Mahusiano Ya Uchumba Baina Ya Mwanamme Na Mwanamke

SWALI:

 

Assalam aleykum warahmatulah wabarakat,

hakika shukran ni za mwenyezi mungu (alhamdulilah), kuna ukht alikuwa na mahusiano ya uchumba na akhi na malengo yao ni kufunga ndoa insha'ala na walipendana kwa misingi ya dini, baada ya ahki kulipeleka swala hili kwa wazazi, wakawa wamemkatalia kwa kuwa hawakupenda kabila la huyo binti, kijana akaamua kuvunja mahusiano na ahadi hiyo ya ndoa. Kwa kutoa sababu kuwa asingeweza fanya dhambi ya kutowatii wazai wake, je maamuzi hayo ni sahihi? Pia nini anatakiwa kufanya huyu binti aliyeachwa hali ya kuwa ndugu zake baadhi wanafaham ana mchumba? Hakika binti huyo yuko katika wakati mgumu sana, anaomba msaada' insha, allah allah akufanyie wepesi ktk kumpatia majibu.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu mahusiano ya uchumba baina ya mwanamke na mwanamme.

Hakika hukutuelezea haya mahusiano ya uchumba ni ya aina gani kwani mengi yanatoka nje ya mipaka iliyowekwa na shari’ah yetu tukufu.  

Ama namna ya kumsaidia ndugu yetu katika huu mtihani. Tunaona kuwa hii imekuwa ni kheri kwa mume kukataa huo uchumba kwa wakati huu kwani ingekuwa matatizo makubwa kwa msichana kuweza kuendana na wakwe zake. Ni kheri kwa kuwa hivyo ndivyo alivyotaka Allaah Aliyetukuka:

Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui” (al-Baqarah [2]: 216).

Linalotakiwa ni kumfahamisha dada yetu kuwa huu ni mtihani na inafaa yeye awe na msimamo wa kushikamana na Dini. Pia achukue tahadhari asikubali kuingiliana katika uchumba na yeyote ila ikiwa mume kweli anataka kumuoa basi aende kwao akampose kishari’ah, kisha waanze kukaa kama mume na mke.

Mwanamme bila shaka amefanya makosa inabidi apatiwe nasaha aache tabia hiyo. Aombe msamaha kwa Mola wake na ajiondoe katika udanganyifu wa aina yoyote ule. Naye akitaka kuoa asiingie katika uchumba na mahusiano yake bali azungumze na familia yake kama anaona hilo ni muhimu na bila shaka ni muhimu ili asimpatie msichana matumaini ya bure.

Bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

Mawasiliano Na Mchumba Baada Kuposa Na Kabla Ya Ndoa

Mchumba Bado Hana Uwezo Kunioa, Je, Kuwasiliana Kabla Ya Ndoa Kunakubalika?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share