08-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: 'Uthmaan Bin 'Affaan (Radhiya Allaahu 'Anhu) - 1
‘Uthmaan Bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Ambaye Alibashiriwa Pepo
Jina Lake Na Ukoo Wake
Jina lake ni ‘Uthmaan bin ‘Affaan bin Abul-‘Aas bin Umayyah bin ‘Abdus Shams, alikuwa Mquraysh wa Bani Umayyah. Ukoo wake na ule wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) unakutana kwa ‘Abdu Manaaf
Alizaliwa katika mji wa Twaaif miaka sita baada ya mwaka wa Ndovu, sawa na 576 M Mama yake aliitwa Arwaa bint Kuraya bin Habiyb bin Abdus Shams, na bibi yake alikuwa Al-Baydha bint ‘Abdil-Muttwalib bin Haashim, shangazi wa Mjumbe wa Allaah.
Ukoo Wake
‘Uthmaan alipewa lakabu ya Abu ‘Abdillaah (Baba ‘Abdullaah) na Abu ‘Amr. ‘Abdullaah alikuwa mtoto kwa Ruqayyah bintiye Mjumbe wa Allaah. ‘Abdullaah alifariki dunia alipokuwa na umri wa miaka sita yaani, mwaka wa nne wa Hijriyyah.
Aidha ‘Uthmaan alipewa lakabu ya Dhun-Nurayn (mwenye nuru mbili) kwa sababu aliwaoa Ruqayyah na Umm Kulthuum mabinti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa mtu pekee aliyeoa mabinti wawili wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Maumbile Yake
‘Uthmaan hakuwa mrefu wala mfupi, alikuwa mzuri wa sura na nywele rangi ya njano na ndevu nzito. Alikuwa na mifupa mikubwa na mabega mapana.
Alifahamika kwa ndevu zake za rangi ya njano, alikuwa na nywele nyingi na nywele nyuma ya masikio yake.
‘Abdullaah bin Hazm alisema:
“Nilimwona ‘Uthmaan. Sijawahi kumwona mwanaume au mwanamke mwenye sura nzuri kama yake.”[1]
Kurejea Katika Uislamu
Si jambo la kushangaza kuwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kurejea katika Uislamu. Alikuwa amemiliki kufanya vizuri, na kwa maumbile yake hakupenda jambo lililokusudiwa kushusha heshima ya mtu.
Alifahamika kwa hayaa zake, na alikuwa na sifa nzuri hata kabla ya kusilimu. Kila mara akihudhuria mikutano ya watu wa hadhi yake. Mara nyingi alikuwa akipatikana nyumbani kwa Abu Bakr As-Swiddiyq, pahala walipokuwa wakikutana watukufu wa Kiquraysh.
Abu Bakr alikuwa rafiki kwa watu wake kutokana na kujiweka na watu wa kawaida na utu wake. Alikuwa mtu mtukufu miongoni mwa Maquraysh, na alikuwa anajua miamala mibovu ya watu wake. Waheshimiwa na Kiquraysh wakienda kwake kwa haja mbali mbali. Alikuwa na ujuzi na mweledi wa mambo mengi, na alikuwa na lugha ya umbuji iliyowafanya watu wengi wamwamini. Abu Bakr aliwaalika katika Uislamu watu waminifu. ‘Uthmaan bin ‘Affaan alikuwa miongoni mwa wale walioalikwa na Abu Bakr kurejea katika Uislamu. Alimwambia:
“Ole wako, ‘Uthmaan! WaLlaahi, wewe ni mtu mwenye busara na mwerevu unayetofautisha haki na batili. Masanamu mnayoyaabudu ni mawe yasiyosikia, hayaoni wala hayana faida wala madhara!”
‘Uthmaan alisema”
“Ndiyo hasa. WaLlaahi, si chochote lakini ni kama ulivyosema.”
Abu Bakr alisema.
“Huyu Muhammad bin ‘Abdillaah, ambaye Allaah Alimtuma kuwa Mjumbe kwa binadamu wote. Je, ungependa kuja kumsikiliza?”
‘Uthmaan alijibu:
“Ndiyo, Ninataka.”
