09-Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Sura Ya 7: Jihaad, Mitihani Na Kifo Chake
Sura Ya 7: Jihaad, Mitihani Na Kifo
Jihaad Yake
Maisha ya Ibn Taymiyyah yalitengana (na maisha ya watu wengine) kwa kuwa na sifa kubwa kubwa za kuamrisha mema, kukataza maovu na kufanya Jihaad kwa ajili ya Allaah. Alichanganyisha nafasi yake ya kusomesha, utoaji wa fatwa za kishari’ah na uandishi pamoja na matendo yenye nafasi ya juu kabisa. Ukweli ni kwamba, maisha yake yote yalizungukwa na Jihaad. Pamoja na maelezo mafupi mno ya kuangalia maisha yake ndani ya nyanja hii, tunaweza kuona idadi kadhaa ya matukio:
Jihaad Yake Katika Kuamrisha Mema na Kukataza Maovu
-Uharibifu wake wa masanamu na maeneo, kama vile uharibifu wa nguzo, ndani ya Masjid at-Taariykh huko Damascus, ambao watu walikuwa wakiiombea kutokana na nguzo hiyo baraka,[1] na vitu vyote ambavyo vilikuwa vikitumika kwa kuviabudia kinyume na Allaah na ambavyo kuwazuia watu kuzuru sehemu kama hizo. Tendo hili kakamavu lilitanguliwa na hatua mbili: kwanza, kwa kueleza ukweli wa sehemu hizi (zinazodhaniwa kuwa ni tukufu) ambazo nyingi zao zilisimuliwa kwa uharibifu na kwamba makaburi mengi ambayo yakitukuzwa na kufanyiwa ziara kwayo, ukweli ni kwamba yalikuwa hayana mnasaba wowote kwa wale wanaowasifia nao.[2] Pili, kwa njia ya mijadala ya kitaalamu kupitia mahojiano ya moja kwa moja, vitabu na barua, na kuelezea shirki hiyo na uzushi unaoungama katika matendo kama hayo na pia kupitia uwasilishaji wa maoni ya wapinzani na kuzikana hoja zao.
-Aliandika barua kwa aliyekuwa Mfalme wa Ukiristo nchini Cyprus akimualika katika Uislamu na kuweka wazi uongo na ufisadi unaofanywa na mapadri na watawa hali ya kuwa wakielewa vyema kwamba walikuwa juu ya upotovu. Baada ya kutaja uchaji Allaah wa Mfalme, mapenzi yake ya elimu na tabia zake nzuri kwa watu, Ibn Taymiyyah baadaye akamualika kuingia katika Uislamu na kufuata imani sahihi. Alifanya hivi katika mtindo laini na wenye maelezo yanayoelezea utaalamu wake, na akimuhimiza kuwa na ukarimu mbele ya Waislamu waliopo nchini Cyprus, wala asithubutu kubadili dini ya hata mmoja miongoni mwao.[3] Pia aliingia kwenye mijadala pamoja na Wakiristo, baadhi yake yeye mwenyewe aliinukuu ndani ya kitabu chake cha al-Jawaab as-Swahiyh.[4]
-Alifanya vikao vingi dhidi ya Masufi. Moja ya kikao chake maarufu kilikuwa dhidi ya Bataa'ihiyyah.[5] Aliwakana na kuweka wazi tabia zao za ki-Shaytwaan kama vile kuingia ndani ya moto na kutoka bila ya jeraha na madai yao kwamba hilo ni kuonesha miujiza yao ya kiasili. Alieleza kwamba hata kama wakifanya hivi au kuruka angani, haitokuwa ni ushahidi kwamba yanaweza kutumika kutangaza ukiukwaji wao wa Shari’ah kuwa ni sahihi.[6] Aliwapa changamoto kwa kuwataka kuingia kwenye moto pamoja nae kwa masharti kwamba awali ya yote wajikoshe kwa siki na maji ya moto. Hatimaye, waliwekwa wazi na kushindwa na wakakubali utiifu wa moja kwa moja katika Qur-aan na Sunnah.[7]
Ndani ya mwaka 699H, yeye na idadi kadhaa ya swahibu zake walipambana na wauzaji walevi; wakavunja vyombo vyao, kumwaga ulevi wao na kuwatwiisha kwa adhabu idadi yao kadhaa, (tendo ambalo) liliwafanya watu kutoka nje na kushangilia jambo hili.[8]
-Ama kwa vikao vyake dhidi ya watawala na nasaha zake kwao, vilikuwa ni maarufu. Moja kati ya kikao chake maarufu mno kilikuwa dhidi ya Ghaazaan, mtawala wa Tartar. Katika kipindi ambacho Tartar waliamuru vitisho na utawala (wa kidhalimu), alizungumza kwa mtawala akiwa na maneno makali kuhusiana na vitendo vyao, wakitandaza ufisadi na kwenda kinyume na vikwazo vya Waislamu hali ya kuwa wao wenyewe wakidai kuwa ni Waislamu. Vivyo hivyo, maneno yake mazito kwa Sultaan an-Naaswir, yalimlazimu Sultaan huyo kuacha kutekeleza matendo yasiyofaa kishari’ah.[9]
-Ibn Taymiyyah pia alikuwa anawaathiri watawala kurudia kwenye jukumu lao la kuamrisha mema na kukataza maovu. Mfano wa hili ni pale rushwa ilipotanda mno na ikaja kutambulika kama ni zana ya kuwezesha kupata nafasi za kiofisi na pia katika kukimbia adhabu ya kifo mnamo mwaka 712H, amri rasmi ikapelekwa Damascus, kutoka kwa Sultaan, ikieleza kwamba hakuna mtu yeyote atakayeruhusika kupatiwa nafasi au ofisi kupitia njia za pesa au rushwa na kwamba muuaji ahukumiwe kwa mujibu wa Shari’ah; amri hii ilitokana na ushauri wa Ibn Taymiyyah.[10]
Kuna mifano mengine inayofafanua jitihada za Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah), katika kuamrisha mema na kukataza maovu. Nitaeleza baadhi ya matukio hayo hapa chini kwa upana:
Jihaad Yake Dhidi Ya Wazushi na Madhehebu Potofu
Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah alijitolea jitihada zake kubwa katika kuyakana madhehebu tofauti mbalimbali. Yeye binafsi aliwahi kwa mwili wake kuwapa changamoto baadhi ya watu kutoka dhehebu la kizawa la Kisufi, ambalo likitambulikana kama ni Bataa’ihiyyah ambalo lilijihusisha kwenye michezo kama vile kutembea juu ya moto ili kuwashangaza jamii kubwa ya watu. Aliwaomba kutembea pamoja naye juu ya moto kwa sharti kwamba wajioshe wenyewe kwanza kwa siki na maji ya moto. Ukataaji wao uliziweka wazi ujinga wao, na hivyo Ibn Taymiyyah akauweka wazi uongo wa dhehebu la Bataa’ihiyyah.[11] Hali kadhalika, alimkana Muhiyyud-Dyin Ibn ‘Arabiy na upotofu wa Wahdat al-Wujuud.
