Makasudio Sahihi Ya Aliyekunja Uso (Suwrat ‘Abasaa) Kujibu Tafsiri Ya Wapotoshaji
Makasudio Sahihi Ya Aliyekunja Uso (Suwrat ‘Abasa)
Kujibu Tafsiri Ya Wapotoshaji
Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy (Rahimahu Allaah)
Imepokelewa kuwa siku moja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa na wakubwa wa Ma-Quraysh akiwalingania Diyn kwa hima kubwa akitaraji kuwa wakisilimu wakubwa hao, na wanyonge wao watafuata kwa sababu wengi kati ya wanyonge walitaka kusilimu lakini walijizuia kwa kuwaogopa wakubwa wao hao.
Wakati huo akatokea kipofu mmoja aliyesilimu tokea zamani aitwaye Ibn Ummi Maktuwm (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), na bila kujua kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameshughulika akawa anampigia kelele kumwambia: “Ee Rasuli wa Allaah, nifunze na mimi katika aliyokufunza Allaah.”
Akawa anayarudia maneno hayo, na kwa vile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameshughulika kutaka kuwasilimisha viongozi wale wakubwa, akamfinyia uso yule kipofu wala asimsikilize, ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipomteremshia aayah za mwanzo za Suwrah-‘Abasa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
عَبَسَ وَتَوَلَّىٰ ﴿١﴾ أَن جَاءَهُ الْأَعْمَىٰ ﴿٢﴾ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّهُ يَزَّكَّىٰ ﴿٣﴾ أَوْ يَذَّكَّرُ فَتَنفَعَهُ الذِّكْرَىٰ ﴿٤﴾ أَمَّا مَنِ اسْتَغْنَىٰ ﴿٥﴾ فَأَنتَ لَهُ تَصَدَّىٰ ﴿٦﴾ وَمَا عَلَيْكَ أَلَّا يَزَّكَّىٰ ﴿٧﴾ وَأَمَّا مَن جَاءَكَ يَسْعَىٰ ﴿٨﴾ وَهُوَ يَخْشَىٰ ﴿٩﴾ فَأَنتَ عَنْهُ تَلَهَّىٰ ﴿١٠﴾ كَلَّا إِنَّهَا تَذْكِرَةٌ ﴿١١﴾ فَمَن شَاءَ ذَكَرَهُ ﴿١٢﴾
Alikunja kipaji na akageuka. Alipomjia kipofu. Na nini kitakachokujulisha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) huenda akatakasika? Au atawaidhika na yamfae mawaidha? Ama yule ajionaye amejitosheleza. Nawe unamgeukia kumshughulikia. Na si juu yako asipotakasika. Ama yule aliyekujia kwa kukimbilia. Naye anakhofu. Basi wewe unampuuza. Laa hasha! Hakika hizi (Aayah) ni mawaidha. Basi atakaye ahifadhi na awaidhike. [Suwrah ‘Abasa (80: 1 - 12]
Shia wanasema kuwa makatazo ndani ya aayah hizi si kwa ajili ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu si yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekunja uso na kugeuka na kwamba yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawezi kukunja uso wala kukosolewa, bali aliyekosea na kukosolewa ndani ya aayah hizo ni ‘‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu).
Tatizo ni kuwa baadhi yao hawana uoga hata kidogo, na wako tayari kubadilisha maneno ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa), kwa ajili ya kutaka kuiuza bidhaa yao mbovu.
Sisi Tunasema: Lau kama aliyeteremshiwa aayah hizi ni ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), basi hii ni sifa kubwa kwake, kwa sababu mtiririko wa aayah unatujuulisha kuwa aliyekatazwa ni mtu aliyekuwa akiwalingania watu katika Diyn, na hii ni sifa nzuri hata kama atakatazwa au kukaripiwa kidogo na Mola wake (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
عَبَسَ وَتَوَلَّىٰ ﴿١﴾أَن جَاءَهُ الْأَعْمَىٰ ﴿٢﴾وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّهُ يَزَّكَّىٰ ﴿٣﴾
Alikunja uso na akageuka. Kwa sababu alimjia kipofu. Na nini kitakachokujulisha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) huenda akatakasika? [‘Abasa: 1-3]
Kutokana na Aayah hizi, (kwa rai ya Shia) inaleta maana kuwa kipofu (‘Abdullaah mwana wa Ummi Maktuwm), hakumuendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wala hakumuendea ‘Aliy bin Abi Twaalib wala Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliokuwepo mahali hapo, bali alimuendea ‘‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) kwa ajili ya kutaka kupata mawaidhah na uongofu kutoka kwake. Kwa sababu aliyekunja uso ni ‘‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) na si Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Huu ni ubabaishaji wa maneno, kwa sababu aayah zinatufahamisha kuwa aliyejiwa ndiye aliyekunja uso, na haiwezekani kwa mwana wa Ummi Maktuwm kumuacha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuendea ‘‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu).
