Swawm (Funga) Ya Jumamosi Inapoangukia Siku Ya 'Arafah Au 'Aashuraa Inafaa?
Swawm (Funga) Ya Jumamosi Inapoangukia Siku Ya 'Arafah Au 'Aashuraa Inafaa?
Swali La Kwanza:
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatu.
Shukran kwa kazi zenu munazofanya kuelimisha umma.
Tumeelezewa kwamba haifai mtu kufunga saum ya sita katika siku ya jumamosi, je hii ni sawa. Je ikiwa nafunga saum ya 13, 14 & 15 ikiangukia jumamosi nifunge au vipi? Shukran
Swali La Pili:
Eti kufungua Jumamosi haifai hata ikiwa ni siku ya Arafa au Ashoora?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Tunawashukuru ndugu zetu waliouliza maswali hayo ambayo kwa nyakati za karibuni limeleta utata sana baina ya Wenye elimu, Wanafunzi na pia Waislamu wa kawaida.
Utata huu umesababishwa na kufahamika Hadiyth hii kuwa ni ya makatazo katu, nayo inasema:
Kutoka kwa 'Abdullaah bin Busr kutoka kwa kaka yake kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Msifunge (Swawm) siku ya Jumamosi isipokuwa ikiwa mmefaridhiwa na Allaah kwenu. Ikiwa mtu hakupata chochote cha kula isipokuwa ganda la zabibu au gome la mti, basi alitafune)) [At-Tirmidhiy, Abuu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ibn Maajah, Ahmad na Al-Haakim] Al-Haakim anasema kuwa hii ni Hadiyth Sahihi kulingana na sharti za Muslim na At-Tirmidhiy akasema ni Hasan]
Wanaopinga kufunga Jumamosi wanategemea Hadiyth hiyo.
Hata hivyo, Abuu Daawuwd anasema Hadiyth hiyo imefutwa na Hadiyth ya Juwayriyyah. Hadiyth ya Mama wa Waumini Juwayriyyah inasema:
Juwayriyah bint Al-Haarith, Mama wa Waumini (Radhwiya Allaahu 'anha) anatuhadithia: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinitembelea Ijumaa siku ambayo ilikuwa nimefunga (swawm), akaniuliza: “Je, ulifunga jana?” Nikasema: “Hapana.” Akauliza tena: “Je, una niyyah ya kufunga kesho?” Nikasema: “Hapana.” Akasema: “Basi fungua.”
Katika Riwaayah nyingine: “Alimuamuru afungue, naye akafungua.” [Al-Bukhaariy, Abuu Daawuwd, Hadiyth sahihi]
Wale wanaosema kuwa inawezekana kufunga siku hiyo wanategemea Hadiyth zifuatazo. Miongoni mwazo ni: Abu Dharr (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru Swawm siku tatu katika kila mwezi – yaani masiku meupe, ambapo mwezi unakuwa umekamilika (tarehe 13, 14, na 15 katika miezi ya Kiislamu). Na akasema kufanya hivyo ni sawa na Swawm za milele” [An-Nasaaiy na Ibn Hibbaan, ambaye amesema ni Sahihi].
‘Ulamaa wanasema kuwa hii ni kauli ya kijumla katika Swawm siku hiyo na huenda Jumamosi ikaangukia moja ya terehe hizo. Na pia ipo Hadiyth ambayo inatupigia mfano wa Swawm ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika suala hilo. Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anafunga (Swawm) siku ya Jumamosi, Jumapili na Jumatatu katika mwezi mmoja na Jumanne, Jumatano na Alkhamiys katika mwezi mwengine.” [At-Tirmidhiy].
Amesema ‘Abdullaah bin ‘Amr bin Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: “Swawm inayopendeza zaidi kwa Allaah ni Swawm ya Nabiy Daawuwd … alikuwa anafunga siku moja na anakula siku moja” [Al-Bukhaariy, Muslim na An-Nasaaiy].
Hii ni Hadiyth ndefu ambayo inapatikana katika Riyaadhwus Swaalihiyn cha Imaam An-Nawawiy, Hadiyth Namba 150.
Jambo ambalo linaweza kupatikana katika kufuata Sunnah hii ya Swawm ambayo ni bora kabisa ni lazima baada ya kila wiki mbili utakuwa ni mwenye kufunga siku ya Jumamosi. Na ikiwa aina hii ya Swawm imeitwa ndiyo Swawm bora na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tutaweza kuitekeleza namna gani?
Juwayriyah bint Al-Haarith, Mama wa Waumini (Radhwiya Allaahu 'anha) anatuhadithia: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinitembelea Ijumaa siku ambayo ilikuwa nimefunga (Swawm), akaniuliza: “Je, ulifunga jana”. Nikasema: “Hapana”. Akauliza tena: “Je, una nia ya kufunga kesho?” Nikasema: “Hapana”. Akasema: “Basi fungua”. Katika Riwaayah nyingine: “Alimuamuru afungue, naye akafungua” [Al-Bukhaariy na Abuu Daawuwd].
Na katika Hadiyth ya Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Usifunge siku ya Ijumaa mpaka uwe umefunga siku kabla yake au siku inayofuata” [Al-Bukhaariy na Muslim].
Kwa hiyo hapa inaonyesha kuwa siku inayofuata baada ya Ijumaa ni Jumamosi.
Imepokewa kwa Abuu Qataadah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Swawm ya siku ya ‘Arafah inafuta madhambi ya miaka miwili; iliyopita na ijayo. Na Swawm ya siku ya ‘Aashuraa inafuta madhambi ya mwaka uliopita” [Jamaa‘ah isipokuwa na Al-Bukhaariy na At-Tirmidhiy].
Wale wenye rai ya kuwa unaweza kufunga Jumamosi wanasema kuwa hii ni kauli ya kijumla kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kufunga siku ya ‘Arafah na ‘Aashuraa siku yoyote itakayokuwa ikiwa ni Jumamosi, Jumapili au siku nyingine yoyote. Na ikiwa hutafunga basi utakuwa umekosa fadhila kubwa sana.
Kwa kukhitimisha, ‘Ulamaa wengi wanaonelea hakuna ubaya wala makatazo ya kufunga (Swawm) Jumamosi ikiwa mtu atafunga siku ya kabla yake au baada yake.
Na kuna ‘Ulamaa wanaoona kuwa Hadiyth ya makatazo ya kufunga Jumamosi ina kasoro. Al-Lajnatu Ad-Daaimah katika fatwa namba 11747, walipomjibu muulizaji aliyeuliza kuhusu kufunga 'Arafah ikiangukia Jumamosi, wanasema kuwa Hadiyth ya makatazo ya kufunga Jumamosi ni dhaifu na inapingana na Ahadiyth nyingi sahihi zenye mnasaba huo.
Kadhalika Imaam Ibn Baaz naye amesema Hadiyth hiyo ni dhaifu na inapingana na Ahaadiyth sahihi.
Na Allaah Anajua zaidi