Ibn Hajar alisema, ‘... Kutokana na sifa za ajabu za mtu huyu (yaani Ibn Taymiyyah) ni kwamba alikuwa ni mtu mwenye nguvu sana miongoni mwa watu dhidi ya watu wa uzushi, Marawaafidhah, Mahuluuliyyah, na Waittihaadiyyah, na kazi zake katika hili ni nyingi na maarufu, na fataawa katika hayo hazina idadi... Ni wajibu wa mtu, ambaye ni mtaalamu wa elimu na amepata ufahamu kwamba atilie maanani maneno ya mtu ambaye imeegemea (elimu yake) katika vitabu vyake maarufu au kutokana na ndimi za wale watu waaminifu wanaofikisha maneno yake kwa usahihi – kisha kujitenga na yale yote yaliyokanwa na kujiamuru kutokana nayo kwa lengo la kutoa ushauri sahihi na kumshukuru kwa sifa zake nzuri kabisa na kwa yale aliyokuwa sahihi kama ilivyo njia ya Wanachuoni.
Iwapo hakuna sifa zozote za Shaykh Taqiyud-Diyn (Ibn Taymiyyah) isipokuwa kwa mwanafunzi wake maarufu Shaykh Shamsud-Diyn Ibn Qayyim al-Jawziyyah, mwandishi wa kazi nyingi, ambazo kutokana nazo wapinzani na wafuasi wake walinufaika nazo, basi hii itakuwa ni ushahidi tosha wa nafasi yake adhimu (Ibn Taymiyyah). Na kwanini iwe vyenginevyo pale ambapo Maimaam wa Kishaafi’iy na wengine, wala usizungumzie Mahanbali, katika kipindi chake kuthibitisha sayansi yake (ya Kiislamu) muhimu.[12]
Ama kwa mnasaba wa kuwakana watu wa uzushi na hatari waliyonayo kwa Waislamu, Ibn Taymiyyah amesema, ‘Pindipo baadhi ya watu walipomuuliza Imaam Ahmad Ibn Hanbal kwamba hawajisikii vizuri katika kuwapinga watu, aliwajibu, ‘Iwapo mimi ni wa kukaa kimya, ni namna gani watu wajinga walio wengi watauelewa ukweli kutokana na uongo?’ Wale walioanzisha maandiko ya kipotofu ambayo yanapingana na Qur-aan na Sunnah na wale waliozua mambo ya ‘ibaadah, basi ni wajibu juu yao kwamba waelezewe na kwamba Waislamu watahadharishwe dhidi yao – kwa makubaliano ya Wanachuoni Waislamu walio wengi. Ukweli ni kwamba, pale Imaam Ahmad bin Hanbal alipoulizwa kuhusiana na mtu anayefunga, kuswali na kujitenga pekee ndani ya Msikiti kwa ‘ibaadah; iwapo atakuwa ni mtu muhimu kwake kuliko mtu anayezungumza dhidi ya wazushi? Alisema, ‘Pale anapofunga na kuswali na kujitenga pekee, basi anafanya kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe. Hata hivyo, pale anapozungumza dhidi ya wazushi (watu wa bid’ah), anafanza hivyo kwa manufaa ya Waislamu kwa ujumla wake, na hili ni bora zaidi.’