Walipokuwa katika hali hiyo, Mjumbe wa Allaah alifika akifuatana na ‘Aliy bin Abi Twaalib aliyekuwa amebeba kanzu. Abu Bakr alipomwona akija, alimsogeza karibu yake na kumnong’oneza kitu. Alikaa kitako na alimwambia ‘Uthmaan:
“Ewe ‘Uthmaan! Mjibu Allaah kuhusiana na Pepo Yake. Mimi ni Mjumbe wa Allaah kwako na Viumbe Wake.”
‘Uthmaan alisema:
“WaLlaahi baada ya kusikia maneno hayo, sikuweza kujizuia ila kurejea katika Uislamu, na nikatamka Shahada: “Nakiri kwa moyo ya kuwa hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah, na kuwa Muhammad ni Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Mjumbe Wake.”
Kuhajiri Kwake
Mateso waliyofanyiwa Waislamu na makafiri wa Makkah yalitofautiana kulingana na hadhi ya mtu. Wanyonge kama vile; watumwa na watumwa walioachwa huru waliteswa sana. Makafiri walijitahidi kuwakashifu na kuwazuia kuukubali Uislamu. Hoja ya mbinu hiyo ilikuwa kuwashajiisha wadogo kuwa dhidi yao.
Ama watu watukufu, kama wale wa makabila yenye nguvu, machifu wa makabila yao walitekeleza jukumu hilo. Adhabu ilikuwa kupigwa au kuwekwa kizuizini.
‘Uthmaan aliporejea katika Uislamu, ‘ammi yake Al-Hakam bin Abil-‘Aasw bin Umayyah alimfunga mnyororo na kumwambia:
“Je unaitelekeza dini ya mababu zako na kufuata dini ya mzushi? WaLlaahi, sitokufungua mpaka utakapoacha dini uliyoingia.”
‘Uthmaan alijibu:
WaLlaahi sitoiacha wala kusogea inchi moja kutoka katika dini hiyo.”
Al Hakam alipoona anang’ang’ania katika dini yake, aliondoka.
Makafiri hawakuacha kuwatesa na kuwaadhibu Waislamu. Mjumbe wa Allaah alipoona yaliyokuwa yakiwasibu Waislamu, na kuwa hakuweza kuwatetea, aliwambia:
“Itakuwa vema kwenu kuhamia (kukimbilia) Ethiopia, kwa kuwa kuna Mfalme anayewatendea vizuri watu (raia) wake. Ni nchi ya ukweli, na nataraji Allaah Atawawezesha kwenda huko.”[2]
Baada ya maelezo hayo, Waislamu walikwenda Ethiopia wakikimbia mateso na wakikimbilia kwa Allaah pamoja na dini yao. Hawa walikuwa Waislamu wa mwanzo kuhama.
Juu ya kuhama kwa ‘Uthmaan na mkewe, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Allaah awe pamoja nao, kwa kuwa ‘Uthmaan alikuwa wa mwanzo kukimbilia kwa Allaah baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Luut.
Kubashiriwa Pepo na Ushahidi
Abu Muusa alisimulia.
Siku moja, nilikuwa nimekaa katika bustani na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Al-Madiynah, alipokuja mtu na kuomba ruhusa ya kuingia.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Mfungulie lango, na umbashirie Pepo.” Kwa hiyo nilimfungulia, alikuwa Abu Bakr, nilimbashiria Pepo. Mtu mwingine alikuja na kuomba ruhusa ya kuingia. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Mfungulie lango, na umbashirie Pepo.”Alikuwa ‘Umar. Nilimfungulia, na nikampa habari njema za Peponi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameegemea kisha akasimama wima na kusema:
“Mfungulie lango, na mbashirie Pepo na utukufu utakaomshukia.” Alikuwa ‘Uthmaan. Nilimfungulia lango na nikampa habari njema za Peponi, na nikamwambia aliyodhukuru Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
’Uthmaan alisema; “Allaah pekee Ndiye Anayestahili kuombwa msaada.”[3]
Katika mapokezi mengine Anas alisema:
“Mjumbe wa Allaah, Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan walipanda Mlima Uhud. Mlima ulipotetema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Nyamaza (tulia) Ewe Uhud kwa sababu kuna Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mkweli na Mashahidi wawili juu yako.”
