Nimemaliza Eda Ya Talaka Lakini Bado Ananipigia Simu, Je Inafaa?

SWALI:

Waalaikum salaam,

Hamukuwahi kinijibu swala langu la pili,sasa tumewachana na mume wangu muna advise gani au duas gani mwaweza kunipatia.

Ameniuliza kama aweza kunipigia simu on and off ,mimi nimemkatalia kwani nishamaliza iddah sasa,na mimi  si mkewe tena.

 


 

JIBU:

 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza tunaomba samahani sana kwa kuchelewa kukujibu swali lako la pili, lakini sababu tushaweka kwenye tangazo kuwa ni vigumu kujibu maswali yote haraka kama mnavyotaka au kutarajia, kutokana na kuwa na maswali mengi yaliyomo ambayo yanasubiri kujibiwa. Na wenye kuyajibu ni wachache tena wana shughuli nyingi sana.

Nasiha njema za kukupa dada yetu ni kuwa ubakie katika taqwa (ucha Mungu) kila wakati kwa kujichunga kila upande, katika hijaab yako ya kisheria, kujihifadhi mwili wako na kila aina ya mapambo kitendo ambacho kitakupeleka kwenye fitna.  

Mkumbumbuke sana Allaah سبحانه وتعالى asubuhi na jioni kwa kusoma sana Qur-aan, nyiradi za Sunnah na Du'aa nyingi ili Allaah سبحانه وتعالى  Akuruzuku mume mwenye kheri na wewe, ikiwa ni kurudiana naye mumeo wa mwanzo madam hajakuacha mara tatu au ukajaaliwa kupata mume mwingine Atakayekujaalia Allaah سبحانه وتعالى .

Ama kuhusu kutaka kukupigia simu na kuzungumza na wewe na hali umeshamaliza eda yako, kama ulivyotambua kuwa sasa wewe si mkewe tena, hivyo yeye si mahram wako. Kwa hiyo haiwapasi nyinyi kuwasiliana kwa aina yoyote. Kuwa na khofu ya kutaka kumridhisha Allaah سبحانه وتعالى  na sio kumridhisha binaadamu hata kama ni kipenzi vipi kwako. Kufanya hivyo utakuwa umedhihirisha mapenzi makubwa ya Mola Wako na umepata utamu wa iymaan kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

 ((ثلاث من كن فيه وجد حلاوة الإيمان : أن يكون الله ورسوله أحب إليه مما سواهما ، وأن يحب المرء لا يحبه إلا لله ، وأن يكره أن يعود في الكفر كما يكره أن يقذف في النار))    البخاري و مسلم   

 ((Yeyote atakayemiliki matatu (haya) atakuwa amepata utamu wa iymaan; awe Allah na Mtume Wake ni  Vipenzi kwake kuliko chochote, mwenye kumpenda mwenzake kwa ajili tu ya Allah Pekee na mwenye kuchukia kurudia katika kufru baada ya Allah Kumuokoa, kama atakavyochukia kutupwa motoni)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share