Kama wangelitafakari kidogo tu kabla ya kuandika maandishi yao haya yenye sumu, wangeligundua kuwa maneno yao ni utovu wa adabu dhidi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Hadiyth sahihi zinasema kuwa kipofu yule alimuendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku akimuambia: “Nifundishe katika yale Aliyokufundisha Allaah.” Akawa anaendelea kuyakariri maneno hayo, na kwa vile yeye ni kipofu, hakuelewa kuwa wakati ule Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameshughulika kutaka kuwasilimisha wakubwa wa Ma-Quraysh waliokuwa naye akiwa na tumaini kuwa huenda mmoja wao atasilimu. Ndipo alipokunja uso na hakumjibu, na hapo ndipo zilipoteremshwa aayah za kumkosoa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Na hili ni jambo la kawaida kwa mtu yeyote anayekatwa maneno wakati akizungumza, na hili ni funzo kwetu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuwa tusiwakate watu maneno wanapozungumza kwa sababu hili ni jambo linalokera.
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumdharau kipofu yule wala hakumkaripia kwa kumuambia kwa mfano: “Nyamaza!” au “Ondoka hapa!” bali alikunja uso wake tu bila kumjibu. Lakini Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) alimkaripia Rasuli wake na kipenzi chake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kuwa kipofu yule hawezi kuuona uso wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala kujua kuwa amekasirikiwa.
Ikiwa Aayah hizi ameshushiwa ‘‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), kwa nini basi asikaripiwe kwa unafiki na ukafiri wake kama Mashia wanavyoamini kuwa yeye ni mnafiki. Wakati kitendo cha unafiki ni kikubwa zaidi na kinachostahiki zaidi kukaripiwa kuliko kukunja uso.
Wengine wakasema kuwa eti mwana wa Ummi Maktum hakuwa akiuliza mambo ya Diyn, bali ni mambo ya kidunia tu ndiyo maana akamuendea ‘Uthmaan!
Enyi Shia! Hebu zingatieni vizuri mtiririko wa hizi Aayah:
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَأَمَّا مَن جَاءَكَ يَسْعَىٰ ﴿٨﴾وَهُوَ يَخْشَىٰ ﴿٩﴾فَأَنتَ عَنْهُ تَلَهَّىٰ ﴿١٠﴾كَلَّا إِنَّهَا تَذْكِرَةٌ ﴿١١﴾فَمَن شَاءَ ذَكَرَهُ ﴿١٢﴾
Ama yule aliyekujia kwa kukimbilia. (Ee ‘Uthmaan?) Naye anakhofu (Anakhofu nini?). Basi wewe unampuuza. Laa hasha! Hakika hizi (Aayah) ni mawaidha. Basi atakaye ahifadhi na awaidhike. (Awaidhike na nini?).”
Kama Aayah hizi ametereshiwa ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), basi ni sifa kubwa kwake kwa kukimbiliwa na kutakiwa amsikilizishe kipofu yule mawaidhah apate kuongoka.
Kwa kila mwenye kupenda haki, musikubali kudanganywa na tafsiri kama hizi zenye kubadilisha maneno ya Allaah na kupotosha.
Hii si mara ya mwanzo kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukosolewa ndani ya Qur-aan tukufu. Na sisi tunaamini kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakosolewi kwa kuwa amefanya kitendo cha dhambi, bali hukosolewa kutokana na kujitahidi kwake sana au kwa ajili ya huruma nyingi aliyonayo au kwa ajili ya kuwataka watu waingie haraka ndani ya Diyn ili waepukane na Moto kama ilivyoelezwa katika Suwratul-Kahf.