Hadiyth ya tatu iliyosimuliwa na Sa’iyd bin Zayd inaeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:-
“Abu Bakr yumo Peponi. ‘Umar yumo Peponi. ‘Uthmaan yumo Peponi. ‘Aliy yumo Peponi. Twalhah yumo Peponi. Az-Zubayr yumo Peponi. ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf yumo Peponi, na Sa’d yumo Peponi.”
Sa’iyd aliongezea kusema:
“Na kama utapenda nikutajie mwingine, Nitakutajia.” Kisha akajitaja.”[4]
Mwandishi wa Wahyi
Zaidi ya sifa bainifu njema za ‘Uthmaan alikuwa mmoja wa waandishi wa wahyi. Alisimulia ‘Aaishah:
“Nilimwona Mjumbe wa Allaah akiegemeza paja lake kwa ‘Uthmaan, nilipokuwa nikimfuta jasho usoni mwake wahyi ulipokuwa ukimteremkia alimwambia ‘Uthmaan: “Ewe ‘Uthmaan andika, WaLlaahi, mja huyo ana hadhi mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wa Allaah, na Allaah Aliridhia kutukuzwa kwake!
Alisimulia Ja’far bin Muhammad kwa mamlaka ya baba yake”
“Kila Mjumbe wa Allaah alipokaa, Abu Bakr alikuwa kuliani kwake, ‘Umar alikaa kushotoni kwake na ‘Uthmaan alikaa mbele yake, kwa sababu alikuwa katibu myeka wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).”
Aliyekusanya Qur-aan Tukufu
Wakati wa kupeleka jeshi Armenia, kulikuwa na majeshi mawili ya Waislamu. Moja lilitoka Syria na jengine kutoka Iraaq. Hudhayfah bin Al-Yamaani alishiriki katika jeshi hilo na aligundua tofauti katika matamshi ya baadhi ya maneno katika Qur-aan.
Watu wa Kuufah walisoma Qur-aan kwa mujibu wa mapokezi ya ‘Abdullaah bin Mas’uud ambapo watu wa Syria walisoma kwa mujibu wa mapokezi ya Ubay bin Ka’b
Hudhayfah alichelea tofuati hizo, hivyo alikwenda kwa ‘Uthmaan Khaliyfah na kumwambia:
“Ewe Jemedari wa Waumini! Okoa hili taifa kabla hawajatofuatiana wao kwa wao juu ya Kitabu chao, kwa sababu Mayahudi na Wakristo walitofuatiana kuhusu vitabu vyao.”
‘Uthmaan alitoa khutbah ambapo alisema:
“Enyi watu! Miaka michache imepita tangu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefariki dunia, na mwatofautiana kuhusu Qur-aan, nasema: “Haya ni masimulizi ya Ubay na yale ni masimulizi ya ‘Abdullaah, kwa hiyo miongoni mwao watasema” WaLlaahi, huzisoma vizuri Aayah kadhaa wa kadhaa. Kwa hiyo, nawaalika kila mmoja wenu kuileta, endapo mna sehemu ya Kitabu cha Allaah.”
Watu walileta vipande vya karatasi au vipande vya ngozi vilivyoandikwa juu yake mpaka akikusanya vya kutosha.
Kisha ‘Uthmaan aliwaita walioleta ngozi na vipande vya karatasi na alimwuliza kila mmoja”
“Je uliisikia hii kutoka kwa Mjumbe wa Allaah na je, alikusomea?”
Mtu alijibu: “Ndiyo” Baada ya kusema hayo, alisema, “Nani mwandishi mzuri?”
Walijibu “Sa’iyd bin Al-‘Aasw.”
‘Uthmaan alisema:
“Sa’iyd atoe Imla na Zayd aandike.”
Kwa ajili hiyo Misahafu iliandikwa na kugawanywa kwa watu.[5]
‘Uthmaan alimtuma Hafswah bint ‘Umar mkewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amletee hati iliyokunjwa inakiliwe kwenye Msahafu, kisha alirejeshewa.
Hati zilizokunjwa ziliandikwa wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr baada ya vita ya Al-Yamamaah wakati Maswahaba wengi waliohifadhi Qur-aan walikufa shahidi.
Wakati huo ‘Umar alimwambia Abu Bakr, “Maswahaba wengi waliohifadhi Qur-aan waliuawa siku ya Al-Yamaamah, nachelea kusije kupotea kitu katika Qur-aan. Kwa hiyo nakutaka uamuru ukusanyaji wake.