Hivyo ilikuwa wazi kwamba kuwakana wazushi wazi wazi ni ya manufaa ya jumla kwa Waislamu na inatambulikana kama ni aina mojawapo ya mapambano katika njia ya Allaah. Kwani kuisafisha Diyn ya Allaah na kuitetea kutokana na mavamizi ni wajibu wa kiujumla – kama ilivyokubaliwa na Wanachuoni. Kwani, iwapo Allaah Asingeliwanyanyua baadhi ya watu kuwapinga wazushi, basi Diyn hii ingelishtadi kwa madhara, ufisadi na upotofu. Kwa hakika, aina hii ya ufisadi ni kubwa zaidi kuliko ufisadi unaotokana na wasioamini wanapowateka Waislamu. Kwani pale wasioamini wanapowateka nyara Waislamu, hawaharibu mioyo yao, au Diyn yao, isipokuwa baada ya muda. Ingawa, wazushi wanaziharibu nyoyo tokea hapo mwanzo.’ [13]
Jihaad yake dhidi ya Wakiristo na Raafidhah (Mashia)
Ibn Taymiyyah ameandika Al-Jawaab as-Swahiyh Liman Baddala Diyn al-Masiyh katika vitabu (mijalada) vinne ambavyo ndani yake aliweza kuzielezea pingamizi zote zilizotolewa dhidi ya Uislamu, aliweka bayana hoja kamili mpya na zenye kuridhisha kwa kuegemea Sunnah ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Moja kati ya waliomuandikia wasifu wake Shaykh al-Islaam, ni Shaykh Abu Zahrah, aliyesema: “Kitabu hichi peke yake kinatosha kutoa nafasi kwa ajili yake miongoni mwa wataalamu na madukturi wasomi ambao walitia bidii ya kuisafisha imani.”[14]
Kama kilivyo Al-Jawaab as-Swahiyh, Minhaaj as-Sunnah ni kazi nyengine ya kipekee ya Ibn Taymiyyah ya juu kabisa ambayo ameandika kukana matabaka ya Kishia hapo zamani (na leo) yanayohatarisha ukakamavu wa imani sahihi ya kiasili. Kitabu hicho, chenye vijitabu (mijalada) vinne hadi nane na chenye kurasa zaidi ya 1,600; kimeandikwa kukijibu kitabu cha Minhaaj al-Karaaman cha Ibn al-Muttahir al-Hilliy ambaye, katika hamu yake iliyochupa mpaka, akataka kuthibitisha Utukufu uliopo kwa nafasi ya Kiiimamu (Imamu 12 wa Kishia), akajaribu kuwafanya Makhalifa waongofu watatu wa mwanzo kuwa ni wanafiki na walioritadi na pia kama ni viumbe viovu kabisa vilivyojiingiza kwenye unyanyasaji. Hili, kwa mujibu wa Ibn Taymiyyah, iliushushia hadhi Uislamu na kuifanya dhana ya Utume kuwa ni dhaifu. Hata kwa msingi wa ubishano wake, Minhaaj as-Sunnah ni kitabu muhimu kutokana na mtindo wake ulio wazi na hoja kali kali na maelezo yake ya kuridhisha na usahihi wake.
Nukuu nyingi hazielezi nafasi ya Ibn Taymiyyah kwenye Jihaad dhidi ya Wakiristo kabla ya kufukuzwa kwao nchini Shaam. Hata hivyo Imaam Al-Bazzaar, anataja yafuatayo pale anapojadili ukakamavu na moyo uliopigwa konde wa Ibn Taymiyyah: “Wananasibisha kwamba walimuona katika utekaji wa ‘Akkah, katika muonekano wa kishujaa ambao hauwezi kuelezeka. Wanasema kwamba alikuwa ndio chanzo ya sababu ya kutekwa (‘Akkah) na Waislamu kwa sababu ya matendo yake (mema), na ushauri na muono wake mkali.”[15]
Ama kwa Maraafidhah, walijijengea ngome yao wenyewe katika milima ya al-Jard na al-Kasrawaaniy. Ibn Taymiyyah akawafuata huko ndani ya mwaka 704H akiwa pamoja na kundi la wafuasi wake na kuwataka idadi yao kadhaa kuomba toba na (hivyo) wakasimamisha Shari’ah ya Uislamu juu yao (Maraafidhah). Mwanzoni mwa mwaka 705H, Ibn Taymiyyah alikwenda vitani akiwa pamoja na kundi la kivita na naibu Sultaan wa Shaam na Allaah Akawasaidia wao dhidi ya Maraafidhah.[16]
Jihaad Yake Dhidi Ya Ma-Tartar
Ibn Taymiyyah alikuwa na nafasi kubwa katika kuanzisha Jihaad dhidi ya ma-Tartar. Aliweka wazi ukweli wa masharti yao na kuonesha kwamba ilikuwa ni wajibu kupigana nao, kwanza, kwa sababu ya makubaliano ya Wanachuoni katika wajibu wa kupigana vita na kundi lolote ambalo linakana waziwazi na kukataa Shari’ah za Uislamu na pili, akieleza kwamba kanuni hii inafanya kazi kwa Tartar kwa sababu ya masharti yao.
Aliweka wazi sababu za ushindi na kueleza kwamba sio jambo lisilowezekana au lenye ugumu kupata ushindi dhidi yao iwapo Waislamu watafuata sababu za kupata ushindi kama vile kusimamisha Shari’ah, kuondosha unyanyasaji, kueneza haki na kuwa wakweli kwa niyah zao pale wanaposimamisha Jihaad katika njia ya Allaah.
Ibn Taymiyyah alichukua jukumu la kuyafunza majeshi na kuanzisha makundi ya Mujaahidiyn. Alihusika pia katika mavamizi ya kushtukiza dhidi ya kambi za kijeshi za Tartar. Pia alizamia jimbo ambalo watu wa Baatwiniyah (wenye itikadi ya Kishia) wakiishi katika milima ya Shaam, kwa sababu waliwasaliti Waislamu na kwa siri walishirikiana na maadui wa Uislamu, Matartar na Makrusedi. Ingawa dhehebu la Kibatini lilifanikiwa kumlaghai Ibn Taymiyyah pale walipojifanya kutubia na kuzikataa imani na mila zao mbovu. Lakini alitambua kwamba walimcheza kwa kutumia taqqiyah,[17] na kwamba walibakia kwenye uadui wao kwa Uislamu na Waislamu. Hakuacha kuwapiga vita na kuwasaka, na alitoa fatwa akiweka wazi imani zao zilizojificha na vitendo vyao viovu na akaamrisha haja ya kupigana vita nao.