Allaah Anasema:
فَلَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ عَلَىٰ آثَارِهِمْ إِن لَّمْ يُؤْمِنُوا بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ أَسَفًا﴿٦﴾
Basi huenda ukaiangamiza nafsi yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa ajili yao kusikitika kutokuamini kwao usimulizi huu (Qur-aan). [Al-Kahf: 6]
Ifuatayo ni mifano mingine michache:
Allaah Anasema:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ لِمَ تُحَرِّمُ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكَ ۖ تَبْتَغِي مَرْضَاتَ أَزْوَاجِكَ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١﴾
Ee Nabiy! Kwanini unaharamisha kile Alichokuhalalishia Allaah? Unataka kuwaridhisha wake zako; na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [At-Tahriym: 1]
Na Akasema:
مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُم أَصْحَابُ الْجَحِيمِ ْ﴿١١٣﴾
Haimpasi Nabiy na wale walioamini kuwaombea maghfirah washirikina japokuwa ni jamaa zao wa karibu baada ya kuwabainikia kwamba wao ni watu wa moto uwakao vikali mno. [At-Tawbah: 113]
Na Akasema:
مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَى حَتَّى يُثْخِنَ فِي الأَرْضِ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللّهُ يُرِيدُ الآخِرَةَ وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٦٧﴾
Haikumpasa Nabiy awe ana mateka mpaka apigane kuwaua na kuwajeruhi (maadui wa Allaah) nchini. Mnataka vitu vya dunia, na hali Allaah Anataka (mpate vya) Aakhirah. Na Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Anfaal: 67]
Sisi tunaamini kuwa hizi ni sifa njema na fahari kubwa kwa kiumbe kusemeshwa na kufundishwa na Rabb wake (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na kukosolewa kwa ajili ya huruma zake na wala si sifa mbaya. Lakini wanayoyatambua haya ni wenye akili peke yao.
Allaah Anasema:
لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٢٨﴾ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُلْ حَسْبِيَ اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ ۖ وَهُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ﴿١٢٩﴾
Kwa yakini amekujieni Rasuli anayetokana na nyinyi wenyewe, yanamtia mashaka (na huzuni) yanayokutaabisheni, anakujalini, mwenye huruma kwa Waumini ni mwenye huruma mno, mwenye rahmah. Na wakikengeuka, basi sema: Amenitosheleza Allaah; Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Kwake nimetawakali. Naye ni Rabb wa ‘Arsh adhimu. [At-Tawbah: 128-129]
Ndani Ya Vitabu Vya Kishia
Tafsiri sahihi kuwa aliyekusudiwa ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimo hata ndani ya vitabu vyao na tafsiri za ’Ulamaa wao wakubwa na maarufu, na zinakubaliwa na wanavyuoni mbali mbali wa Shia kuwa aliyekusudiwa ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Anasema At-Tubrusiy ambaye ni mmoja katika Ma’ulamaa wakubwa wa Shia Ithna-‘Ashariyah: “Kule kuambiwa ‘alayhis salaam kuwa aliukunja uso wake siyo tuhuma, kwake.” [Tafsiyr Majma’al Bayaan, ukurasa 266 Juzuu ya 10]
Tembelea tafsiri ya At-Tubrusiy katika anuani hii:
http://www.holyquran.net/cgi-bin/majma.pl
Anaendelea kusema At-Tubrusiy:
“Aayah hii imeteremshwa kwa ajili ya ‘Abdullaah mwana wa Ummi Maktuum na jina lake ni Shurayh bin Maalik bin Rabiy’ah Al-Fahary, anayetokana na kabila la Bani ‘Aamir bin Luay. Aliyemjia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wakati huo alikuwa akiwalingania ‘Utbah bin Rabiy’ah na Abu Jahal bin Hishaam na Al-‘Abbaas bin ‘Abdil Muttwalib na Umayah bin Khalaf akiwalingania wamuamini Allaah, akitarajia kusilimu kwao. Akasema (Mwana wa Ummi Maktuwm): “Ee Rasuli wa Allaah, nifunze na mimi katika Aliyokufunza Allaah.” Akawa anamuita huku akiyakariri maneno yale bila kujua kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameshughulika na watu wengine. Mpaka kuchukizwa na kukabainika usoni mwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na kukatwa maneno yake kila anapotaka kusema. Ikampitikia nafisini mwake kuwa wakubwa wa makafiri hawa watasema kuwa wafuasi wake ni vipofu na watumwa, akageuka asimjibu na kuwaelekea wale aliokuwa akiwalingania, ndipo zilipoteremka aayah.
Akawa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya siku ile akimkirimu na kila anapomuona, husema: “Karibu ewe ambaye kwa ajili yake Amenikosoa Mola wangu.” Kisha humuuliza: “Una haja yoyote?:” Na alimpa ugavana wa mji wa Madiynah mara mbili.”
