07-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: 'Umar Bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu 'Anhu) - 2
Matendo ya Ibada
‘Umar aliyasabilia maisha yake yote kwa Allaah. Kauli yake na kukaa kimya kwake vilitawaliwa na utashi wa Allaah. Furaha na ghadhabu yake ikiwa ni pamoja na kuchukia kwake rushwa, ilikuwa imepunguzwa ukali chini ya mwongozo wa Uislamu, na hakuwa mkali na katili kwa yoyote. Dhamira yake za amali zake zilielekezwa kupata radhi ya Allaah, Muumba Wake. ‘Umar alifikia daraja hii ya wema kutokana na subira na uthibiti katika uchaji Mungu.
Sa’iyd bin Al-Musayyib alisema:
“‘Umar alipendelea kuswali usiku wa manane.”[1].
“‘Umar akipenda kufanya amali zilizomkurubisha na Allaah”, Anas alisimulia.
Mjumbe wa Allaah aliwauliza Maswahaba zake: “Nani anatarajia kufunga leo?” ‘Umar alijibu, “Mimi.” Mjumbe wa Allaah alisema: “Nani aliyesindikiza jeneza leo?” ‘Umar alijibu: “Mimi.”Alisema: “Pepo ni yako.”[2]
Hadithi hii inatajwa katika uadilifu wa Abu Bakr
Tabia Yake
Isipokuwa ‘Umar alikuwa na uhusiaho mzuri na Mtume kwa kuwa Mtume alimwoa binti yake Hafswah, na zaidi ya hayo alikuwa mtu wa ukoo mtukufu, na alikuwa Jemadari wa Waumini hakuwa na kiburi. Kinyume chake, ‘Umar alikuwa na staha. ‘Abdullaah bin ‘Abbaas alisimulia kisa kinachoonesha kuwa alikuwa hivyo na alisema”
Al-‘Abbaas alikuwa na mchirizi nyumbani kwake. Siku moja Al-‘Abbaas alichinja kuku wawili. Ilikuwa siku ya Ijumaa na ‘Umar alivaa kanzu mpya na alielekea Msikitini. Wakati akiwa njiani kuelekea Msikitini, maji yaliyochanganyika na damu ya kuku wale kutoka katika mchirizi yalichafua kanzu ya ‘Umar .
‘Umar aliamuru mchirizi ule ufukiwe. Kisha alirejea nyumbani kwake kubadilisha nguo na akawaswalisha watu.
Al-‘Abbaas alimwendea na kumwambia: “WaLlaahi, ulikuwepo alipouweka Mtume” ‘Umar alimwambia Al-‘Abbaas: “Nakutaka upande mgongoni mwangu mpaka mchirizi utakaporejeshwa pahala alipouweka Mjumbe wa Allaah” Kwa hiyo Al-’Abbaas alifanya hivyo.[3]
Hadiyth hii inaonesha kuwa alikuwa mwenye staha, na hakuwa mkorofi wala fedhuli. Inadhihirisha mapenzi ya dhati na kumheshimu Mtume.
Kuna Hadiyth nyingine inayoonesha tabia yake ya kati na kati. Alipokwenda Syria, askari walikutana naye amevaa kikoi, makobadhi na kilemba. Alipofika kwenye ardhi yenye maji maji, alishuka, na akashika makobadhi mkononi na akashika kichwa cha mnyama wake na kuvuka maji. Aliambiwa, “Ewe Jemadari wa Waumini! Inafaa kwa askari wa makasisi wa Syria kukutana nawe katika hali hiyo?” Alijibu:
“Kwa uhakika Allaah Ametutukuza kwa Uislamu. Kwa hiyo hatutatafuta utukufu kutoka sehemu nyingine.”[4]
Dalili nyingine ya unyofu wake ni pale alipokuja kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib na alimwambia:
“Kwa nini hukutuma mtu aniite?”
‘Umar alijibu:
“Nawajibika zaidi kuja kwako.”
Siku moja, alipokuwa Khalifa alikuwa akibeba kiriba cha maji, aliulizwa:
“Moyo wangu unakuwa ukinishawishi, hivyo nataka kuuadibisha.”[5]
Kujinyima Anasa
‘Umar alijulikana kwa bidii yake kwenye Dini. Twalhah bin ‘Ubaydullaah alisema:
“‘Umar hakututangulia kuingia katika Uislamu au katika kuhajiri, lakini alikuwa ameyapa nyongo maisha ya dunia, na alipenda maisha ya Akhera zaidi. Siku moja, Hafswah bintiye alimwambia:
“Ewe Jemadari wa Waumini.”Hapana madhara endapo utavaa nguo nzuri kuliko hizi na kula mlo kamili, kwa sababu Allaah Amekujaalia vya kutosha na zaidi.”