Kwa matokeo hayo, Abu Bakr alimwambia Zayd bin Thaabit akusanye kutokana na ngozi, kutoka Al-Asab (matawi ya mtende yaliyoondolewa majani yake, ambapo sehemu ya Qur-aan iliandikwa juu yake na kutoka mioyo ya Ummah na Kiislamu. Zile hati zilizokusanywa alikuwa nazo Abu Bakr na kisha ‘Umar alipofariki dunia zilitunzwa na Hafswah bint ‘Umar. Kisha ‘Uthmaan alizichukua na alimwamuru Zayd bin Thaabit, Abdullaah bin Az-Zubayr, Sa’iyd bin Al-Aasw, ‘Abdur-Rahmaan bin Al-Haarith bin Hishaam azinakili katika Mus-haf.
Kwa hiyo ‘Uthmaan aliwapa maelekezo yafuatayo:-
“Endapo mtatofuatiana juu ya kitu chochote, kiandikeni kwa mujibu wa lugha ya Kiquraysh kwa sababu ilishushwa kwa lugha hiyo.”
Hivyo walifanya, baada ya kunakili hati zilizokunjwa (scrolls), ‘Uthmaan alizirejesha kwa Hafswah na kisha akapeleka nakala ya Msahafu kwa kila jimbo na aliamuru aina nyengine ya Mus-haf ichomwe moto. Ulimwengu wa Kiislamu unashukuru kwa kitendo hiki cha ‘Uthmaan.
Iwapo tungeorodhesha aliyofanya ‘Uthmaan katika njia ya Allaah tungeweza kutengeneza orodha kamili. Hapa inatosha kutaja matukio matatu ambayo ni ushahidi ulio wazi juu ya utoaji wake mkubwa kwa ajili ya Allaah.
Kutoa Katika Njia ya Allaah
Kuliandaa jeshi kwa Vita ya Taabuuk
Vita ya Taabuuk inaitwa ‘Vita ya majonzi baada ya kauli ya Allaah. (9:117).
“Allaah Amekwishapokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari waliomfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu.” (9: 117)
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwataka watu kuelekea vitani na aliwafahamisha sehemu waliyokuwa wakienda ili wajiandae. Aliwanasihi watu wa Makkah na makabila ya Kiarabu kupigana na akawataka watu kutoa sadaka na akawataka watoe katika njia ya Allaah. Watu wengi waliitikia kwa kutoa mali nyingi kama sadaka.
Wa kwanza kutoa sadaka yake alikuwa Abu Bakr ambaye alitoa mali yake yote iliyofikia Dirham 4000.
’Umar alitoa nusu ya mali yake.
‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf alitoa wakia (ounce) 200 za dhahabu na fedha.
‘Aaswim bin ‘Adiy wasaqi 70 za tende.
‘Uthmaan alitoa zana kwa thuluthi ya jeshi (1/3), ngamia 950 na farasi 50.
Ibn Is-haaq alisema: “‘Uthmaan alitoa kiasi kikubwa kwa kulipa jeshi zana za kivita. Hapana aliyetoa zaidi yake katika njia hii. Alipeleka dinari elfu moja na kuziweka juu ya paja la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “‘Uthmaan hawezi kudhuriwa na chochote kuanzia siku ya leo.” (At-Tirmidhiy).
Kisima cha Rumah
Kuna tukio jingine linaloonesha mapenzi ya hali ya juu na huruma huyu Swahaba.
Mali zote za dunia si chochote ikilinganishwa na alichoahidi na Allaah. Waja wake walitumia miongoni mwa alivyowapa.
Muhajirina walipofika Madiynah walipata matatizo ya ukosefu wa maji ya kutosha. Mtu mmoja katika Banu Ghifaar alikuwa na kisima kikiitwa ‘Rumah’ na akiuza kiriba kimoja cha maji kwa Mudd moja.”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwuliza:
“Je unakiuza kwa chemchemi ya Peponi?” Yule mtu alijibu: “Ewe Mjumbe wa Allaah! Sina kitu zaidi ya hiki, siwezi kufanya hivyo.”