Anaendelea kusema At-Tubrusiy ambaye ni mmoja wa Ma’ulamaa wakubwa wa Shia akijibu hoja za wenye madai hayo:
“Kutajwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amekunja uso siyo tuhuma kwake. Kama mtu atasema: ‘Ikiwa kweli amekosolewa, hii ina maana kuwa kumkunjia mtu uso ni dhambi?
Jawabu: ‘Kukunja uso au kutabasamu mbele ya uso wa kipofu si kitendo cha dhambi kwa sababu kitendo hicho hakimdhuru, na kwa ajili hiyo si kitendo cha dhambi.’
Huenda ikawa Allaah Amemkosoa Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili awe na tabia bora kupita zote na kumtanabahisha juu ya utukufu wa Muislamu anayetafuta uongofu na kumjuulisha kuwa kumuongoza Muislamu apate kuthibiti katika imani yake ni bora kuliko kutegemea kusilimu kwa mshirikina.”
(Mwisho wa kunukuu maneno ya At-Tubrusiy)
Mwanachuoni mwengine wa KiShia aitwae Al-Jibaiy anasema: “Ndani yake mna fundisho kuwa hapo mwanzo kitendo cha kukunja uso hakikuwa cha dhambi, mpaka amri ya kukataza ilipoteremka.”
Anaendelea kusema:
“Imepokelewa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa kila anapomuona ‘Abdullaah mwana wa Ummi Maktum humuambia: “Karibu karibu, hapana Wa-Allaah! Allaah Hatonikataza tena juu yako.” Na alikuwa mpole sana kwake.”
Maneno kama haya pia yamenukuliwa kutoka mmoja katika ’Ulamaa wakubwa wa Shia Muhammad Haadi Al-Yuusufiy kutoka kwa At-Tubrusiy katika kitabu chake ‘Encyclopedia ya Taariykh’ Juzuu ya 1, ukurasa 494.
Na maneno hayo pia yameandikwa na mwanachuoni wa ki-Shia Al-Majlisiy katika Bihaar al Anwaar, juzuu ya 17, ukurasa wa 78.
Yamenukuliwa maneno kama haya pia kutoka kwa mwanachuoni mkubwa wa ki-Shia katika wakati wetu huu Muhammad Husayn Fadhlullah katika tafsiri yake ‘Wahyul Qur-aan’.
Atakaye anaweza kuutembelea ukurusa huo katika mtandao wake unaopatikana penye anuani ifuatayo:
http://arabic.bayynat.org.lb/books/quran/abas1.htm
Hebu tumsikilize Ayatullah Muhammad Husayn Fadhlullah akiwajibu Mashia wenzake wanaosema kuwa waliokusudiwa katika aayah zile ni ‘Uthmaan au mtu katika watu wa kabila la Bani Umayyah. Anasema mwanachuoni huyu wa ki-Shia:
“Riwaya inayonasibishwa na Imaam Asw-Swadiq (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) kuwa aayah imeteremshwa kwa ajli ya mtu wa kabila la Bani Umayyah haikubaliani na mtiririko wa aayah. Kwa sababu ni wazi kuwa kusudi la aayah hizo ni kuwa aliyekusudiwa ni mtu mwenye kumiliki sehemu muhimu katika kuifikisha risala na kwamba mtu huyo anabeba jukumu la kuwatakasa na kuwafundisha wale waliokwisha hidika na kuikubali risala hiyo kwanza, ili wawe na msingi mzuri na uwezo wa kuifikisha Dini kwa watu, kinyume na wale wasiohidika ambao hawastahiki kupewa juhudi kubwa.”
(Mwisho wa maneno ya Muhammad Husayn Fadhlullah)
Kutokana na haya, tunaona kuwa waliosema kuwa aliyekusudiwa katika aayah zile ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) si Masunni peke yao. Bali pia yamesemwa na Maulamaa wakubwa wa ki-Shia ambao ni At-Tubrusiy, Al-Majilisy, Al-Yuusufiy na Muhammad Husayn Fadhlullah kama tulivyoona.
Na hii chini ni anuani ya mtandao unaoitwa Az-Zahraa wa mwanachuoni wao aliyesema uongo juu ya aayah hizi, na ndani ya mtandao huu zimo hotuba mbili za Muhammad Fadhlullah akitamka kuwa aayah hizo ziliteremshwa kwa ajili ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
http://www.mezan.net/sounds_files/sounds1/7/r007.html