Kwa upande mwengine, hakupatapo kuridhia ukweli pale anapojadiliana na watoto wa kifalme na wafalme kutokana na dharau zao katika kuihami ardhi ya Uislamu dhidi ya maadui wa ndani na nje. Hili linaonesha dhahiri kupitia barua yake kwa Sultaan an-Naaswir Muhammad Ibn Qalawuun. Ndani ya barua hiyo, alitishia kuendeleza taifa litakalojitenga kutoka katika utawala wa Kisultani, na kuutoa uaminifu wake kwa kiongozi mwengine ambaye hatoacha kuhami na kusimama dhidi ya uvamizi wa Matartar.
Pale mji wa Damascus ulipoanguka kwa mara nyengine ya pili kwa Matartar, Ibn Taymiyyah alikataa kusimama kwa kujishushuia hadhi, kwani alikubaliana pamoja na viongozi wa nchi hiyo kuchukua hatua muhimu kwa ajili ya ustawi wa Waislamu kwa kukutana na kiongozi wa Matartar. Ingawa walikuwa hawana nguvu kujihami wenyewe, hata hivyo alichukua hatua ya dharura katika kuhamasisha kuonana na Sultaan wa Matartar aitwaye Ghaazaan, akimuomba usalama wa watu wa Damascus bila ya kuisalimisha ngome yao. Hakuwa na moyo wenye kukubali na ulio na ujinga kama walivyo mashaykh wengine waliokutana na Ghaazaan wakimuomba msamaha na kuwakubali kwao. Lakini alikabiliana nae Ghaazaan uso kwa uso na kumuelezea kwamba uvamizi wa Damascus hautakuwa mrefu kwani Waislamu wanaendelea kupindua. Usalama ukapatikana kwa Waislamu wa Damascus kutokana na juhudi ya ukakamavu na ushujaa wa Ibn Taymiyyah.
Ibn Taymiyyah pia alishirikiana na Sultan an-Naaswir Ibn Qalawuun katika vita vyake dhidi ya Ghaazaan aliyedai kuwa ni Muislamu na kujipachika jina lake la Mahmuud. Ilithibitika kwa Ibn Taymiyyah kuwa vyenginevyo, kwa sababu Ghaazaan alikataa moja kwa moja kusimamisha Shar’iah za Kiislamu na hakuwa mwenye kuzithamini Shar’iah za Allaah. Alitawala nchi kwa kutumia kitabu cha al-Yaasiq ambacho kilikuwa na mchanganyiko wa shari’ah kutoka Ukiristo, Uyahudi, Uislamu na sheria za Genghis Khan mwenyewe. Alizikataa Shar’iah zilizoshushwa kwa Waislamu ndani ya Qur-aan na Sunnah.
Katika mwaka 702H, habari kuhusiana na kurejea kwa Matartar mjini Shaam zikaenea. Ibn Taymiyyah akafanya haraka kwenda kwa Sultaan wa Misri kuomba msaada dhidi ya hatari za Matartar na ubepari wao uliokuwa maarufu sana, haswa pale watawala wa Allepo na Hama walipoitupa miji yao na kukimbilia Damascus. Pale Matartar walipofikia Homs na Ba’lbek, Ibn Taymiyyah akaajiri mabaki ya jeshi ambalo liliondoka Hama na miji mengine. Aliliunganisha jeshi na kuanza kuandamana kwenda Damascus ili kuwa mbele katika daraja, hadi majeshi ya Khaliyfah al-Mustakfi na Sultaan an-Naaswir Ibn Qalawuun yalipofikia Damascus. Siku ya Jumamosi, Ramadhwaan ya pili, jeshi la Waislamu likawa limekamilika, na mashirikiano kwa ajili ya vita yalikuwa yameshaanza nje ya Damascus ili kuulinda mji huo kutokana na madhara yoyote. Eneo la vita lilikuwa ni Marj as-Safar.
Pale Matartar waliposikia kwamba jeshi kubwa linakuja, wakafanya haraka kukutana nao nje ya Damascus. Hivyo, mpango wa mwanzo wa Ibn Taymiyyah ukawa umefanikiwa kwani aliwazuia Matartar kufanya uharibifu zaidi wa mji. Kwani umuhimu wa mwanzo wa Matartar ulikuwa ni kuliharibu jeshi la Waislamu, (lakini walishindwa kufanya hivyo) wakauacha mji (wa Damascus) bila ya uchokozi.
Majeshi hayo mawili baadaye yakakutana, kila moja likiwa na mawazo kichwani mwake ya kuliharibu jeshi la mwengine, na vita vikaanza mara moja. Ilikuwa ni wakati wa adhuhuri na Waislamu ndani ya vita hivyo walikuwa wamefunga siku hiyo katika vita vya Shaqhab, vilivyopiganwa ndani ya mwezi wa Ramadhwaan. Ibn Taymiyyah akawaamuru kufungua Swawm kwa kufuata muongozo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kila mmoja wao aliomba kutoka kwa Allaah aidha Shahaadah au ushindi. Ndani ya fikra zao ni Swahaba wa Nabiy (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na warithi wao waongofu (Mataabi’iyn). Wasiwasi wao wa mwanzo ulikuwa ni kuuhami Uislamu na kuuharibu uadui wa Matartar kwa namna yoyote, wakihakikisha kwamba hawatojaribu kurudi tena katika ardhi ya Uislamu kwa ufisadi wao, tofauti na ilivyokuwa mara ya mwanzo pale Matartar walipojitengenezea makundi mapya, yao wenyewe, baada ya kushindwa katika vita vya A’in Jaluut na kurudi katika uvamizi wa ardhi za Waislamu.
