Familia Katika Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Familia Katika Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Alhidaaya.com

 

 

Shukrani zote ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)

 

Ni katika baraka zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa Muislamu Kumuwezesha kufunga mwezi wa Ramadhawaan na kuutumia wakati wake wa usiku kwa Swalah. Ni mwezi ambao ndani yake amali njema huzidishwa malipo na watu hupandishwa daraja (vyeo). Ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Huwaachia huru baadhi ya watu kutokana na Moto. Kwa hivyo Muislamu ni lazima ajitahidi sana kufanya mambo mema katika mwezi huu; ni lazima afanye hima katika kuutumia wakati wa uhai wake wenye ibada. Kuna watu wangapi ambao wamenyimika katika mwezi huu kutokana na maradhi, mauti au kukosa maelekezo mema.

 

Muislamu ni lazima ajitahidi sana (kufanya matendo mema) katika wakati wake wote ndani ya mwezi huu; anayo majukumu yasiyoweza kuepukika juu ya watoto wake, kuwalea  vizuri na kuwatunza vyema,  kuwahimiza kufanya kila aina ya vitendo vyema na kuwafanya waendelee kukuwa navyo – kwa sababu  mtoto hukulia katika mwenendo ambao wazazi wake wamemzoeza.

  

Katika wakati wa siku hizi zilizobarikiwa, baba na mama wana nafasi adhimu ya kufanya yenye manufaa, na tunaweza kutoa ushauri ufuatao kwa wazazi:

 

 

1 - Kuzifuatilia Swawm za watoto wao na kuwapa moyo wale wanaoshindwa kufanikisha.

 

 

2 - Kuwahimiza kuhusu Swawm halisi inavyotakiwa, na sio tu kujizuilia kula na kunywa, lakini ni njia ya kufikia kwenye Kumcha Allaah (Taqwa), na hiyo ni nafasi maalumu ya kusamehewa madhambi na kulipwa malipo mema.

 

Imesimuliwa kutokana na Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alishuka kutoka juu ya minbar na akasema: “Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn.” Akaulizwa, “Ee Rasuli wa Allaah, kwa nini umefanya hivyo?” Akasema, “Jibriil alinambia, ‘amekula khasara yule ambaye Ramadhwaan imemfikia na akawa hakusamehewa dhambi zake, na nikasema, ‘Aamiyn’. Baadaye akasema, ‘amekula khasara yule ambaye ameishi na hali ya kuwa amewaona wazazi wake mpaka wakawa vizee, mmoja wao au wote wawili, lakini ikawa hajaingia peponi,’ na nikasema, ‘Aamiyn’. Baadaye akasema, ‘amekula khasara yule ambaye wakati unapotajwa ikawa yupo na asikutakie Rehma juu yako,’ na nikasema, ‘Aamiyn’.”

 

Imepokelewa na Ibn Khuzaymah, 1888; at-Tirmidhiy, 3545; Ahmad, 7444; Ibn Hibbaan, 908. Angalia Sahiih al-Jaami’, 3501.

 

 

3 – Wafundishe (watoto) adabu nzuri na namna ya kula, kwa mfano kula kwa kutumia mkono wa kulia na kunywa kwa  kutumia mkono wa kulia na kuchukua chakula kutoka mbele ya nafasi zao (wasichukue upande wa mwengine); wakumbushe kwamba kufanya israfu  katika  chakula ni Haraamu na ni madhara kwa mwili.

 

 

4 – Usiwaachie kutumia wakati mrefu katika kula futari ikafikia hadi wakakosa Swalah ya jamaa ya Maghribi.

 

 

5 – Wakumbushe kuhusu hali za masikini na mafaqiri ambao hawawezi kumudu hata tonge ya chakula angalau wakaondosha moto wa njaa yao; Wakumbushe hali za wale wote ambao aidha huhama au hupigania Jihadi kwa ajili ya kutaka ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika sehemu zote.