Alimwambia:
“Hukumbuki ya kuwa Mjumbe wa Allaah na Abu Bakr walivyokuwa wakiteseka?” Alianza kuwataja mpaka alipolia. Kisha alisema:
“WaLlaahi, nitashirikiana nao maisha magumu waliyokabiliana nayo mpaka nitakapoungana nao katika daraja za juu (bora).
Abu ‘Uthmaan alisema:
“Nilimwona ‘Umar akitupa Jamrah ilhali amevaa Izaar (kikoi) yenye kiraka.”[6]
Anas alisema:
“Niliona viraka vinne katika shati la ‘Umar.”
‘Abdullaah bin ‘Aamir alisema:
“Tulitoka kwenda Hija na ‘Umar bin Al-Khattwaab, hatukusimika hema mpaka tuliporejea. Tulipotaka kupumzika, tulitandika mkeka, na tulitandaza shuka kwa ajili ya kivuli chini ya mti.”[7]
Kuwajali Raia Zake
‘Umar alikuwa akijishughulisha sana na mambo ya raia zake. Alikuwa akiwakagua, aliwasaidia na akitatua matatizo yao. Mara nyingi akijichosha kwa kuwafikiria wengine. Kichocheo cha nguvu zake kilikuwa kwa ajili ya Akhera, na alisema:
“Iwapo nitalala mchana, raia zangu wanaweza kudhuriwa, na iwapo nitalala usiku naweza kukasirika.”
Siku moja, ‘Umar alikwenda sokoni na kijana wa kike alimfuata na kumwambia:
“Ewe Kamanda wa waumini! Mume wangu amefariki, na nina watoto wadogo. Nachelea waonaje wakapotea. Mimi ni binti ya Khifaf bin Ayman Al-Ghifaariy ambaye alikuwa pamoja na Mjumbe wa Allaah katika Al-Hudaybiyah.
Alimwambia:
“Karibu ndugu!”
Alipakia kwenye ngamia magunia makubwa mawili ya chakula na nguo. Alimpa yule mwanamke na kumwambia:
“Chukua, na Allaah Atakupa kingine kabla ya kumalizika hiki.”
Mwanaume aliyeshuhudia hilo alimwambia:
“Umempa kingi ewe Kamanda wa Waumini!” Alijibu:
“Nataraji uondokewe na mama yako. Namkumbuka baba yake na binamu yake walipokuwa wakiizingira ngome kwa muda mrefu mpaka Allaah Alipowapa ushindi, na tukachukua ngawira zake.
Siku moja kikundi cha wafanya biashara kilifika msikitini, ‘Umar alimwambia ‘Abdur-Rahmaan “uwalinde usiku wa leo.”
Waliwalinda usiku kucha huku wakimwomba Allaah awaruzuku. Usiku ule alisikia mtoto akilia na akafuatilia ile sauti ya kilio cha mtoto, alimkuta na mama yake. Alimwambia:
“Muogope Allaah, na umtendee wema mwanao.” Kisha alirejea
mahala pake. Kabla ya kuingia alfajiri, alimsikia tena yule mtoto akilia, na akaenda kumwangalia:
“Je, mama si mama mwema? Huyu mtoto ana matatizo gani?”
Mama alijibu”
“Ewe mtumwa wa Allaah! Namlazimisha aache kunyonya lakini hataki.”
Akamwuliza sababu ya kufanya vile. Alisema, kwa sababu ‘Umar hatengi posho ila kwa walioacha ziwa.”
Alimwuliza:
“Mtoto ana umri gani?” Alijibu: “Miezi kadhaa.”
Alimwambia:
“Mapenzi yakafike. Usimwachishe kunyonya kwa lazima.” Aliswali Subhi, watu hawakuelewa kisomo chake wakati akiswali Subhi kutokana na kulia sana. Alipotoa At-Tasliym alisema:
“Ni jinsi gani ‘Umar anafadhaishwa! Ni watoto wangapi wameteseka au kufariki dunia?”
Kisha alimtaka mpiga mbiu atangaze kuwa ni marufuku kwa wanawake kuwaachisha ziwa watoto wao mapema. Akaamuru ya kuwa posho ilipwe kwa kila mtoto anayezaliwa, na akapeleka nakala ya shar’ah hiyo sehemu zote za dola.[8]
‘Usiku mmoja alipokuwa akivinjari, alisikia sauti za watoto waliokuwa wakilia, ‘Umar alijongelea nyumba ile na kusema:
“Ewe mjakazi wa Allaah! Watoto hawa wana shida gani?”