Shaykh al-Islaam alikuwa ni kiongozi wa jeshi, akiyatengeneza vyema malengo ya Waislamu, ingawa kwa upande mwengine hupigana na adui kwa ushujaa, akiwasukuma nyuma kurudi majumbani kwa kutambaa, wakawavunja Matartar, wakiizuia hatari yao na kuwaondoa Waislamu mbali na matishio yao. Hatimaye, wakaliacha jeshi la adui likiwa halina matarajio yoyote daima kurejea katika ardhi ya Uislamu. Mapigano ya Shaqhab yalikuwa ni mapigano ya mwisho kabisa baina ya Matartar na Waislamu.
Baada ya kufanya Jihaad dhidi ya Matartar na kuwashinda, tunamuona Ibn Taymiyyah akithamini vita hivyo, akichambua mafunzo ya kimanufaa ambayo yanaweza kufikiwa kutokana na mapigano hayo na kuelezea maeneo ya ulinganishi baina ya mapigano hayo dhidi ya Matartar na mapigano mengine ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).[18]
Mapigano yalikuwa na nafasi kuu katika majibu ya Ibn Taymiyyah kwa wale waliojaribu kumzuia na kuvunja nguvu makubaliano ya Waislamu. Walikuwa wakijaribu aidha kuwatisha Waislamu kwa kukithirisha mno uwezo na nguvu za adui, au wakidai kwamba Matartar ni Waislamu, na hivyo, kuwa ni udhuru wa kutopigana nao. Majibu ya Ibn Taymiyyah kwa Waislamu, ambao waliweza kurubuniwa na yale yaliyosemwa kuhusiana na kutowajibika kupigana na Matartar, yalikuwa ni maneno yake: “Iwapo mutanikuta mimi katika hadhi ya Matartar basi niueni!”
Jibu lake katika uwanja wa vita lilikuwa wazi na kwamba alianza kuwapiga vita Matartar, hivyo kutoacha nafasi ya Waislamu waliorubuniwa au waliokuwa na mawazo mengine kuhusiana na maamuzi muafaka katika kumpiga vita adui.
Hizo ni baadhi ya mifano ya Jihaad ya Ibn Taymiyyah, Allaah Amshushie rehema Zake, na uunganishi wake wa elimu pamoja na vitendo.
Mitihani na Kufungwa kwa Ibn Taymiyyah[19]
Ibn Taymiyyah alipitia mitihani mingi katika maisha yake na ni kazi ngumu kuipitia na kuielezea kwa namna nzuri ndani ya utafiti huu mfupi kuhusiana na yeye. Hivyo, nitataja tu orodha ya ile mitihani maarufu.
-Mtihani alioupata kwa sababu ya maandiko yake ya al-Hamawiyyah katika mwaka 698H.
-Mtihani alioupata kwa majadiliano yake kwa sababu ya maandiko ya al-Waasitwiyyah katika mwaka 705H.
-Mtihani alioupata kwa kuitwa kwake Misri na kufungwa katika mwaka 705H kwa miezi 18.
-Mtihani alioupata pamoja na Suufiyyah (Masufi waliomchongea kwa Kiongozi wa nchi) nchini Misri baada ya kuachiwa huru.
-Kufukuzwa kwake kwenda Alexandria katika mwaka 709H na kufungwa huko kwa miezi 8.
-Mtihani alioupata kwa sababu ya maamuzi mahsusi kuhusiana na talaka na kufuatiwa na kifungo katika mwaka 720H, kwa miezi mitano.
-Mtihani alioupata kwa sababu ya maamuzi yake ya Kishari’ah kuzuia kufanyika misafara mahsusi kuyazuru makaburi na kufuatiwa na kifungo katika mwaka 726H hadi kufa kwake katika mwaka 728H, Allaah amshushie rehema zake.
Majibu ya Ibn Taymiyyah kuhusiana na mitihani yote hii aliyokabiliana nayo yalikuwa daima ni majibu ya uhakika ambayo yaliyageuza mithani hii na madhara – kwa msaada wa Allaah – kuwa ni nafasi kuu ya kuiongeza Iymaan na kufikia pasipo na shaka katika maarifa na matendo.
