Ukimkumbuka Allaah Naye Atakukumbuka (Fadhila Za Dhikru-Allaah)

 

Ukimdhukuru Allaah Naye Atakukumbuka

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ﴿١٥٢﴾

 

Basi nidhukuruni na Mimi Nitakukumbukeni; na nishukuruni wala msinikufuru.” [Al-Baqarah: 152]

 

 

Je, kuna aliye bora zaidi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atukumbuke? Bila shaka hakuna, kwani Yeye Ndiye tunayemhitaji katika maisha yetu duniani na Aakhirah. Hivyo basi tujitahidi kumdhukuru kila siku, kila wakati kwani Yeye  (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuamrisha tumdhukuru kwa wingi.    Na Anatuahidi kuwa pindi tutakapomdhukuru,  Naye Atatukumbuka, Atazidi kutuongoza, Atatuteremshia Rahmah Zake, na Atatulipa malipo mema mengi duniani na Aakhirah. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا ﴿٤١﴾ وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٤٢﴾  هُوَ الَّذِي يُصَلِّي عَلَيْكُمْ وَمَلَائِكَتُهُ لِيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا ﴿٤٣﴾ تَحِيَّتُهُمْ يَوْمَ يَلْقَوْنَهُ سَلَامٌ ۚ وَأَعَدَّ لَهُمْ أَجْرًا كَرِيمًا ﴿٤٤﴾

 

“Enyi walioamini! (mlioamini)! Mdhukuruni Allaah kwa wingi wa kumdhukuru. Na Msabbihini asubuni na jioni. Yeye (Allaah) Ndiye Anakurehemuni, ns Malaika Wake (wanakuombeeni maghfirah na rahma) ili Akutoeni kutoka katika viza kuingia katika Nuru. Naye daima ni Mwenye kurehemu Waumini. Maamkizi yao Siku watakayokutana na Naye; ni “Salaam” na Amewaandalia ujira wa ukarimu.” [Al-Ahzaab: 41-44]

 

 

'Aliy bin Abi Twalhah ameripoti kuwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allahu 'anhumaa) amesema kuhusu Aayah:

 

اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا ﴿٤١﴾

“Mdhukuruni Allaah kwa wingi wa kumdhukuru.”

 

"Allaah Hakuwaamrisha waja Wake kutekeleza wajibu wowote bila ya kuweko mipaka iliyojulikana na Hupokea nyudhuru za wale wasioweza kutekeleza (wajibu huo). Ama kumdhukuru Allaah, Hakuweka mipaka na hakuna atakayekuwa na udhuru wa kutokuweza kumdhukuru Allaah isipokuwa atakayedhalilika kwa kupuuza na kudharau, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ

“mdhukuruni Allaah msimamapo, na mkaapo na mnapolala ubavuni mwenu..” [An-Nisaa:103]

 

Kwa maana; Mdhukuruni usiku na mchana, katika ardhi kavu au baharini, safarini au mnapokuwa  majumbani, katika hali ya utajiri au umasikini, katika hali ya maradhi au katika siha, kwa siri au hadharani; katika hali zote na mazingira yoyote, Allaah Anasema:

   وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٤٢﴾

“Na Msabbihini asubuhi na jioni.”

 

Mkifanya hivyo Yeye na Malaika Wake Watatuswalia." [At-Twabary 20: 280]

 

 

Swalaah ya Allaah kwa waja Wake ina maana: Anawasifu waja Wake kwa Malaika na pia maana nyingine ni Rahmah.  Swalaah kutoka kwa Malaika ina maana: ni du'aa zao na kutuombea maghfirah.

 

 

Na katika Hadiyth ifuatayo imethibiti kuwa Allaah (‘Azza wa Jalla) humkumbuka mwenye kumdhukuru:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ (( يَقُولُ اللَّهُ تَعَالَى: أَنَا عِنْدَ ظَنِّ عَبْدِي بِي وَأَنَا مَعَهُ إِذَا ذَكَرَنِي، فَإِنْ ذَكَرَنِي فِي نَفْسِهِ ذَكَرْتُهُ فِي نَفْسِي ، وَإِنْ ذَكَرَنِي فِي مَلَإٍ ذَكَرْتُهُ فِي مَلَإٍ خَيْرٍ مِنْهُمْ ، وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ بِشِبْرٍ تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ ذِرَاعًا، وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ ذِرَاعًا تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ بَاعًا، وَإِنْ أَتَانِي يَمْشِي أَتَيْتُهُ هَرْوَلَةً)) البخاري , مسلم, الترمذي و ابن ماجه

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, ((Allaah Ta’aalaa, Anasema: Mimi ni vile mja Wangu anavyonidhania. Niko pamoja naye Anaponikumbuka katika nafsi yake, Ninamkumbuka  katika nafsi Yangu, anaponikumbuka katika hadhara, Ninamkumbuka katika hadhara bora zaidi. Na anaponikaribia shibiri Ninamkaribia dhiraa; anaponikaribia dhiraa, Ninamkaribia pima, anaponijia kwa mwendo (wa kawaida) ninamwendea mbio)) [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]

 

    

Maonyo Ya Kughafilika Kumdhukuru Allaah

  

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaonya wale ambao nyoyo zao zimeghafilika na kumdhukuru Yeye; Anasema:

 

 

  فَوَيْلٌ لِّلْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُم مِّن ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ أُولَـٰئِكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٢٢﴾

“Basi ole kwa wenye nyoyo ngumu kutokumdhukuru Allaah. Hao wamo katika upotofu bayana.” [Az- Zumar: 22]

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye pia ametuonya katika Hadiyth nyingi, tutataja baadhi yake:

 

