Adhabu Ya Kaburi
Adhabu Ya Kaburi
Imekusanywa Kutoka Katika Duruws Za
Imaam Muhammad Bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
Anasema Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu):
Zipo dalili nyingi sahihi zinazoelezea juu ya Adhabu ya kaburini. Allaah Anasema:
النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ﴿٤٦﴾
“Wanadhihirishiwa moto asubuhi na jioni, na Siku itakayosimama Saa (itasemwa): Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa.” [Ghaafir: 46].
Hii ni dalili katika Qur-aan kuwa Fir’awn na watu wake wanadhihirishiwa adhabu asubuhi na jioni kabla ya Siku ya Qiyaamah. Kwa sababu Aayah inaendelea kusema: “na Siku itakayosimama Saa” Maana yake ni kuwa hiyo adhabu iliyotajwa ya kudhihirishiwa Moto asubuhi na jioni ilikuwepo kabla ya Siku ya Qiyaamah.
Na katika Hadiyth nyingi Swahiyh Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Muombeni Allaah akukingeni na adhabu ya Moto.” Wakasema: Tunajikinga kwa Allaah na adhabu ya Moto. Akasema: “Muombeni Allaah Akukingeni na adhabu ya Kaburi.” Wakasema: Tunajikinga kwa Allaah kutokana na adhabu ya Kaburini. [Muslim]
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alisema juu ya Muislamu: “Anapanuliwa kaburini mwake kiasi cha upeo wa macho yake.” [Al-Bukhaariy]
Dalili kama hizi ziko nyingi sana, na haijuzu mtu kuzikanusha kwa ajili ya matamanio ya nafsi yake.
Adhabu ya kaburini ni ya kiroho na si jambo linalohusu mwili, na hii ndiyo sababu ikawa imani juu yake ni katika mambo ya ghaibu. Na hali ya mambo katika maisha ya Barzakh hayawezi kukisiwa kwa hali ya maisha yetu ya hapa duniani.
Isitoshe, adhabu ya kaburini na neema zake anayadiriki maiti peke yake na wanaadamu wengine hawawezi kuyaona wala kuhisi au kuyadiriki. Mfano wake ni sawa na mfano wa mtu anapoota usingizini. Anaota kuwa anakwenda anarudi, anapigwa anapiga. Anajiona yupo mahali penye nafasi kubwa na mara nyingine anajiona yupo penye nafasi ndogo iliyodhikika. Anayaona yote wakati walio karibu yake hawayaoni wala hawayahisi. (Mwisho wa maneno ya Imaam Ibn Uthaymiyn)
Kama ilivyoeleza Aayah ya adhabu wanayopata Fir’awn na watu wake hadi siku ya Qiyaamah, pia zipo Aayah nyingi zinazoelezea juu ya neema wanayopata Waumini na pia juu ya adhabu wanayopata makafiri wanapotolewa roho zao, na baada ya kutolewa roho zao.
Allaah Anasema:
وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ يَتَوَفَّى الَّذِينَ كَفَرُوا ۙ الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ﴿٥٠﴾ ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٥١﴾
“Na lau ungeliona pale Malaika wanapowafisha wale waliokufuru, wanawapiga nyuso zao na migongo yao na (wanawaambia): Onjeni adhabu iunguzayo. Hayo ni kwa yale (maovu) yaliyotangulizwa na mikono yenu; na kwamba Allaah si Mwenye kudhulumu waja.” [Al-Anfaal: 50-51]
Na Akasema juu ya Shuhadaa:
وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ ﴿١٦٩﴾ فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُوا بِهِم مِّنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴿١٧٠﴾
“Na wala usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu, bali wahai, kwa Rabb wao wanaruzukiwa. Wanafurahia kwa Aliyowapa Allaah kwa fadhila Zake na wanawashangilia ambao hawajaungana nao, walio nyuma yao, kwamba: Hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.” [Aal-Imraan: 169-170]
Aayah kama hizi za kuadhibishwa makafiri pale wanapotolewa roho zao na baada yake, pamoja na neema wanazopata Waislamu wanapotolewa roho zao na baada yake pamoja na Adhabu wanayopata Fir’awn na watu wake ni nyingi sana, jambo linalotufanya tusiweze kukanusha juu ya adhabu ya kaburini zilizotajwa wazi wazi na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth zake nyingi Swahiyh.