Uitwaji wake nchini Misri, kwa mfano, ulimfanya kujadiliana na kuendelea na kuwaelezea wazushi ambao walieneza imani zao katika kila pembe ya nchi. Kutupwa kwake katika kifungo (jela) ilikuwa ni alama nyengine ya Baraka hii, kwani jitihada zake katika kuelimisha wafungwa na kuwalainisha hadi kufikia hatua ya kwamba utoaji wa elimu na Diyn ndani ya jela ulizidi baadhi ya taasisi zilizo nje ya jela. Hili lilitokezea kote; Misri (Cairo) na Alexandria. Uamuzi wake wa kubakia Misri baada ya kuachiwa ilikuwa kama alivyoelezea ndani ya barua[20] kwa mama yake, kwa sababu ya mambo muhimu kwa Diyn na dunia. Hili lilileta uzuri zaidi katika kusaidia Sunnah na kuwadidimiza wazushi. Moja kati ya matokeo ya uhakika ilikuwa ni vitabu na nyaraka alizoandika na alizotunga ndani ya jela. Pia aliwaomba radhi wale waliomdumaza, hata pale Ibn Taymiyyah alipopata nafasi ya kulipiza kisasi haswa. Mmoja miongoni mwa maadui zake, Ibn al-Makhluuf, Jaji wa ki-Maalikiy aliyesema: “Hatujaona mfano wa Ibn Taymiyyah; tulimlaghai lakini hatukuwa na uwezo kumzidi nguvu, pale alipokuwa na uwezo wa kutuzidi sisi nguvu, badala yake alituombea msamaha na kutuhami kwa niaba yetu.” [21]
Matokeo yake mengine ya uhakika ni kwamba mitihani hii ndani yake wenyewe yalikuwa ni sababu ya kuenea kwa kasi mno kazi za Ibn Taymiyyah.[22]
Kifo chake, Allaah Amshushie Rehema Zake juu yake
Hatimaye pale alipopigwa marufuku kuwa na kitabu chochote, karatasi au kalamu akiwa katika kipindi chake cha mwisho cha jela, Ibn Taymiyyah akajitolea muda wake wote katika kufanya ‘Ibaadah na kusoma Qur-aan. Alibakia katika hali hii kwa kipindi kifupi hadi alipoaga dunia mnamo tarehe ishirini Dhul-Qa’dah mwaka wa 728H. Aliugua kwa siku chache ambazo zilipelekea kifo chake.
Hili lilikuja kuwa ni mshituko mkubwa kwa watu na walitoka nje kwa idadi kubwa.
Wanahistoria wanakadiria kwamba kifo hichi ni moja kati ya mazishi machache na walilinganisha na mazishi ya Imaam Ahmad Ibn Hanbal, Allaah Awe radhi naye.
Ibn Taymiyyah alifariki kipindi alichokuwa kifungoni, kwa chuki na fitna alizotiwa Sultaan kutoka kwa wale maulamaa waliokuwa nwakimshindwa kielimu na wenye husda na mafanikio yake makubwa ya kielimu, kiucha Mungu, kiutendaji, kiufuasi na kukubalika kwake. Vilevile fitna tele za Masufi waliokuwa wakitaja mambo mengi kuhusiana naye kutokana nay eye kuwapinga uzushi na upotofu wao wa Diyn.
Hata hivyo, ukiachilia mbali hayo, mazishi yake yalishuhudiwa na wengi na yalikuwa ni maarufu na makubwa sana.
Imaam Al-Bazzaar amesema:
“Mara tu watu waliposikia kifo chake, hakuna mtu hata mmoja aliyetaka kuwepo Damascus ambaye alikuwa na uwezo wa kuhudhuria Swalah na alitaka kubakia hadi alipohudhuria na kutoa muda kwa ajili hiyo. Matokea yake, masoko ya Damascus zikafungwa na shughuli zote za kimaisha zikasimama. Magavana, wakuu, Wanachuoni (Maulamaa) walitoka nje. Walisema kwamba hakuna wingi wa watu ulioacha kufika, kwa mujibu wa ufahamu wangu – isipokuwa watu watatu tu ndio hawakuhudhuria; hao watatu walikuwa wakitambulika kwa uadui wao dhidi ya Ibn Taymiyyah, walijificha wasionekane na watu kutokana na hofu ya maisha yao.” [23]
Ibn Kathiyr ametaja kwamba naibu Sultaan hakuwepo na Taifa likajiinamia kwa lipi la kufanya. Kisha naibu wa jela akaja kutoa rambirambi zake na kukaa karibu na Ibn Taymiyyah. Aliwafungulia njia wale Maswahibu wa karibu na watu wapenzi kuingia kumuona. Wakakaa pamoja naye, wakilia na kumshukuru.[24] “Kisha wakaanza kumuosha Shaykh… wakawaruhusu wale tu ambao waliosaidia katika kuosha kubakia pamoja naye. Miongoni mwao alikuwa ni Shaykh al-Haafidh al-Mizziy na kundi la waongofu wakuu na watu wema; watu wa elimu na Iymaan… kisha wakatangulia pamoja naye kwenye Jaami’ al-Umawiy. Kulikuwa na watu wengi mbele ya janaazah, nyuma yake, kwa upande wa kulia na kwa upande wa kushoto. Hakuna isipokuwa Allaah Aliyeweza kuwahesabu, kisha mtu mmoja akapiga ukulele “Hivi ndivyo yanavyotakiwa majeneza ya Maimamu wa Kisunnah!” Kwa hilo, watu, wakaanza kulia… pale adhana ya adhuhuri ilipoadhiniwa wakaswali hapo hapo kisunnah na kinyume na namna ya mila zilizozoeleka. Pale walipomaliza kuswali, naibu Khatwiyb akatoka – kwani khatwiyb mkuu alikuwa hayupo alikuwa Misri – na akaongoza Swalah juu ya Ibn Taymiyyah… Kisha watu wakamiminika kutoka kila pembe na milango yote ya Jaam’i… na wakakusanyika katika soko la al-Khayl.” [25]
Katika ardhi iliyo wazi, jeneza lake likaingizwa chini na ndugu yake, ‘Abdur-Rahmaan, akaongoza Swalah yake. Kisha jeneza lake likachukuliwa kaburini mwake na kuzikwa kwenye sehemu ya makaburi karibu na ndugu yake wa kiume, ‘Abdullaah, Allaah Awashushie rehema zake wote hao.