 

 

6 – Mikusanyiko hii (ya mwezi wa Ramadhwaan) inatoa nafasi nzuri ya kuwajumuisha jamaa pamoja na kuthibitisha mshikamano wa koo.  Mazoea kama haya yapo katika baadhi ya nchi, na vile vile ni nafasi nzuri ya kupatanisha na kutengeneza uhusiano uliovunjika baina ya jamaa.

 

 

7 – Inamsaidia mama (kupata nafasi nzuri ya) kutayarisha chakula, kusafisha na vilevile kukiweka chakula muweko unaostahiki.

 

 

8 –Wawahimize watoto kuswali Swalah ya Taraawiyh na kujiandaa kwa ajili ya hiyo Swalah kwa kutokula sana na kujiweka tayari kwa wakati ili kwenda msikitini.

 

 

9 – Kwa kuzingatia Daku, wazazi ni lazima wawafundishe watoto baraka za daku na kwamba daku humpa mtu nguvu ya kufunga.

 

 

10 – Waruhusu kuwa na wakati wa kutosha kabla ya Swalah ya Alfajir ili kwa wale ambao hawakuswali Swalah ya Witri waweze kufanya hivyo kwenye wakati ule,  na vile vile kwa wale wanaochelewesha Swalah zao hadi wakati wa mwisho wa usiku, waweze kusali na pia kila mmoja aweze kuomba du’aa kwa Allaah vyovyote vile mtu apendavyo.

 

 

11 – Pawepo mazingatio ya kwenda msikitini kwa ajili ya Swalah ya jamaa ya Alfajir, kwa wale wanaowajibika kufanya hivyo. Tunaona watu wengine ambao huamka katika mwisho wa usiku kwa ajili ya kula daku, huwa wanarejea tena kulala na kupuuza (kupitwa) na Swalah ya Afajir.

 

 

12 – Ilikuwa ni kawaida ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhwaan kukesha usiku na kuwaamsha watu wake. Hii inamaanisha kwamba familia ni lazima izingatie   kufanya jitihada kwenye wakati huu adhimu (wenye baraka) ili kufanya matendo ambayo yanamridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), huenda mtu Akatukuzwa na Kupandishwa daraja (za Amali zake njema). Kwa hivyo Mume ni lazima awaamshe Mkewe na Watoto wake ili kuyafanya yale ambayo yatawapelekea kuwa karibu na Rabb Wetu (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

 

13 – Hutokezeya wakati mwengine ikawa kuna watoto wadogo katika nyumba ambao wanahitaji kupewa moyo ili waweze kufunga, kwa hivyo baba ni lazima awahimize kuamka kwa ajili ya kula daku, na vile vile awape moyo kwa kuwasifu na kuwatunukia pindi wakimaliza mwezi mzima au hata wakifikisha nusu yake,  na vinginevyo (robo ya mwezi au wiki moja).

 

 

Imesimuliwa kwamba Ar-Rubayyi’ bint Mu’awwidh alisema: Ilikuwa asubuhi ya mwezi wa ‘Ashuraa’ Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipeleka habari kwenye  vijiji vya Answaar akasema“ Yeyote aliyeamka bila ya kufunga, basi na asile kwa  muda wote uliobakia kwa siku ile, na yeyote aliyeanza kufunga basi na aendelee na Swawm yake.” Akasema (bibi huyu): Tulikuwa tukifunga na kuwafungisha watoto wetu, [na tulikuwa tukiwachukua msikitini] na tukiwatengenezea vitu vya kuchezea vya sufi, ili ikiwa mmoja wao atalilia chakula basi humpa kile kitu cha kuchezea (ili kimliwaze) mpaka ufike wakati wa kuftari.

 

Imepokelewa na [al-Bukhaariy, 1859; Muslim, 1136] – Maneno ya kwenye mabano yamepokelewa na [Muslim].

