishwa.

Hukmu Yake: Nusu Ya mahari yaliyobainishwa. Pia hana haja ya kukaa eda.

 

Hali Ya 3:

Nikaah imefungwa, maingiliano yametendekea, mahari yamebainsihwa.

Hukmu yake:  Mahari yalipwe kamilifu.

 

Hali ya 4:

Nikaah imefungwa, maingiliano yametendeka, mahari hayakubainishwa.

Hukmu yake: Apewe mahari yanayolingana na mahari waliopewa wanawake wengine katika familia yake.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share