‘Uthmaan alipofahamishwa hilo, alikinunua kwa dirham 35,000 na alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Je mtapewa chemchemi Peponi, kama nitatoa Bishr kama ulivyofanya?” Mjumbe wa Allaah alisema: “Ndiyo.”
‘Uthmaan alimwambia: “Nimeshakinunua, na nawapa Waislamu.[6] Abu Hurayrah alisema; “‘Uthmaan alinunua Pepo mara mbili” Siku ya Rumah na ile “Siku ya Huzuni”[7]
Upanuzi wa Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
Siku moja watu walialikwa kuchangia ununuzi wa kipande cha ardhi kilichokuwa karibu na Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili upanuliwe. Kama ada, ‘Uthmaan alikwenda kuinunua ile ardhi na iliunganishwa na Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Qataadah alisimulia: Kulikuwa na ardhi jirani na Msikiti. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Nani atakinunua, na atapewa kingine Peponi.
Hayaa/Soni
‘Uthmaan alikuwa mwingi wa haya, na soni humfanya mtu awe mzuri, awe mwanaume au mwanamke. Na kwa ‘Uthmaan ndiyo iliyomfanya kuwa safi na mbali na mambo ambayo yangemchafulia sifa yake. Hayaa ilikuwa ni sifa yake kubwa hata hivyo alikuwa mtu mashuhuri pamoja na kuwa na soni.
Al-Hasan akielezea hayaa (soni) yake: “Angekuwa ndani ya nyumba na milango imefungwa na angekuwa anavua nguo ili kujimwagia maji mwilini. Soni ilimzuia kusimama wima.”[8]
Alikuwa na soni ya kipekee. ‘Uthmaan hakuwa na hayaa mbele ya watu tu bali alikuwa na hayaa hata kwa majini wasioonekana na Malaika ambao walikuwa wanaishi. Kwa hiyo alikuwa na soni iliyoenea kote. Anas alisimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Mkarimu zaidi katika ummah wangu ni Abu Bakr. Mkali zaidi katika masuala ya dini ya Allaah ni ‘Umar. Na mwenye soni ya ukweli ni ‘Uthmaan.”[9]
Mtu mwenye soni kwa kawaida huchunga ulimi wake na ni mwenye bashasha, na anapozungumza huchagua maneno ili asimuudhi yeyote. Sifa hii inamfanya mtu aheshimiwe katika hivyo watu waliamiliana nao na ‘Uthmaan alikuwa mwenye uadilifu na staha.
‘Aishah alisema:
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameegemea nyumba yake na miguu na mapaja yakiwa wazi.
Abu Bakr na ‘Umar waliomba rukhsa ya kuingia, na walipoingia, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alibaki katika hali ile ile. Waliteta na kisha ‘Uthmaan aliomba rukhsa ya kuingia. Papo hapo Mjumbe wa Allaah alikaa wima na kujifunika. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ‘Uthmaan waliteta. Alipotoka, nilimwuliza. “Ewe Mjumbe wa Allaah! Abu Bakr na ‘Umar waliingia, lakini hukukaa wima. Lakini alipoingia ‘Uthmaan ulikaa wima na kujifunika.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimjibu: nisimwonee hayaa mtu anayeonewa hayaa na Malaika?”[10]
[2] As-Siyrah An-Nabawiyyah ya Ibn Hishaam
[3] Al-Bukhariy na Muslim
[4] ‘Usudul Ghaabah 3/580
[5] Imeripotiwa na Ibn ‘Asaakir
[6] Siyar A’laam An-Nubalaa’
[7] Al-Haakim 3/107 (Ni wazi kuwa maneno ya Abu Hurayrah hapana maana ya kuwa Mtume alikuwa akiuza Pepo kama ilivyofanywa na Makasisi wa kanisa la Roma (R.C.), ‘Uthmaan alistahili Pepo kutokana na ‘amali zake. Kutokana nazo, mbili zilitajwa na Abu Hurayrah kwa kununua kisima cha Rumah, tunathibitisha ya kuwa ‘Uthmaan alikuwa mtu mkarimu kwa niaba ya Waislamu, na hii, inadhihirisha ya kuwa Imani thabiti kwa Allaah. “Inasemwa ya kuwa yule asiyejali mambo ya Waislamu si miongoni mwao.”
[8] Musnad Ahmad 543
[9] Imeripotiwa na Ibn ‘Asaakir
[10] Muslim