08-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Yeyote Anayechukua Kutoka Kwa Maswahaba Bila Shaka Amechukua Kutoka Kwenye Qur-aan

 

Yeyote Anayechukua Kutoka Kwa Maswahaba Bila Shaka Amechukua Kutoka Kwenye Qur-aan

 

Maswahaba wa Mtume walijifunza kutoka kwa makhalifah wanne –Allaah Awawie radhi wote. Kwa vizazi mbalimbali, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alitoa ushahidi wa Iymaan yao na Alituonya tusifuate njia nyingine isipokuwa njia yao. Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) anasema

“Na anayempinga Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu, na akafuata njia isiyokuwa ya Waumini, tutamuelekeza alikoelekea, na tutamuingiza katika Jahannamu. Na hayo ni marejeo maovu.” (4: 115).

 

Na katika Hadiyth:

 

“Kwa hakika watu waliokuwepo kabla yenu miongoni mwa watu na kitabu waligawika makundi (madhehebu) sabini na mawili, na bila shaka wafuasi wa dini hii watagawika katika madhehebu sabini na tatu, sabini na mbili wataingizwa Motoni, ambapo moja litakuwa Peponi: nalo ni Jama’ah.”[1]

 

Katika Hadiyth nyingine, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilielezea kundi lililookolewa kama ifuatavyo:

“Ni lile ambalo Mimi na Maswahaba wangu tumo.”[2]

 

Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alisimulia yafuatayo:

“Msiwalaani Maswahaba wa Muhammad; kwani kisimamo cha mmoja wao kwa saa moja ni bora kuliko ‘amali iliyofanywa na mmoja wenu katika maisha yake.”[3]

 

Mpaka hapo tulipofika lazima tubaini muunganiko: Maswahaba walipokea kutoka kwa Makhalifah waongofu (na kutoka kwenye Sunnah), waliofuata Sunnah, na kama tulivyoona kabla, kufuata Sunnah ni kufuata Qur-aan Takatifu. Kwa hiyo, kupitia kiungo hiki, tunaweza kuhitimisha ya kuwa Yeyote aliyechukua kutoka kwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) amechukua kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala); na yeyote anayekataa njia ya Maswahaba kwa hakika amekana Kitabu cha Allaah, ukweli unaoonyesha upotovu na kukinzana kwa wale waliowatangaza Maswahaba- ukiacha watatu miongoni mwao - kuwa ni makafiri (na tunaomba hifadhi ya Allaah!).

 

Wale wanaowaita Maswahaba makafiri, wao ndio wasioamini Qur-aan na Sunnah, na wameachwa bila vigezo sahihi vya kuendesha maisha yao. Wale wasio katika njia sahihi wamepotoka kwa sababu hawashikamani na njia ya watangulizi wema; badala yake wanafuata akili zao kuifahamu Qur-aan na Sunnah. Na kwa sababu hiyo mapote na fikra na madhehebu yamekuwa mengi, na kila moja likisema, “Tunafuata Qur-aan na Sunnah”, Kwa bahati mbaya si wa kweli katika madai yao.

 

 



[1] Ilisimuliwa na Abu Daawuud, Ad-Daarimiy, Ahmad na wengine –Rejea, As-Swahiyhah (204).

[2] Silsilah yake ni Hasan na masimulizi mengine yanathibitisha kwayo, hukmu yake imetajwa ndani ya As-Swahiyhah (203, 204).

[3] Ilisimuliwa na Ibn Abi ‘Aaswim katika Kitabus-Sunnah, wasimulizi katika Silsilah ni waaminifu, wengine zaidi ya Naaswir Bin Dhu’luq, ni wasimulizi wa Al-Bukhaariy na Muslim. Na maimamu wengi wamemtangaza Naaswir kuwa mwaminifu, bila kutaja ya kuwa wapokezi wengi waaminifu walipokea kutoka kwake. Shaykh wetu Al-Albaaniy – Allaah Amrehemu, ametaja hili katika kitabu kilichotajwa (Hadiyth Na. 1006).

Share