Alijibu: “Wanalia kwa kuwa wana njaa.” ‘Alisema: “Je vipi chungu kilichopo jikoni?”
Alijibu: “Ni chungu chenye maji ili watoto wadhani kuwa kimejaa samli, unga na tende. Nafanya hivi mpaka walale.”
‘‘Umar alikaa na kulia. Alikwenda kwenye ghala la chakula na akachukua gunia lenye unga, samli, tende, nguo na fedha na kulijaza pomoni.
Alimwambia Aslam (Mtunza ghala) ‘Nibebeshe mgongoni’ Aslam alijibu: “Hapana nitalibeba badala yako, Ewe Jemadari wa Waumini!” (‘Umar) Alimwambia, “Yaani mama yako akukose Ninawajibika kwao Siku ya Qiyaamah.” Alibeba lile gunia na kulipeleka kwa yule mama. Alichanganya samli, tende na unga kisha akaanza kupika na baada ya kuiva aliwapakulia ili wale. Hakuondoka mpaka alipowaona watoto wakila na kucheza.
Alimwambia Askari:
“Unajua kwa nini sikuondoka mpaka walipokula?” Alijibu,”Hapana, Ewe Jemadari wa Waumini!” Alimwambia: “Nilipowaona wanalia, nilichukia sana na sikutaka kuondoka mpaka nipate utulivu.
Kubashiriwa Pepo
Kuna Hadiyth nyingi zinazombashiria Pepo.
Ibn ‘Umar alisimulia, Mtume alimwona ‘Umar amevaa kanzu nyeupe na akamwambia”:
“Ni mpya au imefuliwa?”
Ibn ‘Umar alisema:
“Sikusikia jibu la ‘Umar.”
Mtume alimwambia:
“Vaa nguo mpya, ishi kwa furaha na kufa ukiwa shahidi. Nakuombea Allaah Akupe utulivu wa macho hapa duniani na kesho Akhera.”
‘Umar alisema:
“Na wewe pia, Ewe Mjumbe wa Allaah”
Abu Muusa alisimulia:
Siku moja, nilikuwa pamoja na Mtume katika bustani ya Al-Madiynah, mtu mmoja alipobisha hodi. Mtume alisema:
“Mfungulie mlango na mpe bishara za Peponi.” Kwa hiyo nilimfungilia, kumbe alikuwa Abu Bakr, hivyo nikampa bishara za Peponi.
Mtu mwingine alikuja na kuomba ruhusa ya kuingia.
Mjumbe wa Allaah Alisema.
“Mfungulie mlango na mpe habari za kufurahisha za Peponi.”
Alikuwa ‘‘Umar. Nilimfungulia na nikampa habari njema za Peponi.
Kisha mtu wa tatu alikuja na kuomba rukhsa ya kuingia Mjumbe wa Allaah alikuwa ameegemea, alikaa amenyooka na alisema:
“Mfungulie mlango na mweleze mazuri ya Peponi kwa wema wake na mateso yatakayomfika.”
Alikuwa ‘‘Uthmaan na nilimfungulia mlango na nikambashiria Pepo, na nikamweleza aliyoyasema Mjumbe wa Allaah.
’Uthmaan alisema:
“Msaada unatakiwa kuombwa kwa Allaah Pekee.” (Al-Bukhaariy).
Katika masimulizi mengine Anas alisema, Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan walipanda mlima wa Uhud. Mlima ulipotetemeka Mjumbe wa Allaah alisema:
“Tulia, Uhud, kwa sababu kuna Mtume, mkweli mmoja na mashahidi wawili juu yako.” (Al-Bukhaariy).
Mu’adh bin Jabal alisimulia:
Kwa uhakika ‘Umar ni mmoja wa wakazi wa Mtume na aliwaelezea aliona nini kwenye ndoto zake, na wakati mwingine alipokuwa macho. Mjumbe wa Allaah alisema:
“Nilipokuwa Peponi niliona Qasri na niliuliza: “Ni la nani hili?” Nilijibiwa: ‘Ni kwa ajili ya ‘Umar bin Al-Khattwaab.”[9]
Baadhi ya Hadiyth za Mtume Kuhusiana Naye
Mtume alisema:
“Miongoni mwa ummah kabla yenu walikuwepo Muhaddathun (watu walipata ufunuo, japokuwa hawakuwa miongoni mwa Mitume. Na kama yupo mtu wa aina hiyo miongoni mwa wafuasi (ummah) wangu, ni ‘Umar.”[10]
Anas alisimulia ya kuwa Mtume alimzungumzia Abu Bakr na ‘Umar .