Imaam Al-Bazzaar amesema:
Kundi la watu waliokuwepo siku hiyo wamekubaliana kwamba walipoona idadi ya watu waliomswalia siku hiyo, hakuna wasiwasi wote kwamba walikuwa zaidi ya 500,000. Wataalamu wa historia wanasema kwamba hawakupata kusikia Swalah ya mazishi kuwa ni kubwa kama hivi isipokuwa ili Swalah ya jeneza al-Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaahu).[26] Hatimaye Shamsud-Diyn al-Waziyr akatokezea na kupelekwa pale liliopo kaburi lake, kwa kuwa hakuwepo hapo kabla, hivyo yeye na magavana pamoja naye wakamswalia Ibn Taymiyyah.
Hakuna jeneza ambalo limeonekana kuathiri hisia za watu katika heshima, ustahifu, ufakhari, uthamini, na shukrani kutoka kwa watu, na yote haya ni kutokana na elimu yake, matendo, zuhd, ‘ibaadah, ukataaji wa dunia, kushughulishwa na Akhera, umasikini wake, kujali, ukarimu, ujanadume, ustahamilivu, msimamo, ushujaa, uoni wa mbali, kuwa muwazi katika kuzungumzia ukweli, kuwa mkali dhidi ya maadui wa Allaah na Nabiy Wake na Diyn Yake, ubinaadamu wake, taadhima, na heshima mbele ya awliya’ wa Allaah, kutotilia maanani mazuri ya dunia, hamu yake ya kupindukia kwa ajili ya Akhera, na utafutaji wake wa hiyo Akhera usiochoka. Na utayasikia mambo haya na zaidi kutoka kwa wanaume, wanawake, na watoto, na wote humsifu kutokana na vile walivyokuwa wakimjua.
Alizikwa siku hiyo (Allaah Awe radhi naye). Kisha watu wakaanza kujikusanya kutoka vijiji na miji mbalimbali wakiwa wengine kwenye vipando wengine kwa miguu kumswalia kwa zamu juu ya kaburi lake, na kila habari za kifo chake zinapoifikia ardhi fulani, humswalia ndani ya Misikiti yake yote, haswa ndani ya miji na vijiji vya Misri, Shaam, Iraaq, Tabriz, al-Basrah, n.k.
Haya yote ni kutokana na namna walivyohisi kuwa na deni mbele ya Shaykh (Allaah Amshushie rehema zake) kwa kuwaongoza kwenye ukweli na taratibu sahihi pamoja na ushahidi wa wazi, ushahidi wa maandiko na elimu, haswa kwa mnasaba wa kanuni za Diyn. Allaah Aliwabariki Qawm hii ambapo uzushi uliibuka ambao uliuuwa Sunnah, na idadi kubwa ya watu walizama kwenye uzushi na haraam katika hali ambayo hawakubutika kabisa! Na Allaah Akawabariki kwa kuwa naye kudhihirisha kanuni za Diyn na ukweli na imani sahihi kwao, na halikadhalika namna yake mahsusi ya kuwapinga wazushi ambayo haijaonekana kwa zaidi yake. Yote haya yalifanywa kwa mdomo wake, kalamu yake, vitabu vyake, na kanuni alizojifunga nazo kuzifuata ambazo zilikubaliana na ukweli na maana halisi, na pia uwazi, maandiko mepesi na ushahidi wa kielimu aliowasilisha ambao hakuna filosofa hata mmoja au wahoji waliomweza au kumkaribia kwa hoja. Yote haya aliyafanya hadi alipokuwa na uwezo wa kuingiza uwezo wake wote na kumtawala kila mzushi, na alikuwa na uwezo wa kuweka wazi na kufuta kila dhana ambazo zilisimamishwa na wakiomba kuzieneza.[27]
Tunamuomba Allaah Amlipe yeye kwa malipo bora kwa niaba ya Uislamu na Waislamu, Ametukuka Yule ambaye Amempa yale aliyokuwa nayo, akampatia uongofu bora kwa yale aliyoongoka nayo, na kumpatia yeye subira nzuri kabisa hadi kufariki kwake, na tunamuomba Allaah Awe Radhi naye, na Atupatie sisi na Waislamu wote maisha na kifo kinachoendana pamoja na Qur-aan na Yeye, na atujaalie sisi kushikamana vilivyo na wote hao kwenye yote waliyokuwa nayo, na tunamuomba Allaah Atujaalie sisi na wale wa baada yake kunufaika na elimu yake.
[1] Nahiyyah min Shaykhul-lslaam Ibn Taymiyyah, uk. 10-11; al-Bidaayah wa an-Nihaayah, 13/34; as-Suluuk li Ma'rifah Duwal al-Muluuk cha al-Miqriyziy, na Badaa'i' az-Zuhuur fiy Waqaa'i' ad-Duhuur cha Muhammad Ibn Ahmad Ibn 'Iyaas al-Hanafiy
[2] Rudia katika Ra-s al-Husayn cha Ibn Taymiyyah kilichoandikwa kwenye Majmu’ 'al-Fataawaa, Sura ya 27 na pia 17/500, 27/173 na 27/61 katika mada ya kaburi la Nuuh.