 

 

An–Nawawiy amesema:

 

Hadiyth hii inaonyesha kwamba ni lazima tuwafunze watoto wetu juu ya kufanya matendo ya ibada na tuwaendeleze ili wakulie nayo, ijapokuwa wao hawahesabiwi (kwa ajili ya umri wao kuwa mdogo). Al-Qaadhi amesema: Imesimuliwa kutokana na ‘Urwah kwamba pale wanapokuwa wao wanaweza kufunga basi huwa ni lazima juu yao kufunga. Hili ni kosa ambalo halina uthibitisho wa hadiyth sahihi, “Kalamu huondoshwa kutokana na (mambo) matatu: kutoka mtoto anapozaliwa mpaka afikiapo kuwa msichana/mvulana …….” Na Allaah ni Mjuzi Zaidi. [Sharh Muslim, 8/14]

 

 

14 – Ikiwa inawezekana, baba na mama ni lazima wende na watoto wao kwenye ‘Umrah (Hijja ndogo) wakati wa Ramadhwaan, na kufanya hivyo ni manufaa juu yao na katika maisha ya baadae, kwa nafsi zao wenyewe wazazi na familia yao pia. Ibada ya Umrah katika mwezi wa Ramadhwaan ina ujira sawa na Hijja. Ni bora kwenda kufanya ‘Umrah katika wakati wa mwanzo wa mwezi wa Ramadhwaan ili kuepuka misongamano ya watu.

 

 

15 – Mume asimbebeshe kazi nyingi kupita uwezo wake mkewe kwa kupika vyakula vingi. Watu wengi huuchukulia mwezi wa Ramadhwaan kuwa ni mwezi wa kubuni vyakula na vinywaji (vya kila aina) na huwa wanazama zaidi kwenye hayo. Hii inapunguza thamani ya uzuri wa mwezi huu na inakwenda kinyume na madhumuni ya kufunga, ambapo ni kufikia Uuchwaji wa Allaah (Taqwa).

 

 

16 – Mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi wa Qur-aan, kwa hivyo tunashauri kila familia iwe inajikusanya pamoja kwa ajili ya kusoma Qur-aan.  Baba aifundishe familia yake namna ya kusoma na maana ya aayah za Qur-aan.  Katika mkusanyiko huo huo kuwe kunafundishwa (aidha kwa njia ya usomaji wa vitabu juu ya) adabu za kufunga.  Katika mwezi wa Ramadhwaan Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Huwawezesha wengi katika wanavyuoni na watafutao elimu  kuandika vitabu ambavyo hutumika kwa ajili ya mihadhara na kufundishia; vitabu hivyo hugaiwa katika sehemu thelathini ambapo kila sehemu huwa na mada  isomwayo kwa siku moja na huleta manufaa kwa kila mtu.

 

 

17 – Ni lazima wahimizwe kuutumia wakati wao kuwapitia majirani na wenye shida (kuhitaji).

Imesimuliwa kwamba Ibn  ‘Abbaas Amesema:  Rasuli  wa  Allaah ( Rehma na Amani Zimshukie Juu Yake) alikuwa ni Mkarimu sana kwa watu, na alikuwa katika kiwango kikubwa zaidi cha ukarimu wakati wa mwezi wa Ramadhwaan. Wakati Malaika Jibriyl alipomjia. Alikuwa akimjia kila usiku akimzoeza Qur-aan pamoja naye. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa Mkarimu sana kuliko hata mvumo wa upepo. [ Imepokewa na al-Bukhaariy, 6; Muslim, 2308].

 

 

18 – Wazazi ni lazima wazikinge familia zao na watoto wao kutokana na kukaa muda mrefu wakati wa usiku na kuupoteza muda katika matendo yasiyokuwa na manufaa, vitu vya kumpumbaza mtu ni haramu? Waovu miongoni mwa watu katika mwezi wa Ramadhwaan huwa zaidi ni kishawishi kikubwa katika kuchochea waliofunga ili wafanye vitendo vibaya na viovu, usiku na mchana.

 

 

19– Ni lazima wakumbuke Mkutano wa Familia katika Jannah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika maisha ya Aakhirah, ni furaha kubwa kukutana huko wakiwa kwenye kivuli cha Ufalme Wake (Allaah). Mikusanyiko hii ya Baraka katika ulimwengu huu inaletwa kutokana na kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kufunga na Kuswali ni njia moja wapo inayopelekea kupatikana furaha.

 

 

 

Share