   قال صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ قَعَدَ مَقْعَدًا لَمْ يَذْكُرِ اللَّهَ فِيهِ، كَانَتْ عَلَيْهِ مِنَ اللَّهِ تِرَةٌ, وَمَنِ اضْطَجَعَ مَضْجَعًا لَمْ يَذْكُرِ اللَّهَ فِيهِ ، كَانَتْ عَلَيْهِ مِنَ اللَّهِ تِرَةٌ)) s

Amesema  Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam: ((Anayekaa kikao chochote kile asimdhukuru Allaah katika kikao hicho basi ana dhambi kutoka kwa Allaah, na anayelala sehemu yeyote ile kisha asimdhukuru Allaah wakati wakuinuka sehemu hiyo basi ana dhambi kwa Allaah))  [Hadiyth ya Abu Hurayrah(رضي الله عنه) Abu Daawuwd (4/264) [4856] na wengineo na taz. Swahiyh Al-Jaami’ (5/342) [6477].

 

 

Na pia,

 

قال صلى الله عليه وسلم: ((مَا جَلَسَ قَوْمٌ مَجْلِسًا لَمْ يَذْكُرُوا اللَّهَ فِيهِ وَلَمْ يُصَلُّوا عَلَى نَبِيِّهِمْ إِلَّا كَانَ عَلَيْهِمْ تِرَةً فَإِنْ شَاءَ عَذَّبَهُمْ وَإِنْ شَاءَ غَفَرَ لَهُمْ))  

Amesema Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam ((Hapana watu wowote wale, wanaokaa kikao kisha wasimdhukuru Allaah humo, wala wasimswalie Nabiy wao ila watakuwa wana dhambi. Akipenda Atawaadhibu na Akipenda Atawaghufuria))  [Hadiyth ya Abu Hurayrah(رضي الله عنه) At-Tirmidhiy [3380] na taz. Swahiyh At-Tirmidhiy (3/140]

 

Na pia,

 

وقال صلى الله عليه وسلم: ((مَا مِنْ قَوْمٍ يَقُومُونَ مِنْ مَجْلِسٍ لَا يَذْكُرُونَ اللَّهَ فِيهِ إِلَّا قَامُوا عَنْ مِثْلِ جِيفَةِ حِمَارٍ وَكَانَ لَهُمْ حَسْرَةً))

Na amesema  (صلى الله عليه وسلم): ((Hapana watu wowote wale wanaosimama katika kikao walichokaa, kisha wasimdhukuru Allaah ila watakuwa wanasimama kama mzoga wa punda, na watakuja juta [kwa kutokumdhukuru Allaah])) [Hadiyth ya Abu Hurayrah(رضي الله عنه)   - Abu Daawuwd (4/264) [4855], Ahmad (2/389) na taz Swahiyh Al-Jaami’ (5/176) [5750].  

 

Basi inatupasa tumdhukuru Allaah (‘Azza wa Jalla) kila wakati hata tunapokuwa tumo katika shughuli zetu tunaweza kumdhukuru, mfano unapoelekea kazini au mtu anapokuwa jikoni, anapotembea njiani na katika shughuli nyenginezo:   

 

 

Bonyeza kiungo kifuataco upate Kitabu cha Hiswnul-Muslim kilichokusanya kila aina za Dhikru-Allaah za kila nyakati, za kila hali na popote ulipo:

 

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

 

 

Baadhi ya Dhikru-Allash zenye thawabu nyingi:

 

 

Baadhi ya Adkhaar ambazo zina thawabu tele na muda wa kuzitamka hauzidi dakika moja!

 

 سُبْحـانَ اللهِ وَبِحَمْـدِهِ عَدَدَ خَلْـقِه ، وَرِضـا نَفْسِـه ، وَزِنَـةَ عَـرْشِـه ، وَمِـدادَ كَلِمـاتِـه

 

Subhaana-Llaahi wa Bihamdihi 'Adada Khalqihi wa Ridhwaa Nafsihi, wa Zinata 'Arshihi wa Midaada Kalimaatih [Taja mara tatu] [Muslim]

 

Namtakasa Allaah (na kila sifa hasi) na namhimidi kwa idadi ya Viumbe Vyake, na kwa idadi ya vilivyoridhiwa na Nafsi Yake, na kwa uzito wa ‘Arshi Yake, na kwa wingi wa wino wa (kuandikia) Maneno Yake. [Muslim]

 

Mfano mmoja tu wa thawabu zinazopatikana kwa kutamka hayo ni idadi ya viumbe vya Allaah. Je viumbe vingapi viliokuweko duniani tokea kuumbwa Nabiy Aadam (‘alayhis-salaam) hadi hivi sasa na idadi ya viumbe Atakavyoendelea kuviumba Allaah (‘Azza wa Jalla) mpaka Siku ya Mwisho? Zingatia idadi ya  Malaika, idadi ya wana-Aadam, idadi ya Majini, idadi ya wanyama wakubwa na wadogo wanaoishi nchi kavu na baharini, wanyama wa angani, idadi ya vidudu vidogodogo, idadi ya miti na mimea ya kila aina ulimwenguni kote. Mbali mengineyo Aliyoyaumba Allaah (‘Azza wa Jalla) kama mbingu, bahari, milima n.k.   

 

Pia bonyeza viungo vifuatavyo upate Adkhaar nyenginezo na faida tele: 

 

 

Adhkaar Zenye Thawabu Tele

 

130-Hiswnul-Muslim: Fadhila Za Tasbiyh, Tahmiyd, Tahliyl Na Takbiyr

 

129-Hiswnul-Muslim: Kuomba Maghfirah Na Kutubia

 

Du'aa Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

Fadhila Za Kumswalia Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم Na Vipi Kumswalia

Hiswnul-Muslim: Fadhila Za Kumdhukuru Allaah

 

 

 

 

Share