Zipi Sifa Za Sumayyah (رضي الله عنها) Shahidi Wa Kwanza Mwanamke Katika Uislaam

Zipi Sifa Za Sumayyah  Shahidi Wa Kwanza Mwanamke Katika Uislaam

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

A, alaikum, ningependa kujua historia ya bibi sumaiyya, na nasaba yake katika uislamu na ana sifa zipi? Ntashukuru nikijibiwa. wasal alaikum

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza tunakunasihi kutokufupisha maamkizi ya Kiislaam na Thanaa au kuwatakia Radhi Swahaba na mengineyo ambayo watu wanakosea kama hivyo. Jambo hilo limekemewa  na ‘Ulamaa wetu. Bonyea viungo vifuatavyo upate faida:

 

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Maandishi

Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu

 

Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alikuwa ni mtumwa wa Abu Hudhayfah bin ‘Abdillaah al-Makhzuwmiy. Na bwana wake alimsifu kuwa alikuwa mwanamke mwenye akili na fahamu nzuri sana.

 

Bibi huyu aliolewa na bwana aliyehamia Makkah kutoka Yemen kwa jina, Yaasir (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Yaasir alijenga urafiki na kuwa chini ya himaya ya Abu Hudhayfah. Baada ya kupita muda Yaasir alimuoa bi Sumayyah. Ndoa hiyo ilikuwa ni nzuri na kukapatikana masikilizano mazuri baina ya wanandoa hao. Walipata mtoto wa kwanza waliomuita ‘Ammaar, na baadaye wakapata ‘Abdullaah na Haarith.

 

Abu Hudhayfah alikuwa ni mtu mkarimu, mwenye huruma na mwenye kuwapenda. Kwa minajili hiyo akaiacha familia huru na akawa ni mwenye kuwasaidia kila wakati kwa hali na mali.

 

Kwa akili muruwa aliyokuwa nayo Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) hakuchelewa kusilimu pindi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoanza kuutangaza Uislaam. Panasemwa kuwa Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alikuwa mtu wa saba katika kusilimu jambo ambalo lilimpatia hadhi kubwa. Kusilimu kwake kulikuwa kwa dhati na Iymaan yake ilikuwa ni kubwa na kila alipopata misukosuko na mitihani alisimama imara kabisa juu ya hilo.

 

Familia hii ya Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) iliposilimu ilipata mitihani na mateso kwa ule udhaifu wao wa kinasaba kama walivyopata Waislaam wengine waliokuwa wenye nasaba duni au watumwa. Kwa ajili hiyo, Sumayyah, Yaasir na ‘Ammaar (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walilengwa na Maquraysh katika kupatiwa adhabu. Wakati mmoja Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipita sokoni akaikuta familia hiyo ya watu watatu ikiadhibiwa kwa adhabu kali sana. Hakuwa na la kuwafanya isipokuwa kuwapatia hima kwa kuwaambia: “Subirini, enyi familia ya Yaasir kwani mashukio yenu ni Peponi”.

 

Abu Jahl, adui wa Allaah ndiye aliyekuwa akimuadhibu sana Sumayyah bint Khabbaat (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), lakini Summayah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) hakuyumba yumba katika Iymaan yake bali alibakia katika uimara na istiqaamah (msimamo). Abu Jahl alijaribu sana kutumia nguvu na kumtisha ili aritadi lakini alikataa hayo bila ya kusita. Abu Jahl hakukubali ule ukweli kuwa mwanamke huyu mwenye Iymaan anaweza kumpuuza yeye kiasi hicho, na kwa hasira kali aliyokuwa nayo iliyojaa kifuani mwake alimdunga mkuki, hivyo kufa kwa kipigo hicho.

 

Na hivyo, akawa Muislaam wa kwanza kuuliwa kwa ajili ya Dini yake wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kufa kwake Shahidi ndicho kilichowapatia wengine ujasiri wa kuweza kusimama imara dhidi ya maudhi, mateso, kejeli na kuipita mitihani waliyokuwa wakikumbana nayo kutoka wka maadui.

 

Familia hii ilijitolea mhanga kwa ajili ya Uislaam, hivyo kuuliwa katika kuitetea Dini. Baba na mama, mama akiwa ndiye wa kwanza, sio katika familia tu bali kwa wakati wote mpaka ulimwengu utakapomalizika. Walijitolea mhanga ili waweze kuisimamisha haki na ukweli na pia kupata thawabu za Kesho Aakhirah.

 

Hao ndio waliotangulia kwa wema na wakatupatia sisi mfano mzuri wa Muislaam mwema na mzuri, mwenye akili, elimu na busara na kuwa na Iymaan ya kweli na matunda yake.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate historia yake na ya mumewe kwa maelezo mapana:

 

 

Sumayyah Ummu 'Ammaar (رضي الله عنها)

 

'Ammaar Bin Yaasir (رضي الله عنه)

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share