“Hawa ndio mabwana wa watu wa Peponi miongoni mwa watu wa mwanzo na wa mwisho isipokuwa Mitume na Manabii (At-Tirmidhi).
Mtume alisema:
“Kuna mtu anayechukia uongo. Huyo ni ‘Umar bin Al-Khattwaab Mtume pia alisema:
Bila shaka, Allaah Aliwapa malaika watu wa ‘Arafah kwa ujumla, na akampa ‘Umar pekee.”
Aidha Mtume alisema:
“Hamtapata mateso endapo mtu huyu atakuwa miongoni mwenu (akimkusudia ‘Umar) ”[11]
Mtume alimwambia ‘Umar
“Naapa kwa Yule Ambaye roho yangu iko Mikononi Mwake, Shaytwaan akuonapo njiani, yeye huchukua njia nyingine tofauti na yako.”[12]
Mtume alisema:
“Aliyekuwa na shauku ya juu kwa Dini ya Allaah ni ‘Umar.”[13]
Mtume alisema:
“Kwa uhakika, Allaah Ameandika ukweli katika ulimi wa moyo wa ‘Umar.”
Baadhi ya kauli za Maswahaba kumhusu ‘Umar
Abu Bakr alisema:
“Hapana mtu kwenye uso wa dunia ninayempenda zaidi ya ‘Umar.”
Ibn ‘Umar alisema”
“Sijapata kumwona yeyote mighairi ya Mjumbe wa Allaah aliye mkali na mkarimu kuliko ‘Umar.”
Ibn Mas’uud alisema:
“Watu wema wanapotajwa, na ‘Umar hutajwa. Alikuwa na maarifa mengi juu ya Kitabu cha Allaah na Dini ya Allaah.”
Hudhayfah alisema:
“Sikumjua mtu aliyeogopa lawama za Allaah zaidi ya ‘Umar.”
Kufa Kwake Shahidi
‘Umar bin Al-Khattwaab aliuawa na Abu Lu-u lu-u ambaye alikuwa mtumwa wa Al-Mughiyrah bin Sh’bah alikuwa mateka wa vita.
Alikwenda kwa ‘Umar kulalamikia juu ya kodi kubwa hivyo, alimwambia: “Unacholipa si kikubwa.”
Aliondoka na ‘Umar Kisha alichukua jambia lenye ncha tatu na kulificha mpaka alfajiri ambapo ‘Umar angeamsha watu kwa ajili ya Swalah ya Subhi, na alimchoma mara tatu. Pigo moja lilikuwa chini ya kitovu ndilo lilosababisha kifo. Kisha aliwachoma watu kumi na mmoja baada ya ‘Umar kisha alijiua.
‘‘Uthmaan bin ‘Affaan alisema: “Nilikuwa mtu wa mwisho kusema na ‘Umar akiwa hai, nilimwona alipokuwa akiweka kichwa chake kwenye paja la mwanae, ‘Abdullaah, huku akimwambia, “Acha shavu langu liwe juu ya ardhi, na ‘Abdullaah alisema: Mapaja yangu na ardhi yote ni sawa.” Alimwambia: Liache shavu langu liwe juu ya ardhi. Mama yako awe mkiwa” Kisha nikamsikia akisema: “Ole wangu, na ole wenu yangu ikiwa Allaah hatonisamehe; mpaka roho yake ilipotolewa.”
‘Umar alimtuma mtoto wake, ‘Abdullaah kwa ‘Aaishah kumwomba idhini ya kumzika pembeni mwa Mtume na Abu Bakr. Alitoa rukhusa na alizikwa pembeni ya rafiki zake wawili akiwa na umri wa miaka 63. Alikuwa Khalifa wa miaka kumi, miezi minne na siku kadhaa.
[1] Swifatus –Safwah.
[2] Ar-Riyaadh An-Nadirah 2/364.
[3] Swifatus-Safwah 2/128
[4] Swifatus-Safwa, 2/380.
[5] Siyar A’laam An-Nubalaa.
[6] Usdul-Ghaabah
[7] Swifatus -Safwah 1/126.
[8] Swifatus –Safwah 1/126.
[9] Majma’ Az-ZawAaid 9/1446
[10] Al -Bukhaariy
[11] Ar-Riyadh An-Naadirah.
[12] Al-Bukhaariy