[3] Risaalah al-Qubrussiyah ya Ibn Taymiyyah, ndani ya Majmu’ al-Fataawaa, Sura ya 28. Hii inapatikana ikiwa na tafsiri pamoja na barua kadhaa za Ibn Taymiyyah: Barua za Ibn Taymiyyah kutoka Jela, kimechapishwa na Ujumbe wa Uislamu (Message of Islam), U.K.
[4] Al-Jawaab as-Swahiyh li man Baddala Diyn al-Masiyh cha Ibn Taymiyyah, 2/172.
[5] Wanatambulika kama ni al-Ahmadiyyah na ar-Rufaa’iyyah kutokana na kujisifia kwao kwa muanzilishi wao Ahmad ar-Rufaa’iy, mzaliwa kutoka kijiji kimoja cha al-Bataa’ih.
[6] Imaam ash-Shaafi’iy (Rahimahu Allaahu), amesema: “Iwapo umeona mtu anatembea juu ya maji au akiruka ndani ya anga, basi usimuamini hadi uhakikishe kisawasawa ukweli na kujinasibu kwake mbele ya Sunnah.”
[7] Majmu’ al-Fataawaa, 11/456-457, al-'Uquud ad-Durriyyah, uk.194 na al-Bidaayah wa an-Nihaayah 14/36.
[8] Al-Bidaayah wa an-Nihaayah, 14/122-123. Baadhi ya matokeo ambayo Shaykh alishiriki yalikuwa bila ya shaka yakifanyika kwa muongozo wa misingi iliyoshikamana na uamrishaji mema na ukatazaji maovu. Yeye mwenyewe Ibn Taymiyyah amejadili miongozo hiyo katika kijitabu chake cha al-Amr bil-Ma'ruuf wan-Nahy 'anil-Munkar.
[9] Al-Uquud ad-Durriyyah, pg. 281; al-Bidaayah wa an-Nihaayah, 14/54; al-Kawaakib ad-Durriyyah, uk. 138.
[10] Al-Bidaayah wa an-Nihaayah, 14/66.
[11] Majmu’ al-Fataawaa, (11/456-457), na al-Bidayah wan-Nihayah (14/36)
[12] Imetokana na ridhaa ya Ibn Hajr iliyopo mwisho mwa kitabu cha 'Radd al-Waafir'.
[13] Majmu’ al-Fataawaa (28/231-232) Imenukuliwa kutoka kwenye jarida la al-Istiqaamah Magazine, iliyonukuliwa kutoka Jarida la As-Sunnah Newsletter – http://www.qsep.com
[14] Ibn Taymiyyah, Hayaatuhu wa ‘Aswruhu wa Araauhu wa Fiqhuhu, uk. 519.
[15] Al'-Alaam al-'Aliyyah, uk. 68.
[16] Al-'Uquud ad-Durriyyah, uk. 179-194, al-Bidaayah wa an-Nihaayah, 14/35 na as-Suluuk, 12/2.
[17] Taqiyyah (التقية) inatafsirikia kilugha kama “kuzungumza kinyume na imani ya ndani ya mtu.” Historia yote (inaonesha kwamba), Mashia wameitumia Taqiyyah kwa ajili ya kuepuka uchunguzi na kuepuka kukamatwa. Tendo la Taqiyyah linawaruhusu makundi ya Mashia kuenea na kukua. Kwa mujibu wa Mwanachuoni wa Kishia: “Ushia usingelienea iwapo kusingelikuwepo Taqiyyah.” (“Taaarikhush Shi’ah” cha Muhammad Husain Ja’far Sahiwal, uk.230). Imamu wa Kishia amesema kwamba Taqiyyah ni: “Kujichanganya pamoja nao (yaani wasiokuwa Mashia) kinjenje lakini kuwapinga kindanindani.” (Al-Kaafi, sura 9, uk.116).
[18] Al-'Uquud ad-Durriyyah, uk. 121.
[19] Imechukuliwa kupitia mtandao
http://www.sunnahonline.com/ilm/seerah/0047.ht iliyoandaliwa na Abu Safwaan Fariyd
[20] Barua, Ibn Taymiyyah’s letters kutoka Jela.
[21] Al-Bidaayah wan-Nihaayah, 14/54.
[22] Al-'Uquud ad-Durriyyah, uk. 283.
[23] Al-A'laam al-'Aliyyah, uk. 82-83
[24] Al-Bidaayah wa an-Nihaayah, 14/138.
[25] Al-Bidaayah wa an-Nihaayah, 14/138.
[26] Katika ‘al-Bidaayah wan-Nihaayah’ (14/130), Ibn Kathiyr amesema: “Ahmad bin Hanbal amesema: “Waambie wazushi kwamba baina yetu na yao ni mazishi,” na hakuna shaka yoyote kwamba mazishi ya al-Imaam Ahmad yalikuwa na watu wengi na makubwa kwa namna na wingi wa watu wa mji huo ulivyokuwa, na namna ya watu walivyojikusanya kwa ajili yake na kumuheshimu, na serikali ikimpenda. Shaykh Taqiyud-Diyn amefariki ndani ya ardhi ya Damascus, na idadi ya watu wake haikufikia karibu na ile ya Baghdad kwa ukubwa. Hata hivyo, walijikusanya kwa idadi kuwa kwa mazishi yake hadi kufikia kwamba iwapo mtawala angeliwalazimisha watu wote kutoka nje, wasingelifikia kutoka nje katika idadi kubwa kama ilivyoonekana siku hiyo, na haya yote ni kwa mtu aliyefariki ndani ya ngome ya jela kwa amri ya mtawala.”
[27] The Lofty Virtues of Ibn Taymiyyah, ukurasa wa 7.